SEYCHELLES imeifuta mechi ya kesho jumamosi ya kufuzu fainali za mataifa ya Africa, AFCON 2015 nchini Morocco dhidi ya Sierra Leone kwasababu ya kuhofia virusi vya ugonjwa wa Ebola.
Hii ina maanisha Seychelles imepoteza mechi na kuathiri nafasi yao katika mashindano hayo.
Mapema jana alhamisi ilithitishwa kwa BBC Sport kuwa Sierra Leone walizuiliwa kupanda ndege kwenye uwanja wa ndege wa Nairobi Kenya ambapo wangesafiri moja kwa moja kwenda Seychelles kucheza mechi ya marudiano.
Maamuzi ya kuizua timu isisafiri yalichukuliwa na idara ya uhamiaji ya Seychelles, ambao wanahusika kuzuia kuenea kwa virusi vya Ebola nchini mwao.
Maamuzi hayo yalifuatiwa na taarifa kuwa rais wa Sierra Leone ametangaza kamati ya afya ya dharura kupamaba na kuenea kwa ugonjwa huo.
Rais wa chama cha soka cha Seychelles, Elvis Chetty aliiambia BBC: “Maamuzi ya kupoteza mechi ni ya chama cha soka cha Seychelles”
“Napenda kusema kwamba chama cha soka cha Seychelles kisilaumiwe kwa hili na chama cha Sierra Leone.
“Tumechukua maamuzi kwasababu ya ushauri uliotumwa na wizara ya afya ya Seychelles.
“Pia tulipokea barua kutoka wizara ya uhamiaji ikisema kuwa haitaruhusu timu ya Sierra Leone kuingia nchini.
“Walituomba kuahirisha mechi kwa muda usiojulikana, kwahiyo tumeona ni bora kupoteza kuliko kuruhusu ichezwe.
Sierra Leone iliyoshinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita, sasa watapewa nafasi ya kucheza hatua inayofuata ya kufuzu.
Chetty aliongeza: “Kwa mtazamo wa kimpira, kiukweli nimevunjwa moyo sana na hali hii. Taifa lilikuwa linaisubiri sana mechi hii tofauti na miaka mingi ya nyuma.”
Seychelles imeyaweka maamuzi yao katika maandishi ili kuyapeleka shirikisho la soka barani Afrika, CAF na watapeleka tangazo saa chache zijazo.
Post a Comment