0
Shem Karenga HIVI KARIBUNI KABLA YA KIFO CHAKE 
 
shemkarenga enzi za ujana wake 

Hakuna mpenzi ama shabiki wa miondoko ya muziki, hususan wa dansi hapa nchini, asiyelifahamu jina la mwanamuziki mkongwe, Shem Ibrahim Karenga. Shem Karenga ametokea kuwa maarufu mno hapa nchini pamoja na mataifa kadhaa jirani, kutokana na umahiri wake wa miaka mingi wa kuimba na kucharaza gitaa kiongozi la Solo.

Wengine wengi wanamfahamu kupitia tungo zake mbalimbali zilizochangia kumpa umarufu, alizozifyatua akiwa na bendi hizi na zile, kama vile ‘Tucheze Segere’, ‘Muna’, ‘Kila jambo’ na ‘Mbelaombe’. Kutokana na kutambua mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi, blog hii leo imefunga safari hadi nyumbani kwake Buguruni kwa Madenge, jijini Dar es Salam na kufanya naye mazungumzo juu ya maisha yake ya kimuziki.

Shem Ibrahim Karenga, mkongwe wa muziki wa dansi Alizaliwa mwaka 1950, Bangwe, Kigoma na kupata elimu ya msingi katika shule ya kimishionari ya Kihezya kuanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1964.
“Kiukweli, nilianza kujifunza muziki tangu nikiwa shuleni kwa sababu mimi nimesoma shule ya Wamishionari, sasa kule tulikuwa tukifundishwa fani hiyo,” ndivyo anavyoanza kusema Karenga.
Karenga anasema kuwa, baada ya kumaliza shule huku shetani muziki akiwa kampanda kichwani, mwaka 1964 alijiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz ambayo maskani yake yalikuwa mjini Kigoma. Anakumbuka kuwa, aliingia Lake Tanganyika akiwa mwimbaji na mcharazaji wa gitaa la besi, ambako pia alikuwa na ujuzi wa kutengeneza gitaa kwa kutumia vifaa vya kuokoteza. Akiwa na Lake Tanganyika Jazz, aliyodumu nayo kwa miaka minane, alianza pia kujifunza vyombo vingine vya muziki kama vile; Drums, Kinanda, gitaa la Rithym na  la Solo’.

 
Kutoka kushoto waliosimama Capy John Simon, Shem Karenga, Muhidin Gurumo, Juma Kilaza, Ally Rashid, Kassim Mapili na Salum Zahoro. Waliochuchumaa Nguza Viking, Mjengo,...

“Mwaka 1972, niliitwa kwenye bendi ya Tabora Jazz kama mwanamuziki mwenye kipaji cha utunzi, mwimbaji na mpigaji  wa gitaa la Solo, nilijiunga na Tabora Jazz nikiwa na vibao vyangu Dada Asha na Lemmy nilivyovitungia Lake Tanganyika, ambavyo vilinipa umaarufu mkubwa nilipo vipakua hapo Tabora Jazz'.
Anasema, Tabora jazz walimchukua akiwa Mtaalam wa muziki, ambako hata hivyo alipokuwa na bendi hiyo alikuwa akijiendeleza zaidi kwa masomo ya jioni kwenye shule ya Sekondari ya Milambo, Tabora pamoja na kusoma vitabu mbalimbali vya muziki
 Katika Tabora Jazz ambako alikuwa pia kama Kiongozi wa bendi, Karenga alikutana na wakali wengine wa muziki kama vile Kassim Kaluona na
Athuman Tembo ambao kwa sasa ni marehemu pamoja na Salum Muzila.

Kutokana na sababu binafsi ambazo hakutaka kuziweka wazi, mwaka 1983 alijiengua kutoka Tabora Jazz na kusimama kabisa kujihusisha na muziki, ambako kilichofuatia ilikuwa ni kifo cha bendi hiyo.

“Mwaka 1990 niliondoka Tabora na kutua jijini Dar es Salaam nilikokutana na Baraka Msirwa katika mwaka huohuo na kuniomba nijiunge na MK Beats ili kuiongezea nguvu,” anasema Kalenga.

Ndani ya MK Beats iliyokuwa ndugu na bendi nyingine iliyotamba vilivyo enzi hizo, MK Group, Karenga alikutana na wakali kama Malik Star,
Sisko Lulanga, Fungo Shomari na Bwami Fanfan.

