Tanzania ni miongoni mwa nchi `tia maji tia maji` kwenye mipango ya soka. Viongozi na mashabiki wanataka kupita njia ya mkato `short cut` ili kupata mafanikio.
Moja ya kosa kubwa wafanyalo watu wengi ni kulifananisha soka letu na mataifa yaliyoendelea (barani Ulaya na Amerika). Utasikia mbona hata Chelsea, Man United, Barcelona wanafukuza makocha?, wanaacha wachezaji?.
Kumbe klabu hizi zina mipango na zimekamatwa na wafanyabiashara ambao wamewekeza pesa zao. Hakuna mfanya biashara atayevulimilia hasara. Mtu anainunua klabu kwa mabilioni ya fedha, mfano Roman Abramovich wa Chelsea. Hawezi kuona kocha anavurunda na kumuacha, lazima achukue hatua kwasababu anataka faida.
Pia klabu za Ulaya, mara nyingi kazi ya kocha ni kutengeneza timu kiuchezaji, (ufundi na mbinu za mpira). kwa asilimia kubwa, wachezaji wanaowakuta wanakuwa tayari wameandaliwa vizuri au ananunua wachezaji waliopikwa tayari. Kwa maana ya kwamba, wana misingi ya mpira, kazi yake inabaki kuunganisha timu kwa kutumia wachezaji walio tayari kufanya kazi.
Kama kazi yako ni kuufundisha mpira na kuunganisha wachezaji katika falsafa yako, yaani wachezaji wote ni wazuri, inashindikanaje kufukuzwa unaposhindwa kuwapa mbinu sahihi za mpira?. Ndio maana makocha wengi Ulaya wanawajibishwa kwa kushindwa kuipa mbinu za uhakika timu yake.
Kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia, Zdravko Logarusci (wa kwanza kushoto)
Leo hii huwezi kufananisha klabu za Tanzania (Simba, Yanga) na klabu za Ulaya. Simba na Yanga ni klabu kongwe na kimsingi zinapendezesha soka la Tanzania. Hizi ni klabu za wanachama, kwa msingi huo, wanachama wana nguvu kubwa na wanaweza kuleta athari hata kwa benchi la ufundi.
Unajua siku zote, watu wanaochaguliwa kwa kunyoshewa vidole na wananchi au wanachama, kwa asilimia kubwa wanawajibika kwa watu hao. Leo hii Mbunge hawezi kuwadharau wananchi wa jimboni kwake kwasababu anajua kuna uchaguzi unakuja.
Leo hii kiongozi wa klabu ya Simba au Yanga anachaguliwa kwa kupigiwa kura na wanachama. Halafu ana malengo ya kugombea tena baada ya muda wake kumalizika, anashindwaje kukubaliana na matakwa ya wanachama hata kama si ya kimpira?
Mara nyingi utawasikia mashabiki na wanachama wa klabu hizi wakitoka povu kwa kuwakandia makocha na wachezaji, mara fulani hafai, kocha fulani fukuza, mchezaji fulani ameshuka kiwango, au kwanini kocha hampangi fulani.
Kitaalamu, kocha ndiye mwamuzi wa mwisho kuamua mchezaji gani anapangwa na nani hapangwi. Yeye anachagua kikosi. Hata katika usajili, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuagiza nani asajiliwe na nani aachwe na si viongozi.
Leo hii Jose Mourinho, Aserne Wenger, Brendan Rodgers akiamua kumnunua mchezaji, anapeleka pendekezo lake kwa viongozi, wanaangalia kapuni kama kuna kitita, kama mzigo upo wanaingia sokoni. Kama watashindwa bei, watamwambia kocha hatutamnunua
Kama tunapenda kujifananisha na ulaya, basi hata hili tujaribu basi kujifananisha. Kwanini watu wanaoitwa `Friends of Simba` (F.O.S) wamsajilie mwalimu timu au kwanini Yusuf Manji na wenzake wamsajilie kocha wachezaji? Huu ni uzamani kabisa.
Lazima kila mtu afanye majukumu yake. Inafika wakati, hakuna njia ya mkato zaidi ya kuzibadili Simba na Yanga kuwa katika mfumo wa kampuni na si klabu ya wanachama.
