0


Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange `Kaburu`

MAGUMASHI yameendelea kutawala katika usajili wa soka la Bongo ambapo viongozi wanazidi kujifanyia mambo kwa mahaba yao.
Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba mshambuliaji hatari wa Mbeya City fc, Saady Kipanga  anazurula jijini Dar es salaam na makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu ikishinikiza asajiliwe.
Kamati ya usajili ya Simba chini ya mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe haimhitaji Kipanga, badala yake inamtaka mshambuliaji wa Ruvu Shooting ya Pwani, Elias Maguri, lakini Kaburu analazimisha asajiliwe Kipanga.
Kwasababu Kaburu ni makamu wa Rais anaweza kuwa na nguvu ya kumsajili Kipanga, lakini mwisho wa siku sio mahitaji ya timu na atakuwa amefanya hivyo kwa matakwa binafsi na mahaba yake.
Kaburu aliwahi kufanya jambo hili tena katika usajili wa Abdallah Juma na Paul Ngalema kutoka JKT Ruvu. Wachezaji hawa hawakuwepo katika mahitaji ya timu, lakini Kaburu akawasajili na wakaendelea kukaa benchi mpaka wakatimka zao na kujiunga na Mtibwa Sugar.
Kitendo kama hicho kinajirudia tena ambapo Kipanga anataka kuingia katika majanga hayo ya kurubuniwa na kwakuwa anatamaa, atahitaji kupata hela za haraka, lakini nafasi ya kucheza itakuwa finyu.
Kama kweli anataka kusajiliwa kwa `staili` ya magumashi kiasi hicho, bila kujali uhitaji wa timu, ataishia kuharibu kipaji chake.

Mshambuliaji halali wa Mbeya City fc, Saady Kipanga
MAGUMASHI YAKO WAPI KATIKA SUALA HILI?
Saady Kipanga ni mchezaji wa Mbeya City  fc. Alisajiliwa mwezi desemba mwaka jana kutokea klabu ya Rhino Rangers na kupewa mkataba wa miaka miwili.
Kwasasa amebakiza  mwaka mmoja wa kuitumikia Mbeya City fc. Kiutaratibu ni mchezaji halali wa Mbeya City na kama klabu inamhitaji, hakuna jinsi, lazima wafike Mbeya kuzungumza biashara.
Kipanga si mchezaji huru. Yupo mapumziko baada ya Mbeya City fc kuamua kuvunja kambi kutokana na shirikisho la soka Tanzania kusogeza mbele ligi kuu mpaka septemba 20 mwaka huu.
Kaburu anafanya mambo kizamani kwasababu Simba na Yanga zimezoea kusajili kinyume na taratibu. Duniani kote, timu haiwezi kuongea na mchezaji binafsi bila kuishirikisha timu yenye mkataba naye.
Biashara ya Kipanga inaweza kufanyika baina ya klabu ya Mbeya City fc na Simba, lakini si Kaburu na Kipanga. Huu ni `upuuzi` usiotakiwa tena wakati huu Tanzania inahangaika kujinasua katika magumashi ya soka.
Kaburu ni mtu wa mpira na bila shaka anajua kanuni na taratibu za usajili, kwanini ashindwe kuheshimu mkataba wa mtu?
Halafu kwanini atake kumsajili yeye? Kaburu ni kocha?, au ni mjumbe wa kamati ya usajili?
Kiutaratibu, kocha mkuu ndiye anayependekeza wachezaji wa kuwasajili na kupeleka majina kwenye kamati ya usajili.
Leo hii Kaburu anataka kumsajili Kipanga wakati jina la mchezaji lililopo mezani ni Elias Maguri. Kamati ya usajili inamtaka Maguri, kwanini Kaburu ashinikize kusajiliwa kwa Kipanga, kuna nini nyuma ya pazia”
KUTOJITAMBUA KWA SAADY KIPANGA
Kipanga ni miongoni mwa wachezaji waliokosa ueledi kabisa. Kwanini anashindwa kuheshimu mkataba? Yeye ni mchezaji wa Mbeya City fc.
 Kwa maana hiyo kama timu au kiongozi yoyote anamfuata na kuzungumza naye ili amsajili, lazima awaelekeze kwa viongozi wa Mbeya City kwasababu wao ndio wana haki zote.
Kuzurula na kaburu hapa mjini badala ya kuwasiliana na viongozi kama anataka kuichezea Simba ni kukosa elimu tu. Haya ndio matatizo ya wachezaji wa Tanzania.
SOMO KWA KIPANGA
Abdallah Juma na Paul Ngalema walikuwa wachezaji wazuri, lakini walirubuniwa na Kaburu na kusajiliwa Simba. Kiukweli hawakuhitajika na klabu. Wakaishia kukaa benchi na kuua vipaji vyao mpaka wakaamua kuondoka.
Kipanga naye anaingia katika mkumbo huo. Itamgharimu na kipaji chake kitaishia hapo asipojiangalia.
 



Post a Comment

AddThis

 
Top