Athumani Idd ‘chuji’ bado anagangaika kutafuta timu baada ya kutemwa na Yanga
TIMU mbalimbali za ligi kuu soka Tanzania bara zinaendelea kufanya usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu mpya unaotarajia kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Dirisha la usajili linatarajia kufungwa Agosti 27 mwaka huu kufuatia Shirikisho la soka Tanzania kusogeza mbele siku 10 kutoka siku ya mwisho ambayo ilikuwa Agosti 17.
Usajili maana yake ni rahisi tu. Ni kuongeza nguvu katika kikosi kilichotumika msimu uliopita. Inawezekana kubalisha wachezaji wote, lakini huwa ni vigumu kutokea katika mchezo wa soka.
Timu inaweza kufanya usajili wa aina mbili. Kuwapandisha wachezaji kutoka kikosi B au kutafuta wachezaji wapya nje ya timu hiyo.
Kinachofanyika siku zote ni kupunguza wasiokufaa na kuongeza wachezaji wapya watakaokuongezea nguvu zaidi katika mipango ya ligi.
Kama kusajili mara nyingi ni kuongeza nguvu, basi watu wanaotakiwa kuhusika zaidi ni wakuu wa mabenchi ya ufundi kwasababu wao ndio wanajua mapungufu ya vikosi.
Makocha ndio watu pekee wanaokaa na wachezaji kwa muda mrefu, wanawafahamu kwa kila kitu, wanatambua nidhamu na viwango vyao, hivyo wanapopendekeza fulani aachwe na fulani aongezwa abaki, lazima waheshimiwe.
Nahodha wa zamani wa Simba na Taifa Stars Henry Joseph Shindika bado mambo hayajamnyokea baada ya kutemwa na Simba sc
Lakini kibongobongo, nao makocha wanakuwa na mambo yao nyuma ya pazia. Wengine wanaweza kupendekeza kuachwa kwa mchezaji kwa sababu binafsi. Tunajua baadhi ya makocha wanakuwa na mahusiano mabaya na wachezaji nje ya uwanja, hivyo huamua kuwaondoa.
Ni kweli, lazima kocha awe na mchezaji anayemtii ili wafanye kazi kwa mafanikio, lakini kuna wakati ‘udingi’ wa makocha unaleta matatizo kwenye timu. Mfano makocha aina ya Luis Felipe Scolari aliyetimuliwa na Brazil, kwa mtazamo wangu hawastahili katika soka la kisasa.
Naamini zaidi makocha vijana, makocha wa kisasa. Makocha ambao wakati fulani wanaachana na migogoro binafsi na mchezaji na kufanya kazi ya uwanjani, halafu mambo mengine baadaye.
Nawapenda makocha wanaowachukulia wachezaji kama ‘washikaji’ tu. Kosa likitokea wanakaa na kuzungumza na si kutumia ubabe wa cheo.
Betram Mombeki (kushoto) alizinguana na Loga na kuachwa na Simba
Oooh! Nilishasema ni hivi, basi inakuwa hivyo. Hashauriki, haambiliki hata kama amekosea. Hawezi kuwaelewa vijana wake kwa kuwasikiliza wanahitaji nini. Hawa ni makocha wa kizamani sana, mpira umebadilika.
Ninaposema makocha wa kisasa simaanishi moja kwa moja suala la umri. Kocha anaweza kuwa ‘Dingi’, lakini akajua namna ya kuishi na vijana wake ambao ni wadogo kiumri na wana mambo mengi ndani na nje ya uwanja.
Inafahamika kuwa nidhamu ya mazoezi, nidhamu ya ndani na nje ya uwanja kwa baadhi ya wanasoka nchini Tanzania ni ndogo sana. Ndio maana wachezaji wengi wanaachwa na timu zao.
Hata hivyo, timu kubwa za Simba na Yanga mara nyingi zinawaharibia wachezaji kwa kuwachukua na kuwatelekeza hovyo. Hata namna wanavyovunja mikataba ni uzamani mtupu. Mara wachezaji wasilipwe haki zao, kila kukicha utasikia migogoro inatokea wanapoachana na wanandinga wake.
