0

HII haitakuwa ni mara ya kwanza kuandika kuhusiana na namna Mtibwa Sugar wanavyofanya mambo yao kwa mfumo wao wa kipekee, nikaeleza wazi kuwa unanivutia.


Nakumbuka mara ya mwisho nilizungumzia namna ambavyo timu hiyo inavyoweza kufanya vizuri bila ya kuwa na wachezaji wa kigeni.

Si kwamba Mtibwa Sugar haijawahi kusajili wachezaji wa kigeni, la hasha. Lakini ni nadra na hata isipokuwa nao, basi inaendelea kufanya vema.

Msimu huu hadi Ligi Kuu Bara inasimama, Mtibwa Sugar imepata sifa mbili kuu; kwanza kuwa timu inayoongoza ligi hiyo, pili; ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza hata mchezo mmoja.

Usisahau Mtibwa Sugar haina mchezaji hata mmoja wa kigeni, hali kadhalika haina hata kocha mmoja wa kigeni.

Ukiachana na hayo, kuna mambo mengi wadau kama tukikubali kujifunza, tunaweza kuitumia Mtibwa Sugar kama shule.

Kwani pamoja na kuwaamini sana wachezaji wa kizalendo na bado ikaendelea kufanya vizuri, pia imekuwa ikiwaamini makocha wazalendo tena wale wanaokulia katika mazingira ya timu hiyo.

Unakumbuka wakati fulani safu ya benchi lao la ufundi ilikuwa hivi; kocha mkuu, Mecky Maxime, msaidizi wake, Zuberi Katwila na kocha wa makipa, Patrick Mwangata.

Hawa wote ni wazalendo waliowahi kucheza katika kikosi cha Mtibwa Sugar na pia timu ya taifa, Taifa Stars.

Wameaminiwa, timu yao inafanya vizuri na wameweza kuifanya kazi yao hadi kuiondoa kabisa Mtibwa Sugar kuwa kwenye kundi la timu zenye hofu ya kuteremka daraja.

Badala yake ni kati ya zile zinazowania kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara, nafasi ya pili au kubaki kwenye kundi la kati, yaani hakuna presha ya kushuka au kuwa bingwa.

Kitu kizuri naweza kusema, ikiwezekana wafanye kila linalowezekana wachukue ubingwa ili kuingia kwenye kundi, hata wazalendo wana uwezo huo wa kuchukua ubingwa maana katika siku za hivi karibuni, makocha wanaobeba ubingwa ni wale wa kigeni tu!

Kingine ambacho naweza kusema ndiyo nilikilenga zaidi kwamba tunaweza kujifunza kupitia kwa Mtibwa Sugar ni kuhusiana na wachezaji ambao huonekana hawafai kwenye klabu zao, halafu Mtibwa Sugar inawachukua na wanafanya vema.

Hii si mara ya kwanza au ya pili, Mtibwa Sugar imekuwa ikiwachukua wachezaji kutoka katika klabu mbalimbali na hasa Yanga na Simba ambako walitoka wakionekana wamekwisha au wamepoteza mwelekeo, halafu wanaanza kufanya vema.

Mfano wa karibu kwa msimu huu ni David Luhende aliyetoka Yanga akionekana hana lolote au Mussa Hassan Mgosi na Henry Joseph, wakongwe walioonekana ni kazi bure Simba, leo ndiyo wanaozisumbua klabu zao za zamani zikikutana na Mtibwa Sugar!

Mtibwa Sugar inajua namna ya ‘kujipikilisha’ na wakongwe hao hadi msosi unaiva vizuri na wanakuwa tishio kwa waliowaona hawana kitu. Jiulize wanafanyaje?

Ukiachana na hivyo, pia angalia Mtibwa Sugar walivyo na uwezo mkubwa wa kuwafufua wachezaji wenye vipaji, wakawapa nafasi na baadaye kuwa kivutio kikubwa kwa wakongwe kama Yanga na Simba au Azam FC.

Safari hii, Simba imelazimisha hadi imefanikiwa kumpata beki wa kulia kutoka Mtibwa Sugar, Ramadhani Kessy ambaye kabla hakuonekana kama ni lolote hadi timu hiyo ilipompa nafasi.

Usisahau Amir Maftah wakati akiwa beki bora wa kushoto nchini alitokea Mtibwa Sugar kwenda Yanga kama ilivyokuwa kwa akina Victor Costa Nampoka na Mgosi pia ambao walijiunga na Simba na baadaye kuwa lulu.

Lazima tukubali mfumo wa Mtibwa Sugar ni bora. Tukikubali pia ni rahisi sana kujifunza na tunaweza kubadilisha mambo kadhaa.

Post a Comment

AddThis

 
Top