0
Ofisa Habari mwenye mbwembwe na majigambo mengi wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, juzi aliishiwa ujanja na kujikuta akikimbilia polisi baada ya kutishiwa kifo na mzee mmoja anayedaiwa kuwa ni kiongozi wa Coastal Union aliyemtaja kwa jina moja la Kitendo.

Mkasa huo wa aina yake ulitokea juzi Jumamosi wakati timu hiyo ilipokwenda kuuangalia uwanja watakaochezea mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union iliyotarajiwa kupigwa jana Jumapili kwenye uwanja huo.

Masau ameiambia SALEHJEMBE kuwa mbali na kiongozi huyo kumtishia kifo, pia alimshambulia kwa matusi makali ya nguoni ambayo ni aibu kuyasema mbele ya watu.

“Kama unavyojua kanuni za soka, timu ngeni inatakiwa kufanyia mazoezi kwenye uwanja husika itakaoutumia kwa ajili ya kuuzoea uwanja, lakini viongozi wa Coastal Union walituomba tukafanyie mazoezi uwanja maalum waliotupa wakiomba kuutumia kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya kombaini ya Mombasa.

“Kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo kati yetu na Coastal Union tukaona tuwaachie wautumie na sisi tukaenda kuutumia huo uwanja waliotupatia, lakini jioni baada ya mazoezi tukaona ni vyema tukawapeleka wachezaji wetu wakautazame uwanja.

“Tulipofika kwenye Uwanja wa Mkwakwani tuliotakiwa kuutumia, ndiyo akanyanyuka mzee huyo (Kitendo) aliyekuwa amekaa jukwaani na kuanza kunitolea matusi ya nguoni na kunitishia kuniua kwa njia ya upepo.

“Baada ya kunipa vitisho vile, nikanona ni vyema niende nikatoe taarifa polisi, kwa sababu kitisho cha kumuua mtu siyo kidogo, huyo mzee ndiye aliyeanzisha fujo za mwanzoni nilizofanyiwa hapa Mkwakwani wakati tulipokuja kucheza na Mgambo.

“Hivyo, mara baada ya kutoka uwanjani hapo, mimi na viongozi wangu tukaenda Kituo cha Polisi cha Chumbageni hapa Tanga kwa ajili ya kwenda kuripoti, pia tukatoa taarifa kwenye Chama cha Soka Mkoa wa Tanga na kwa viongozi wa Coastal Union,” alisema Masau.

Post a Comment

AddThis

 
Top