0

Kufuatia ‘ sintofahamu’ na mgogangano ambao umekuwepo katika siku za hivi karibuni kuhusiana na namna uhalali na uendeshwaji wa Bodi ya Ligi kuu nchini, nilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi hiyo , Yahaya Ahmed ambaye ametoa ufafanuzi mzuri ambao unaelezea mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya Bodi hiyo, Maswali na majibu mengi yenye ufafanuzi utayapa katika ‘ mahojiano haya maalumu’

Habari yako Mwenyekiti. Kuna mambo mawili/matatu ambayo tunahitaji ufafanuzi kutoka kwako kama Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi. Kwanza tungependa kufahamu kitu gani ambacho kimekwamisha mkutano mkuu wa Bodi ya LIgi kushindwa kufanyika licha ya ligi kuu Tanzania Bara kumalizika msimu uliopita?

YAHAYA; Mkutano mkuu wa bodi huwa haufanyiki mara baada ya kumalizika kwa msimu. Kuna mipango yake, mkutano mkuu wa bodi unafanyika mara moja kwa Mwaka na tayari tumepanga kuufanya . Katika hili si mambo ya ligi bali katiba ndiyo inasema hivyo.

Lini mmepanga kufanya hivyo?
YAHAYA; Tarehe 15, Novemba ( mwezi ujao)

Utakuwa na ajenda zipi?
YAHAYA; Ajenda zake ni nyingi lakini kubwa itakuwa ni kujadili kujaza nafasi ya Mkurugenzi ambaye amekosa sifa za kuendelea kushikilia nafasi hiyo. Tutatazama mahesabu ya Mwaka mzima, masuala ya uendeshaji wa Bodi ya ligi, na vilevile mkutano utapisha uelekeo wa ligi kuwa chini ya chombo huru. Moja ya majukumu waliyopewa Bodi ya ligi mwaka jana ni kutengeneza ‘ Chombo huru katika ligi ya Tanzania’. Hizo ndizo ajenda kuu ambazo zitazungumzwa katika mkutano mkuu.

Je, wewe utaachia nafasi yako ‘ eti, kwasababu tu’ timu yako ya Mtibwa Sugar ilimaliza nje ya nafasi sita za juu katika ligi kuu msimu uliopita?
YAHAYA; Katiba haisemi hivyo, Wakurugenzi wa kwanza watapatikana kwa kuangalia msimamo wa ligi iliyopita, nikimaanisha timu sita zilizomaliza katika nafasin za juu ni waanzilishi wa Bodi hivyo katiba inasema kuwa kila baada ya miaka minne utaratibu huo utakuwa ukitumika. Mlimbikizo wa matokeo ya timu kwa misimu minne mfululizo ndiyo unatoa wawakilishi sita ambao wanaunda Bodi ya ligi. Hatufanyi hivyo kila msimu ndiyo maana unaona Mbeya City FC hawapo katika Bodi licha ya kumaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita.

Kwa hiyo unamaanisha kuwa mabadfiliko katika Bodi ya ligi hufanyika kila baada ya miaka minne na si kila msimu kama inavyosemwa na baadhi ya wadau?
YAHAYA; Uongozi wote wa ‘ Primier League Board’ unabadilika kila baada ya miaka minne. Ndivyo ilivyo kwa sababu ‘ unachaguliwa’ . Labda niongeze kitu; wakati tunaanzisha Bodi ya ligi kuu, wakati ule watu sita wa mwanzo watapatikana kutokana na timu zilizomaliza nafasi ya kwanza hadi ya sita. Kwa msimu uliomalizika kabla ya uchaguzi, na watu hao watakaa katika ofisi kwa muda wa miaka minne, ila endapo timu itashuka daraja itapoteza sifa hiyo, mfano ni Pamba FC iliyokuwa ligi daraja la kwanza. Nafasi hiyo itajazwa katika mkutano mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

Kwa mtazamo wako ‘ binafsi’ unafikiri Bodi ipo katika ‘ Muundo sahihi’?
YAHAYA; Siwezi kukujibu hilo, Katiba ndiyo inatakiwa ‘ iseme’. Katiba imeundwa hivyo na imesainiwa na rais wa TFF. ‘ Namna ya kuwapata viongozi unaangalia matokeo ya miaka minne mfululizo ya timu katika ligi’ na si mwaka mmoja. Timu iliyoingia katika nafasi sita za juu kwa miaka minne itakuwa inafaa kuingia katika Bodi. Coastal Union, Mtibwa Sugar wameendelea kuwa katika Bodi ingawa walikuwa nje ya nafasi sita msimu uliopita. Hivyo mtazamo wangu ‘ hautakuwa na maana’ kwa kuwa katiba inesema hivyo.

Moja ya mapungufu yaliyopo katika uongozi wenu ni uwepo wa watu walewale ambao walichaguliwa na rais Leodgar Chilla Tenga wakati akiwa kiongozi wa TFF. Je, nyie mtaachia nafasi zenu kuelekea mchakato wa uundwaji wa chombo huru kitakachosimamia ligi au mtaendelea kuwepo katika kamati kama ilivyokuwa wakati wa mchakato wa uundwaji wa Bodi?
YAHAYA; Muono wa uendeshaji wa soka nchini ni kuelekea kuwa na chombo huru, wakati wa mchakato wa kwanza ulikuwa ni kuunda kamati itakayosimamia, mchakato wa pili ilikuwa ni kuunda Bodi ya ligi ambayo haipo huru. Kiutendaji inafanya kazi yenyewe lakini kiutawala ipo chini ya TFF. Hatua ya tatu ni Bidi yenyewe ya ligi kujikamilisha ili kuwa chombo huru. Ajenda hiyo inaanzia katika Bodi ya ligi, inakwenda katika mkutano mkuu, inakwenda katika kamati ya utendaji baada ya hapo inakwenda TFF huko ndipo litatoka jibu la kukubalika au vinginevyo.

Kwa nafasi yako, una mamlaka ya kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Bodi, Je, tayari umefanya hivyo, ni kina nani?
YAHAYA; Nimepewa nafasi ya kuteua wajumbe wawili lakini kuna sifa maalumu. Nimemteua mjumbe mmoja tu ambaye ni mwanasheria, Damas Ndumbaro ambaye atakuwa akitusaidia mambo ya sheria.
Ooh! kumbe, Dk. Damas Ndumbaro ni miongoni mwa wajumbe uliowateua kwa kuwa ilifahamika awali ni mwanasheria wa vilabu.
YAHAYA; Ndumbaro ni mwanasheria, ni mtu mwenye taaluma ya sheria wa vilabu ambaye vilabu 12 viliamua kumpatia nafasi hiyo wiki mbili zilizopita ili awe anawawakilisha katika mambo yao ya sheria, hakuna ubaya kwa kuwa nafasi yake katika Bodi ya ligi si ya kuajiriwa. Anaruhusiwa kufanya kazi nyingine.
Umezungumzia vilabu 12 vya ligi kuu wakati kuna vilabu 14, je, kuna klabu ambazo hazijakubaliana na hoja hiyo?
YAHAYA; Hakuna klabu iliyopinga, vyote vimekubaliana isipokuwa kuna vilabu ambavyo havikushiriki katika mkutano. JKT Mgambo na JKT Ruvu.
Geofrey Nyange Kaburu anaingiaje katika mkutano mkuu wa Bodi wakati hujamteua?
YAHAYA; Anaingia kwa nafasi ya uwakilishi wa klabu ya Simba SC. Hivyo ameingia kama mbadala wa rais wa klabu yake.

Post a Comment

AddThis

 
Top