0
Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia, Goran Kopunovic, amefanikiwa kuweka rekodi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayomalizika kesho Jumanne visiwani Zanzibar.



Kopunovic aliyechukua mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri aliyeondolewa kukinoa kikosi cha Simba mwishoni mwa mwaka jana, ameiongoza timu hiyo kushinda michezo minne mfululizo ya Kombe la Mapinduzi, rekodi ambayo haijafikiwa na kocha yeyote katika michuano hiyo.

Maana yake iwapo atashinda mechi ya kesho ya fainali dhidi ya Mtibwa Sugar ataishindilia rekodi hiyo kuwa bora kwa kushinda mechi tano mfululizo na akipoteza, itakuwa mechi yake ya kwanza kupoteza katika michuano hiyo.

Awali Simba ilianza kwa kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa wakati kocha huyo akiwa jukwaani akishuhudia huku kocha msaidizi, Selemani Matola akiwa analiongoza benchi hilo la ufundi.

Baada ya mchezo huo, Kopunovic akaanza kuiongoza Simba kuifunga Mafunzo bao 1-0 halafu wakapata ushindi kama huo dhidi ya JKU, michezo yote hiyo ikiwa ni ya makundi.


Katika hatua ya robo fainali wakaitandika Taifa Jang’ombe mabao 4-0 na juzi Jumamosi wakafanikiwa kuingia fainali kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi ya Zanzibar, kama Simba wakifanikiwa kuifunga Mtibwa kesho Jumanne kwenye mchezo wa fainali basi kocha huyo atakuwa amemaliza michuano hiyo akiwa hajapoteza wala kutoa sare mchezo wowote tangu aanze kuinoa Simba.

Post a Comment

AddThis

 
Top