SIKU za hivi karibuni kama sehemu ya udhamini wake, kampuni ya TBL kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi vifaa vya michezo kwa klabu za Simba, Yanga kwa ajili ya msimu wa 2014/15 wa Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza septemba 20 mwaka huu.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema vifaa walitoa ni pamoja na mipira, viatu, soksi, shin guards, nguo za mazoezi, nguo za kawaida, gloves na vitu vingine vingi ambavyo vitawezesha timu hizi za Simba na Yanga kucheza wakifurahia kuvaa vifaa vyenye ubora wa hali ya juu.
Ni lengo zuri kwa mdhamini kama TBL kutoa vifaa hivyo kwa klabu hizo, lakini kwa nyakati tulizokuwa nazo, si sahihi kwa klabu za Simba na Yanga kugawiwa jezi na viatu.
Hizo pesa zinazotumika kununua hivyo vifaa, ni mara mia klabu zingepewa pesa `keshi` kuliko utaratibu wanaofanya, kwasababu hela ni nyingi mno.
Simba na Yanga wana uwezo wa kuingia mikataba na makampuni yanayozalisha vifaa vya michezo. Kinachotakiwa ni kuwa na mtazamo chanya wa kibiashara wa kutumia nembo za klabu ili kuingia mikataba na makampuni yanayozalisha vifaa vya michezo.
Unaweza kutolea mfano, juzi juzi tumeona klabu ya Asernal imeingia mkataba na kampuni ya Puma . Pia Manchester United imeingia mkataba na kampuni ya Adidas.
Kutokana na klabu za Simba, Yanga kuwa na mashabiki wengi, ni fursa kubwa kama watatafuta wataalamu ambao wana mitazamo ya kibiashara na kuona mashabiki wengi walionao Tanzania nzima, wanaweza kutumika kama njia ya kuzinufaisha klabu hizi kama ambavyo klabu nyingine za ulaya zinafanya.
Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe akimkabidhi vifaa Mkurugenzi wa Masoko wa Yanga, George Simba. Anayeshuhudia ni Hafidh Saleh, Meneja wa Yanga. (Picha: Executive Solutions).
Kwa mfano Mfano, Simba, Yanga, wakatafuta kampuni ambayo inatengeneza vifaa vya michezo kama vile Puma au uhl sport. Jezi ambazo wanavaa Simba na Yanga zinazalishwa na kampuni ya uhl sport .
Kwanini Simba na Yanga wasiingie mkataba wa moja kwa moja na uhl sport ili wawe wanasambaza vifaa kwa klabu hizi na kutengeneza jezi za ziada kwa ajili ya mashabiki wake.
Kwa maana ya kwamba, uhl sport wanaingia mkataba na Simba au Yanga, wao si wanazalisha vifaa, wanakuwa na wajibu wa kuwavalisha Simba au Yanga. Faida yake ni kwamba, uhl sport anatangaza biashara yakekwa kutumia fursa ya Simba na Yanga kuvaa zile jezi, kwasababu klabu hizi zinatangazika na zinajulikana.
Pia wanaingia mkataba na uhl sport wa kuwapatia vifaa Simba na Yanga bure, lakini wanakubaliana kuwagawia idadi ya jezi nyingine kwa ajili ya kuuza kwa mashabiki. Kwa mfano, jezi elfu 50 au laki moja ambazo uhl sport wanatengeneza, wanawapa Simba waziuze labda kwa shilingi elfu 20.
Kama gharama za kutengeneza jezi moja kwa kujumuisha mambo yote, malighafi, teknolojia na usafiri ni shilingi elfu 10, jezi ikifika Tanzania, labda iuzwe kwa shilingi elfu 20.
Kikosi cha Simba msimu uliopita
Katika ile elfu 20, Simba wanachukua shilingi elfu tano, halafu shilingi elfu 15 inarudi kwa wale uhl sports.
Kampuni ya uhl sport inatoa vifaa bure, lakini inatumia fursa ya kufanya biashara, kivipi? Wanatengeneza jezi za ziada kwa ajili ya mashabiki.
Mashabiki wananunua jezi elfu 20, kwasababu Simba wao hawazalishi,wanatumia fursa ya kuwa na mashabiki tu, shilingi elfu 15 inarudi kwa mzalishaji, halafu shilingi elfu tano inabaki Simba. Hapa wanakuwa wamefanya biashara.
La pili sasa, kama Simba au Yanga wameingia mkataba na uhl sports, ina maana ile hela ambayo TBL wanaitumia kununua jezi za kuigawia klabu, inaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya Simba na Yanga. Ina maana uchumi wa klabu hizi unastawi kutokana na fedha hizo.
Hii ni kwa viongozi wa Simba na Yanga. Wanatakiwa kupata elimu kuwa , huu utaratibu unaotumika ni wa kizamani. Wabadilike, wawe na wataalamu kwa watendaji wao.
Wawe na wataalamu wa masoko na biashara, yaani wakurugenzi wa masoko. Wawe na watu ambao wataweza kuzisaidia klabu hizi kutumia fursa walizonazo kupata fedha nyingine za ziada, ambazo ni nyingi tu, lakini wamekosa watu sahihi,wenye ueledi wa masuala haya ya kibiashara na mambo ya masoko kwa ajili ya kutumia fursa ya mashabiki wengi wanaozisapoti klabu hizi kama njia ya kujitengenezea pesa.
Kikosi cha Yanga sc msimu uliopita
Puma wanaingia mikataba na klabu za Afrika au nchi za Afrika, lakini ni tofauti na wafanyavyo katika klabu kubwa za Ulaya kama vile Manchester United, Asernal au Real Madrid.
Hayo makampuni pamoja na kuzigawia klabu hizi vifaa, bado wanazitumia kama sehemu ya kujitangaza na kuitanua kibiashara yao kwasababu tayari ni kubwa.
Kwahiyo , Manchester United hawawezi kuingia mkataba na Adidas kwa ajili ya kumuuzia jezi ili apate faida, ila Adidas ndiye anaihitaji Manchester United kutokana na ukubwa alionao ili autumie kutangaza kampuni ili iweze kuwa maarufu na kupata fursa ya kufanya bishara na klabu nyingine.
Ndio maana, Adidas wanaipa Manchester United mabilioni ya hela ili kuvaa jezi ambazo wao wanazalisha, lakini kwa soko la Afrika, klabu bado hazijafika ukubwa kama klabu za Ulaya. Njia inayotumika ni kugawiwa vifaa bure, halafu wanarudisha gharama zao kupitia mfumo mzuri uliotengenezwa wa kuuza jezi kwa timu za Taifa au klabu.
Ile faida wanagawana kati ya Taifa au shirikisho la soka kama ni mkataba wa timu ya taifa, au klabu. Hii ina faida kwa pande zote mbili, klabu inatumia fursa ya mashabiki wake kusukuma biashara ya ile kampuni.
Kwa mfano ukipiga hesabu ya shilingi elfu 5 kwa kila jezi.Kama zimetengeneza jezi laki moja maana yek ni 5,000 x 100,000. Unapata kama shilingi za kitanzania milioni 500,000,000. Huo ni mzigo mmoja.
Umeona jinsi klabu inavyoweza kutengeneza hela? ni hela nyingi mno. Umeona? Ni hela ndefu. Umeona fursa ya kuingia mkataba na makampuni yanayozalisha hivyo vifaa? Inaweza kuzisaidia klabu kupata hela nyingi na kuepusha kuitumia hela wanayopata kutoka kwa mdhamini kununulia vifaa.
Viongozi Simba, Yanga, amkeni, fursa ipo, sema hakuna watu sahihi!.
Post a Comment