Baada ya kujiunga na MK Beats iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Tukunyema’, Karenga aliisuka vema na kuinyanyua vilivyo hasa kwa vibao moto wa kuotea mbali vilivyozitetemesha vikali bendi nyingine
zote za wakati huo.

Mwaka 1995, MK Beats ilisambaratika, ambako mwaka uliofuata, yaani 1996 alianzisha bendi ya Tabora Jazz Star kwa kushirikiana na mtu
aliyemtaja kwa jina la Ibrahim Didi.

“Bendi ya Tabora Jazz Star ndio niliyo nayo hadi sasa nikiwa Mkurugenzi Msaidizi, ambako nafasi ya Mkurugenzi Mkuu imeshikiliwa na Didi mwenyewe,” anasema Kalenga.

Akizungumzia anavyouona ushindani wa kimuziki akiwa na bendi yake hiyo ya Tabora Jazz Star, Karenga anasema kwa upande wake mambo si mazito sana kwa kuwa ana mashabiki wake wa tangu huko nyuma.

Kwa upande wa mafanikio, Karenga anasema ukiondoa nyumba nzuri aliyoiporomosha nyumbani kwao Kigoma, anashukuru kuona ana marafiki wengi na anaishi atakavyo akiwa anamudu vema kuitunza familia yake.

Ushauri anaoutoa kwa wanamuziki na mashabiki wa dansi ni kuwa, wasibabaike kwani muziki huo ni wa kudumu, ambako hata hivyo anasikitika kuona kuna uhaba mkubwa wa vijana warithi wa miondoko hiyo
kwa sasa.

“Unajua, sisi tulirithi dansi kutoka kwa baba, kaka na wakubwa zetu wengine, lakini ni masikitiko makubwa kuona vijana wetu wa sasa wanarithi muziki hewa wa Bongo Fleva,” anasema.

Anasema, sababu ya kuuita muziki wa Bongo Fleva kuwa hewa ni namna wasanii wake wanavyopora midundo na ala kutoka nje huku wakijidai kuwa ni mtindo mpya wa muziki hapa nchini.

Mkongwe huyo anayebainisha siri yake ya kukubalika katika muziki kuwa ni bidii na juhudi za dhati kwenye fani hiyo, anasema anavutiwa na wasanii wote wanaofanya vema katika sanaa.

Kama ilivyo kwa wakongwe wengine wengi wa muziki, Karenga amefaulu kuwarithisha muziki watoto wake wawili wa kiume ambao ni Ramadhan na Mussa waliowahi kuwika vilivyo katika bendi ya TOT Plus.

“Mussa ni mwimbaji na rapa mahiri, ambako kaka yake, Ramadhan ni mcharazaji wa gitaa kiongozi, Solo,” anasema Kalenga, baba wa watoto sita.


shem karenga enzi za uhai wake
Watoto wengine wa Kalenga ambao hawakubahatika kurithi kazi yake ya muziki ni Tausi, Biata pamoja na Rehana

TAARIFA ZA KIFO CHAKE 
Shem Karenga amefariki dunia. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, ukindoa msiba wa Muhidin Maalim Gurumo, huu ndio msiba mwingine mkubwa zaidi katika muziki wa dansi na muziki wa aina zote kwa ujumla wake hapa nchini.

Shem Karenga ambaye ni mmoja wa wanamuziki wenye historia ya kipekee hapa nchini, amefariki JANA katika hospitali ya Amana, Ilala.

Mtoto wa marehemu, Rama Karenga, ameiambia Saluti5 kuwa msiba uko nyumbani kwao Buguruni na mazishi yanafanyika leo.

Moja ya wimbo wake uliotingisha bara la Afrika ni “Asha” ambao baadae ulirudiwa na mwanamuziki maarufu wa Congo, Lokasa ya Mbongo.

TAARIFA ZA MAZISHI
Shem Ibrahim Karenga Atazikwa leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam saa 10 alasiri. 

Mwili wa marehemu utapelekwa katika msikiti wa Manyema, Kariakoo saa 8 mchana kwa ajili ya
kuswaliwa!

mungu mlaze mahala pema peponi shem karenga ,,AAMINA .

Post a Comment

AddThis

 
Top