0


KLABU ya Yanga imembwaga mshambuliaji wake Mganda, Khamis Kiiza ‘Diego wa Kampala’ baada ya kusajiliwa kwa Wabrazil wawili, Andrey Coutinho na Geilson Santos Santana `Jaja`.


 Baada ya Jaja kusaini mkataba wa miaka miwili jana makao makuu ya klabu ya Yanga, kulikuwa na utata ni mchezaji gani atapigwa chini kati ya Kiiza na Emmanuel Anord Okwi.

 Awali ujio wa Jaja ulielezwa kuwaweka kitimoto Kiiza na Okwi, huku mmojawapo akitakiwa kutolewa kafara.

 Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba kocha Maximo amependekeza kuachwa kwa Kiiza kutokana na ripoti iliyoachwa na Hans Van Der Pluijm.

 Mzigo huo uliofuatwa chini ya kapeti unasema kuwa Pluijm katika ripoti yake aliyowasilisha kwa viongozi baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, alisema ili Emmanuel Okwi acheze Yanga sc, lazima Kiiza aondolewe.
 Kwa kuzingatia mapendekezo hayo, Maximo amefuata ushauri huo na sasa Kiiza rasmi anaondoka Jangwani.

 Katika hatua nyingine, imeelezwa na chanzo cha uhakika kuwa Maximo amewabana viongozi wa Yanga akiwataka wajenge uwanja wa mazoezi wa Kaunda ili kuepukana na adhaa anayoipata.

 Maximo amewakazia na amesema hakuna jinsi, lazima uwanja huo ujengwe muda huu.

 Pia amewataka viongozi kuboresha vyumba vya jengo la Jangwani ili wachezaji wote waishe pale.

 Taarifa zinasema, Maximo amesema haiwezekani timu kukaa saa mbili kwenye foleni inapoelekea uwanjani na kurudi kambini.

 Kwa mazingira hayo anataka wachezaji wake wakae makao makuu ya Yanga, mitaa ya Twiga na Jangwani, halafu uwanja  wa Kaunda ujengwe.

 Mbrazil, Marcio Maximo anafahamika kwa kuwa na msimamo mkali katika mambo yake.

Post a Comment

AddThis

 
Top