SAKATA la usajili wa mshambuliaji wa Mbeya City, Saady Kipanga, kwenda Simba, limechukua sura mpya baada ya viongozi wa klabu hiyo kushindwa kuelewana kwa maelezo kwamba kigogo mmoja amemsajili kibabe bila wenzake kuridhia.
Awali viongozi wa Kamati ya Usajili kwa ushirikiano na viongozi wengine wa Simba, walikubaliana kufuta usajili wa mchezaji huyo. Lakini baadaye mmoja wa vigogo hao (jina tunalo) aliliibua suala hilo upya juzi Jumatano kwa madai kuwa tayari amemsainisha Kipanga mkataba wa miaka miwili.
Siku hiyo kamati hiyo ilikutana kujadili mustakabali mzima wa usajili na kufunga kazi hiyo ili kocha apate muda wa kukaa na wachezaji husika, lakini ishu ya Kipanga ikatibua uelekeo wa kikao. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Suala hilo lilionekana kuwagawa baadhi ya wajumbe wa kamati ambapo walio wengi walionekana kupinga juu ya usajili huo huku wajumbe watatu pekee wenye ushawishi wa kifedha wakiunga mkono. Wajumbe wengi walikuwa wakimtaka Elius Maguli ambaye yupo kwenye orodha ya matakwa ya kocha.
Mbeya City watoa tamko
Uongozi wa Mbeya City umesema kuwa ulipokea barua ya kiongozi mmoja wa juu wa Simba juu ya maombi ya usajili wa Kipanga, Deus Kaseke na Anthony Matogolo na kuwapa masharti ya kutimiza.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe, alisema baada ya kuijibu barua hiyo ya Simba, hawakupokea mwendelezo wowote wa mawasiliano juu ya usajili hivyo wanashangaa kusikia Kipanga kasajiliwa Simba wakati bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na klabu hiyo na kama ni kweli watashtaki.
“Kuna barua ilitumwa kutoka Simba na tuliwajibu, lakini hakuna majibu yaliyorudi kutoka kwao, hivyo tunasubiri itakuwaje maana tunasikia tu kuwa wamemsajili, huo utakuwa usajili wa kinyemela na uvunjaji wa kanuni za usajili, sisi tumewasiliana na TFF juu ya hilo.
“Kanuni zipo wazi huwezi kufanya mazungumzo na mchezaji ambaye ana mkataba kuanzia mwaka mmoja na klabu nyingine labda angebakiza miezi sita, wachezaji wetu wanatakiwa kufika kambini, Kipanga ni mmoja wao,” alisema Kimbe.
Kuhusiana na usajili wa Maguli ndani ya Simba, Mwanaspoti linajua kwamba Wekundu wa Msimbazi hao wameshatuma ofa Ruvu Shooting. Jana Alhamisi walitarajia kumalizana naye huku uongozi wake ukikiri kupokea barua kutoka Simba.
“Tunakutana viongozi kujadili, lakini hatuwezi kumzuia mchezaji ambaye ameonyesha nia ya kwenda kucheza timu yoyote kwani tukimzuia hatafanya vizuri kwetu, Simba wametuma barua lakini haina ofa yoyote ila tutamruhusu akachezea Simba kwani ndio timu aliyoipenda, naamini tutakubaliana na hatuwezi kuwakomoa kwa kutaka fedha nyingi,” alisema Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire.
Post a Comment