0
WANANDINGA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars wana matumaini ya kuwafunga Msumbiji (Black Mambas) katika mechi ya marudiano itakayopigwa kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu kwenye uwanja wa taifa wa Zimpeto mjini Maputo.

Taifa stars ilitoka sare ya mabao 2-2 mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Mambas ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam, hivyo wanahitaji ushindi wa mabao 1-0 au sare ya mabao 3-3 ili kufuzu hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Africa, AFCON, nchini Morocco.
Mlinda mlango namba mbili wa Stars ambaye katika mechi iliyopita alikaa benchi, Aishi Manula amesema kama kama Msumbiji walipata  mabao mawili Dar es salaam nao wanaweza kupata ushindi mjini Maputo.

                          Mlinda Mlango namba mbili wa Taifa stars, Aisha Manula
 
“Watanzania wakitulaumu ni sahihi, wakati fulani sio sahihi kwasababu mpira ni mchezo wa makosa. Ili tufunge lazima Msumbuji wafanye makosa na ili wao wafunge, lazima sisi tufanye makosa”. Alisema Manula.
“Tutajipanga vizuri, wao wameweza kupata mabao mawili kwetu, sisi tunapoenda Msumbiji tutahitaji kupata bao la mapema. Tukishinda ushindi wowote hata moja bila tutasonga mbele”. Aliongeza Manula.
Aidha, mlinda mlango huyo wa Azam fc aliongeza kuwa mpira wa miguu wakati fulani unakwenda na bahati, hivyo Mungu ndiye anajua nini watavuna ugenini.
“Watu wanafikiria tofauti, lakini huwezi kujua nini Mungu ametuandalia . Tuwaombe watanzania waendelea kutuamini kwasababu timu yetu ilivyo, inaweza kupata matokeo mazuri”.
“Makosa madogo madogo yaliyotokea yanaweza kurekebishika na tukafanya vizuri”. Alisisitiza Manula.
Kikosi cha Taifa Stars kinatarajia kuondoka kesho (Julai 24 mwaka huu) kwenda Mbeya ambapo kitapiga kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya marudiano dhidi ya Msumbiji.
 Mechi hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kutafuta tiketi ya kushiriki Fainali za Afrika (AFCON) zitakazochezwa mwakani nchini Morocco itafanyika wikiendi ya Agosti 2 na 3 mwaka huu nchini Msumbiji.
 Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka nchini Julai 31 mwaka huu kwenda Johannesburg, Afrika Kusini ambapo itafanya mazoezi ya mwisho kabla ya kutua Maputo kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa wa Zimpeto.

Post a Comment

AddThis

 
Top