Leo hii ukipita katika mazoezi ya JKT Ruvu, unamkuta Athamani Idd ‘Chuji’, Henry Joseph, Jabir Aziz, Betrem Mombeki na wengineo wakifanya majaribio ili wasajiliwe.
Jabir Aziz (kushoto) aliachwa na Azam fc baada ya mkataba wake kuisha mwishoni mwa msimu uliopita
Ukienda Mwadui unawakuta Mohamed Banka, kwa mara nyingine Chuji, mara Juma Jabu wanafanya majaribio. Kila timu ndogo ya ligi kuu ukilinganisha na Simba, Azam na Yanga inasheheni nyota waliotemwa na klabu hizo.
Swali linakuja? Inakuwaje ‘Chuji’, Joseph, Aziz wanafanya majaribio JKT Ruvu kwa muda mrefu wakati ametoka kucheza Simba au Yanga kwa kiwango cha juu?
Hivi unadhani Chuji ameshuka kiwango kiasi kwamba JKT Ruvu au Mwadui fc wamuangalie kwa mwezi mmoja au zaidi?
Unadhani Henry Joseph kaisha kiasi kwamba hawezi kupata timu zaidi ya Simba au Yanga? Hapana. Kuna kitu kinatafutwa zaidi.
Wachezaji wengi wa Tanzania hasa wanaotemwa na timu kubwa wanasahau kuwa katika maisha kuna kupanda na kushuka. Inapotokea unashuka, lazima uwe na nidhamu ya hali ya juu ili kurudi mchezoni.
Mfano mzuri ni jinsi ambavyo Amri Ramadhani Kiemba ‘Baba wawili’ alivyojitunza. Aliachwa na Simba, Yanga akajiunga na timu ndogo kama Kagera Sugar na mpaka akaenda Miembeni Zanzibar, lakini akarudi kwa nguvu kutokana na nidhamu ya mazoezi.
Mfano wa wachezaji kama hawa ni wachache sana. Leo hii Fundi, Shaaban Kisiga ‘Malone’ anasajiliwa na Simba licha ya umri kwenda kutokana na nidhamu ya mpira aliyonayo. Amekaa kwenye ‘game’ kwa muda mrefu.
Wachezaji wa Kibongo wanawika msimu mmoja au miwili tu, mara unasikia kachuja. Anapoenda timu ndogo, anafanyiwa majaribio kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Tatizo la wachezaji wanaocheza Simba na Yanga wakienda JKT Ruvu au timu nyingine, wanataka kuishi maisha yale yale.
Kama Yanga alikuwa anapata posho kila akikutana na kiongozi kama Yusuf Manji, Seif Magari na wengine, anataka akikutana na mwenyekiti wa Ndanda fc amtoe kichache nje ya malipo rasmiJembe: Amri Kiemba (kushoto) ni mfano wa kuigwa
Eti!, bosi vipi nimepigika, nitoe kidogo bhaaasi? Kumbe bosi mwenyewe hana hizo hela na anafanya mipango ya kumuingizia mshahara mwisho wa mwezi na hata wakati fulani anachelewa kutokana na uwezo mdogo wa timu kiuchumi.
Inapotekea mazingira haya,wachezaji wengi wanaanza vurugu na utovu wa nidhamu na kuona maisha yamekuwa magumu katika klabu hizo.
Cha msingi ni kwamba, JKT Ruvu, Ndanda fc, hapawezi kuwa sawa na Yanga, Azam, au Simba. Mchezaji akienda huko ajue kuna vitu atakosa tu. Zile pesa zakutoana kishikaji kutoka kwa akina Hans Poppe, Seif Magari, Davis Mosha huwa hazipo.
Jambo la muhimu ni kujua kuwa katika maisha kuna kupanda na kushuka. Ukienda timu ndogo unapata nafasi kubwa ya kucheza, jenga nidhamu nzuri ya mazoezi, utarudi katika kiwango chako na kurudishwa Simba au Yanga kama shujaa.
Lakini kama tabia za utovu wa nidhamu zitaendelea, makocha wa timu ndogo na viongozi wataendelea kuwafanyia majaribio kwa miezi miwili na zaidi wakiwahofia kuharibu timu zao.
Post a Comment