0
Kipre Tcheche amefunga mabao 47 katika ligi kuu ya Tanzania Bara tangu alipowasili katika kikosi cha Azam FC, Januari, 2011. Mshambulizi huyo raia wa Ivory Coast tayari ana tuzo moja ya ufungaji bora na ile ya mchezaji bora wa mwaka. Alifunga mabao 17 wakati alipotwaa tuzo ya ufungaji bora msimu wa 2012/13 na alifunga mabao 14 msimu uliopita ambayo yaliisaidia timu yake kutwaa ubingwa wa kwanza wa Bara. Kipre amekuwa mfungaji bora wa Azam FC mara mbili mfululizo.

Didier Kavumbagu amefunga mabao mawili katika mchezo wake wa kwanza akiwa na Azam katika ligi kuu, Mrundi huyo alifunga mabao 22 katika misimu miwili aliyoichezea Yanga. Tayari ana mabao 24 katika ligi kuu ya Tanzania. Kavumbagu anaungana na wafungaji bora wa ligi kuu, John Bocco na Kipre katika safu ya mashambulizi ya Azam FC, na mwanzo wake mzuri akicheza na Kipre unaweza kumfanya mshambulizi huyo wa timu ya Taifa ya Burundi kufungfa mabao zaidi msimu huu.
Amis Tambwe ameanza na bao. Alifunga mabao 19 katika michezo 23 msimu uliopita na bao lake dhidi ya Coastal Union katika sare ya kufungana mabao 2-2 Jumapili iliyopita ni bao la 20. Je, Tambwe ni bora zaidi kuliko washambuliaji wote wa kigeni? Inaweza kuwa hivyo lakini upande mwingine uwezo wa Kipre ni mkubwa mmno kuliko mshambulizi yeyote nchini. Azam inajivunia kuwa naye kutokana na mchezaji huyo kuwa mtulivu, msikivu, mwenye nidhamu na mtu anayetambua vyema majukumu yake nchini.
Wote watatu ni wafungaji –hasa, Tambwe ni mmaliziaji mzuri, Kavumbagu pia ni mfungaji ambaye si rahisi kupoteza nafasi mbili mfululizo anazopata. Wawili hao hucheza pamoja katika kikosi cha Burundi. Kavumbagu hutumia nguvu anaporuka juu kuwania mpira, Tambwe ni mchezaji mwenye ‘ target’ hufunga mabao ya kichwa, hujipanga vizuri katika maeneo ya hatari hivyo kumfanya kuonekana ni mshambulizi anayefunga sana. Tambwe yupo juu ya wote kulingana na takwimu zake lakini yeye husubiri kutengenezewa na wachezaji wenzake kama ilivyokuwa kwa mshambulizi wa zamani wa Kimataifa wa Holland na klabu za Manchester United na Real Madrid, Ruud Van Nistelrooy.
Kipre hucheza pande zote za uwanja. Alitumika kama kiungo wa pembeni katika nusu msimu wake wa kwanza. Alifunga mara tatu. Msimu wa 2011/12 alifanikiwa kufunga mabao yasiyopungua sita akicheza kama msaidizi wa Bocco ambaye alitwaa kiatu cha dhahabu akiwa na mabao 16. Washambuliaji hawa watatu wa kigeni ni bora zaidi ya wote katika ligi kuu ya Bara. Mmoja wao anaweza kutwaa tuzo ya ufungaji bora msimu huu.

Post a Comment

AddThis

 
Top