Mbrazil, Marcio Maximo amekuwa kocha wanne kufanya kazi Yanga SC tangu, Yusuph Manji alipokuwa mwenyekiti wa klabu hiyo katikati ya mwaka 2012. Nafasi ya kwanza muhimu ilikuwa kwa Mbelgiji, Tom Saintfiet ambaye alitimuliwa kazi mara baada ya miezi miwili. Tom alipoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Mtibwa Sugar walipochapwa mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu, mwezi Septemba, 2012.
Ernie Brandts raia wa Uholanzi alichukua timu hiyo na akafanikiwa kuipa ubingwa wa ligi kuu msimu huo. Brandts alifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kuondolewa mara baada ya kufungwa mchezo wa hisani na Simba SC, Disemba, 2013 kwa mabao 3-1 siku chache baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na nafasi yake ikachukuliwa na Mholanzi mwingine, Hans Van der Pluijm ambaye alishindwa kuipa timu hiyo ubingwa ulioangukia kwa Azam FC
Maximo ameonekana anafaa kuwa ‘ meneja’ wa timu hiyo na Manji alionyesha kuvutiwa naye tangu alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza lakini jaribio la kumrejesha nchini lilishindikana kabla ya kuwezekana hivi karibuni. Licha ya kuwa na michuano ya kombe la Shirikisho Afrika, baadaye mwakani, Yanga wanataka kwanza kurudisha ubingwa wa Tanzania Bara ndiyo maana wamemleta Maximo- Mtu mshindi katika falsafa zake za ufundishaji.
UBORA KATIKA BENCHI LA UFUNDI
Maximo ana wasaidizi wa kutosha, yaani kwa maana nyingine amezungukwa na walimu wasaidizi wengi. Leonardo Leiva na Salvatory Edward hawa ni makocha wasaidizi wa Maximo na kila mmoja amekuwa makini katika kazi yake tangu walipoanza kufanya kazi pamoja mwezi uliopita. Juma Pondamali ni kocha wa makipa, huku Shadrack Nsajigwa akiwa kocha wa mabeki. Ubora wa kwanza ambao unaweza kupatikana katika kikosi cha Yanga unatokana na idara yao ya ufundi kuwa na watu wa kutosha ambao wanatambua vyema majukumu yao. Salva ni mshindi wa kweli kiuchezaji na kiufundishaji ameweza kuisuka timu ya pili ya Yanga na kuipa taji la Uhai Cup mwaka uliopita.
Yanga wapo katika muonekano mzuri zaidi ya timu zote kuelekea msimu mpya. Timu yao ni ya muda mrefu huku wachezaji wengi wakiwa pamoja, Maximo hatapata tabu sana kuwekeza mbinu zake. Watakuwa tishio katika ligi kuu, wakiwa na wachezaji kama Juma Kaseja, Deogratius Munishi, Ally Mustapha, Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Nadir Haroub, Oscar Joshua, Juma Abdul ambao ni ‘ kiungo katika ngome ya timu yao’. Haruna Niyonzima, Andrey Coutinho, Saimon Msuva, Mrisho Ngassa, Hassan Dilunga, Omega Seme, Salum Telela, Nizar Khalfan katika nafasi ya kiungo, huku safu ya mashambulizi ikitaraji kuongozwa na Jery Tegete, Gelson Santos ‘Jaja’, Said Bahanunzi, Hussein Javu, Emmanuel Okwi, Hamis Kizza kunafanya mtu usiwe na shaka na timu hiyo kwani imekamilika kiuzoefu, kiubora, labda kama watafeli katika uwajibikaji.
!MAPUNGUFU.
Licha ya kufanya usajili wa wachezaji watatu msimu huu wa usajili, Maximo anaweza kukabiliwa na tatizo kubwa ambalo limekuwepo klabuni hapo kwa miaka mingi. Wachezaji wa kigeni wameonekana kutotulia kwa sababu wachezaji muhimu wazawa huwatenga kwa sababu za kuwaonea gere kutokana na mishahara yao mikubwa. Yanga inahitaji kupata mafanikio hivyo Maximo hatapenda mtu ambaye ataivuruga timu kwa mambo yake binafsi
Hata kama mambo hayo yakikanushwa lakini ndivyo ilivyo katika timu hiyo, Sam Timbe aliathiriwa sana na tabia hiyo licha ya kuonekana ni kocha mzuri wachezaji waligawanyika kiasi cha kuiyumbisha timu hiyo. Licha ya kukusanya wachezaji wengi wenye ubora, Yanga watachemsha kama hawataishi katika misingi ya ujamaa, wakifanikiwa hili sina shaka watakuwa mabingwa msimu ujao. Wana timu bora, walinzi wazuri, viungo wenye ubunifu, washambuliaji wazuri, bechi la ufundi lililojaa na kupangwa vizuri, nini Azam FC, Yanga ni timu yenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, msimu wa 2014/15.
Post a Comment