BONY ALIAMBIA SI NYOTA, HAWEZI KUPIGA PICHA, ALIJUA ANAKOKWENDA, SASA ANATARAJIA KUPATA SH 270M KWA WIKI
MWAKA 2009 nikiwa jijini Abidjan, Ivory Coast, nilikutana na mshambuliaji niliyetambulishwa kwake kwa jina la Wilfred Bony ambaye wakati huo alikuwa akikipiga katika timu ya Sparta Prague ya nchini Czech.
Dereva teksi niliyekuwa nikitembea naye, alinieleza hadithi yake nzuri kwamba alitokea katika klabu ndogo ya Issia Wazi iliyosifika kwa kuibua vipaji lakini pia ilisifika sana kwa ukabila.
Kilichonivutia ni kwamba Bony aliwahi kufeli majaribio katika Klabu ya Liverpool ya England na wananchi wengi wa Ivory Coast waliamini ndiye atakayekuja kuwa Drogba mpya kwa kuwa alizitesa sana timu kongwe za Asec Mimosa na African Sports kwa muda mfupi aliochezea Issia Wazi.
Nilimsogelea Bony, nikazungumza naye ikiwa ni baada ya kujitambulisha. Yalikuwa mazungumzo ya kawaida tu si mahojiano. Kabla ya kuachana niliomba kupiga naye picha, akanitolea nje.
Akaniambia: “Bado mimi si nyota, hauhitaji kupiga picha nami.”
Awali nilidhani anatania, lakini baadaye alishikilia msimamo wake hadi mechi kati ya DR Congo na Ghana ilipoanza katika Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny kidogo sikufurahia, lakini niliamua kuheshimu msimamo wa mshambuliaji huyo ambaye nilielezwa alirudi Ivory Coast.
Miaka minne baadaye, nilikutana na Bony jijini Dar es Salaam. Alikuwa amekuja na kikosi cha Ivory Coast kuivaa Taifa Stars. Nilifika katika hoteli waliyofikia baada ya appointment yangu na kocha Sabri Lamouch kuzaa matunda. Pia niliomba mahojiano na Yaya Toure, lakini siku hiyo aligoma hata kutoka chumbani akisisitiza alikuwa ana ‘focus’ kuhusiana na mechi dhidi ya Stars.
Baada ya mahojiano na Lamouch, nilimuona Bony akipita, nilimsimamisha na kumkumbusha mazungumzo yetu kule Abidjan. Kwa mara ya kwanza niligundua hakuwa akiringa kama nilivyofikiri.
Kwanza alicheka sana, akasema amefurahishwa kukutana nami. Nikamuuliza vipi kuhusu picha, haraka alikubali na tulipomaliza kupiga picha, akaniambia. “Bado sijawa staa, ndiyo naanza mbio za kuwa staa.”
Baada ya hapo aliingia kwenye basi la wachezaji ili kuanza safari ya kwenda Uwanja wa Taifa kuivaa Taifa Stars katika mechi ambayo wageni hao walishinda kwa mabao 4-2, Bony akifunga la nne dhidi ya kipa Juma Kaseja.
Leo Bony, 26, Swansea wamekubali kumuuza kwenda Manchester City kwa kitita rundo cha pauni milioni 30 (Sh bilioni 81) na mshahara mnono wa pauni 100,000 (Sh milioni 270) kwa wiki. Aisee, ninawaza mambo mengi sana, ninajifunza lakini nawatupia wote tutafakari.
Afrika Magharibi ina wachezaji wengi waliofanikiwa kwa kuwa wana uwezo wa kujaribu, wanataka kufanya vema na si waoga kujaribu. Jiulize wachezaji wa hapa nyumbani wanafanya hivyo?
Huenda ni tabia ya Watanzania wengi, hawajiamini na si watu wanaopenda bugudha. Wanataka mambo yaende kiulaini ndiyo maana wengi wanacheza hapa nyumbani tu!
Wakati Bony anakataa kupiga picha nami kwa kigezo kuwa yeye si staa, alikuwa akimaanisha. Siku alipokubali kupiga picha alisisitiza, bado hajawa staa. Lakini sasa hakuna ubishi kuwa ni staa na kweli anastahili kuwa mrithi wa Drogba kama wapenda mpira wa Ivory Coast walivyoamini miaka zaidi ya mitano iliyopita.
Kweli Jonas Mkude anataka kujaribu hiyo, vipi kuhusu Frank Domayo na Simon Msuva? Wote wanasubiri jua la jioni ndiyo waanze kufanya mipango ya kwenda Ulaya?
Wote wanasubiri hadi wapate maudhi, wadharauliwe au kukasirishwa na viongozi wa Simba, Yanga au Azam FC ndiyo wafikirie ni wakati mwafaka kutoka nje ya Tanzania?
Wapo wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza angalau Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya Magharibi kama ambavyo Bony alifeli England akaenda Jamhuri ya Czech, halafu akarudi na baada ya kufanya vema Swansea, sasa anatua kwenye kikosi cha mabingwa wa England. Tuache maneno mengi, jamani amkeni.
Post a Comment