HATUA ya Robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame, inaanza kutimua vumbi leo jumanne mjini Kigali, Rwanda.
Robo fainali ya kwanza itaanza majira ya 9:00 alasiri kwa kuwakutanisha wanyarwanda wawili, Polisi na Atletico.
Mechi hii inatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na viwango vya timu hizo ambazo zinafamiana vizuri katika michuano ya ligi kuu nchini Rwanda.
Robo fainali ya pili itaanza majira ya saa 11:00 jioni ambapo timu mbili pinzani nchini Rwanda, Rayon Sport na APR zitachuana vikali.
Baada ya kuwafahamu washindi watakaocheza nusu fainali leo, robo fainali nyingine mbili zitapigwa kesho jumatano.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam fc maarufu kama Wana Lambalamba watashuka dimbani kukabiliana na El Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El Merreikh katika soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam wamekwaa kisiki ambacho wanahitaji maarifa makubwa kukivuka.
Meneja wa Azam fc, Jemedari Said alisema wamejiandaa vizuri na wanafurahia kuchuana na timu ngumu ambayo itawapa kipimo kizuri cha kujua maendeleo ya kikosi chao.
“Sio pambano jepesi, El Merreik ni timu yenye historia kubwa. Sisi kama Azam hatuwaogopi, tunawaheshimu, tutapambana kupata ushindi ili kutinga nusu fainali na hatimaye fainali na kutwaa ubingwa”. Alisema Jemedari.
Jemedari alisema wachezaji wote waliokuwa majeruhi, Waziri Salum ambaye hajacheza mechi yoyote, Leonel Saint -Preux l, Shomari Salum Kapombe wote walifanya mazoezi, na kwa mara ya kwanza kikosi kizima kilikuwa uwanjani kujiandaa na mchezo huo.
Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.
Post a Comment