0
 Ade Akinbiny  alishinda taji moja tu katika maisha yake ya soka la kulipwa! Tena taji hilo si la ushindi wa timu bali ‘ Mchezaji bora wa mwaka wa Stoke City, 2004.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Nigeria alikuwa mchezaji ghali zaidi wa klabu ya Leicester City wakati aliponunuliwa kwa kiasi cha euro 5.5 Million kutoka Wolvs mapema mwaka, 2000. Ade alisajiliwa kama mbadala wa mshambulizi, Emile Heskey ambaye alikuwa amejiunga na Liverpool kwa ada ya euro 11 million.

  Leicester ilitumia nusu ya pesa ya Heskey kumsaini, Ade lakini hawakuwahi kupata hata robo ya mabao ambayo, Heskey aliyafunga. Ade akageuka ‘ mshambulizi butu zaidi’ kuwahi kutokea katika ligi kuu ya England kwa kuwa alifanikiwa kufunga bao moja tu katika misimu miwili ambayo hakukosena katika kikosi cha kwanza cha Leicester. 

Kila mwisho wa wiki alipangwa kuongoza safu ya mashambulizi lakini hakutoa matunda, siku ambayo alifunga bao la kwanza alishangilia kama ‘ mwendawazimu’ kiasi cha kuzunguka uwanjani akishangilia. Kazi ya mshambuliaji ni kufunga mabao, kutokufunga ni kushindwa lakini bado mchezaji anaweza kuaminiwa na kupewa nafasi ikiwa anatoa mchango mwingine katika timu.

 Kwanini nimemkumbuka, Ade?. Kuna watu ambao bado wanatia shaka kuhusu ujio wa wachezaji wa kulipwa kutoka Brazil ambao klabu ya Yanga SC imewasaini kuelekea msimu mpya wa ligi kuu, Tanzania Bara. Kiungo-mshambulizi, Andrey Coutinho na mshambulizi wa kati, Gelson Santos ‘ Jaja’.
Walio wengi wanasema kuwa, wachezaji hao ambao wameambatana na kocha, Marcio Maximo ni wazuri na watatoa mchango mkubwa kwa mabingwa hao mara 24 wa zamani wa Bara, lakini wapo pia ambao wanasema, Jaja atafuata mkumbo wa wachezaji wengi wa kigeni walioshindwa kufanya lolote licha ya awali kupewa nafasi ya kufanya mambo makubwa.

  Katika miaka ya karibuni ambayo tumeshuhudia wachezaji wengi wa kigeni wakija nchini kucheza soka, klabu ya Yanga inaongoza kwa kusajili wachezaji wa nje. Nafasi ya ushambuliaji imekuwa ikiwatoa jasho kupata ‘ mtu sahihi’.

 Hakuna shaka kuwa soka la kisasa linahitaji mchezaji wa kariba ya Jaja kwenye safu ya mashambulizi ya Yanga kama wanataka kujihakikishia upatikanaji wa mabao. Jaja ni mchezaji mwenye umbo la wastani ambalo linaweza kuwatisha na kuwasumbua mabeki. Si hivyo tu, mchezaji huyo ameonyesha kitu katika muda wa mwezi mmoja ambao amekuwa akijifua na timu hiyo. Jaja ni mpigaji wa ‘ mashuti ya kichwa’, anauwezo wa kumiliki mpira, kutoa pasi na kujipanga katika maeneo yake ya hatari.
Yanga haijapata mfungaji kama, Mkenya, Boniface Ambani ambaye alifunga mabao 18 katika ligi iliyokuwa na michezo 22 msimu wa 2008/09. Kabla ya Ambani, Yanga iliwahi kuwa na mshambuliaji hatari kutoka, DRC, Laurent Kabanda, 2007, lakini mchezaji huyo ( Kabanda, marehemu kwa sasa) hakutulia klabuni hapo na hakufunga bao lolote katika ligi ya Tanzania hadi anaondoka ‘ kiaina’. Licha ya Kabanda, Yanga iliwasajili pia, Aime Mukandila Lukunku raia wa DRC, Bernard Mwalala na Morris Sunguti wote kutoka Kenya. 

Lukunku hakuonekana baada ya kuwa na majeraha yasiyokwisha na baadaye ikagundulika kuwa mchezaji huyo alikuwa na matitizo sugu ya nyama za paja. Mwalala alikuwa mchezaji mzuri lakini yeye alikuwa ni kwaajili ya mechi dhidi ya mahasimu wao tu, Simba SC kwani mchezaji huyo alikuwa akitumia muda mwingi kwenda kwao badala ya kuwa klabuni kabla ya kugundulika kuwa alikuwa akisoma huku akicheza soka. Kama, Mwalala angetulia pengine angekuwa mchezaji bora zaidi wa kigeni kuwahi kuichezea timu hiyo. 

Sunguti alikuwa mfungaji hasa, alifunga mabao 11 katika mzunguko wa pili msimu wa 2009/10 lakini umri wake mkubwa ukafanya asidumu klabuni hapo. Yanga wanatumia pesa nyingi kusaka washambuliaji wa kigeni katika miaka ya karibuni lakini machaguo yote bora huwa ni ya muda mfupi kama ilivyotokea kwa Ambani na Sunguti, ila pia hawana bahati ya kupata mfungaji mahiri wa uhakika.


 Jamal Mba ‘ Jama Mba’ raia wa Cameroon, Mkenya, Moses Odhiambo ni washambuliaji ambao wamewahi kuichezea klabu hiyo ila hakuna ambaye aliweza kumshawishi ‘ mtu wa Yanga’. Mba aliwahi kutwaa tuzo ya ufungaji bora katika ligi ya Cameroon, 1994 ila akiwa na umri mkubwa hakuweza kufunga bao lolote msimu wa 2010/11 katika ligi kuu ya Bara. Odhiambo alikuwa nyota wakati akiichezea, Moro United kisha Simba lakini ndani ya Yanga alifunga mabao mawili tu.


David Mwape raia wa Zambia, Keneth Asamoah raia wa Ghana wote hao waliweza kucheza pamoja katika safu ya mashambulizi msimu wa 2011/12. Mwape alikuwa akicheza vizuri mechi moja na kuharibu iliyokuwa ikifuata, Asamoah alifanikiwa kufunga mabao 12 lakini hayakutosha kutokana na nafasi nyingi ambazo alikuwa akizipoteza. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wachezaji wa kigeni katika klabu kuwa hawapewi sapoti ya kutosha na wachezaji wazawa, lakini kwa mchezaji wa kulipwa anaweza kuishi vizuri nchini kama atajishusha mbele ya wachezaji wenzake na kufanya kazi nzuri uwanjani.
 
Huu si muda mwafaka wa kusema kuhusu, Jaja lakini sifikirii kuwa mchezaji huyo atachemsha katika klabu yake mpya kwa sababu hakuna aliyefanya vizuri. Mbrazil ni Mbrazil tu, Jaja si wale wachezaji wazee ambao walipita Yanga kwa lengo la ‘ kuichuna’ na kuicha klabu hiyo ikikosa makali. Huyu ametoka kwao Brazil kuja nchini kufunga mabao, nina imani naye kubwa ila nitamuweka katika kundi la Ade ambaye aliichezea Nigeria mechi moja tu.


Post a Comment

AddThis

 
Top