KAGERA SUGAR YAIKARIBISHA MBEYA CITY MWANZA IKALE KIPIGO
Kikosi cha Kagera Sugar kimetamba kuwa kitatembeza kipigo kwa Mbeya City Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Kagera wamesema wao ni timu bora kuliko Mbeya City ambao walikuja kwa mbwembwe msimu uliopita lakini msimu huu wameshindwa kuonyesha makali yao.
Mtanange huo unachezwa Mwanza kwa kuwa Uwanja wa Kaitaba wa mjini Bukoba unaotumiwa na Kagera unafanyiwa ukarabati.
Msemaji wa Kagera, Mohamed Hussein, amejigamba kuwa Mbeya City itegemee kipigo kikali kwa kuwa timu hiyo ni zaidi yao kutokana na kupanda ligi kuu tangu msimu wa 2005/06 na haijawahi kushika mkia.
“Mbeya City ni timu kama timu nyingine za Simba na Yanga ambazo tulizichapa na yenyewe isubiri kipigo kitakatifu kwa kuwa ni timu changa kwetu kwani tumepanda daraja tangu msimu wa 2005/06 bila ya kushika mkia hata mara moja tofauti na wao ambao wamepanda juzi tu lakini leo tayari wameanza kutetereka.
“Kikosi chetu kipo vizuri na kwa sasa tupo kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo,” alisema Hussein.
Post a Comment