Yanga wamemleta nchini Marcio Maximo. Kocha huyu alikuwa anaifundisha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kuanzia mwaka 2006 mpaka 2010. Kwa wenye kumbukumbu nzuri, Mbrazil huyu ana msimamo mkali hasa linapofika suala la nidhamu kwa wachezaji.
Maximo yupo na Wabrazil wenzake watatu kwa maana ya msaidizi wake Leonado Neiva, na wachezaji wawili raia wa Brazil, Geilson Santos Santana na Andrey Coutinho ambao wote walisaini mkataba wa miaka miwili.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu anasema wachezaji wote ni mapendekezo ya kocha Maximo na wao wanajitahidi kutekeleza. Kama ni kweli, basi ni jambo zuri katika utendaji wa kazi, hasa muda huu ambao soka linakwenda kisasa zaidi.
Maximo anaonekana kuaminiwa na kuheshimiwa sana na viongozi wa Yanga na mashabiki. Hii inatokana na historia yake. Lakini haiondoi ukweli kuwa kocha huyu anahitaji kupewa muda ili kufikia malengo.
Kwa upande wa Simba, mengi yanazungumza. Wanaye kocha Mcroatia, Zdrvako Logarusic. Jamaa huyu ni mtu mwenye msimamo mkali, hakika Loga hana mchezo kwa wachezaji.
Hawezi kumvumilia mchezaji anapofanya vibaya. Ni kocha sahihi kwa aina ya wachezaji wa Kitanzani. Wanandinga wengi nchini si waumini wa nidhamu ya mpira, hivyo aina ya makocha kama Loga ni muhimu. Lakini kuna mambo tofauti yanazungumzwa.
Viongozi wa Simba wanasema wapo katika mazungumzo na Loga ili wampe mkataba mwingine wa miaka miwili baada ya ule wa awali wa miezi sita kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.
Suala la Loga kupewa mkataba lilianza wakati wa uongozi wa Ismail Aden Rage, walisema kila kitu kimekwenda sawa na atakaporudi kutoka mapumzikoni itakuwa ni kumwaga wino tu.
Hata Rais Evans Aveva alipoingia madarakani, alisema uongozi wake hautamfukuza Loga, lakini siku za karibuni kumekuwepo na taarifa za chini kwa chini kuwa uongozi wa Simba unataka kuachana na Loga na upo katika mazungumzo na kocha wa Gor Mahia ya Kenya, Bobby Williamson.
Viongozi wao wanadai wapo katika mazungumzo ya kumuongezea mkataba, lakini taarifa kutoka vyanzo makini zinadai Loga anaweza kufungashia virago.
Sababu kubwa inayoelezwa ni kwamba Loga anakataa wachezaji wanaoletwa na viongozi kwa ajili ya kusajiliwa. Sasa wanaona anawasumbua tu, bora wakatafuta kocha mwingine.
Kundi la `Friends of Simba` (F.O.S) kwa muda mrefu limekuwa likishutumiwa kuwa na tabia ya kuwasajiliwa makocha wachezaji, na wanafika mbali mpaka kuwapangia timu ya kucheza.
Kocha wa zamani wa Simba, Mserbia, Milovan Circovic aliwahi kulalamika kuwa viongozi walikuwa wanampangia timu. Hata usajili, viongozi walifanya wao.
Hili ni tatizo na kirusi kikali cha soka la Simba. Kama watu hawa wataendekeza tabia hii katika uongozi wa Aveva, basi watashindwa vibaya mno kufikia malengo yao.
Loga ndiye mwenye uamuzi wa mwisho, mchezaji gani asajiliwe na nani aachwe. Viongozi mnamleteaje wachezaji? Kwani hakupendekeza?
Kama kweli aliwapa ripoti na mapendekezo ya wachezaji anaowataka, inakuwaje akatae kuwachukua watu aliowapendekeza? Hapa kama kuna kamchezo fulani.
Nadhani kuna watu wanaendelea na utaratibu wa kujisajilia tu. Kocha kumkataa mchezaji sio tatizo. Labda kuna mengine nyuma ya pazia. Mwisho wa siku yeye atalaumiwa kwa timu kufanya vibaya, ndio maana anakuwa makini kuwaangalia wachezaji.
Kama Simba itamfukuza Loga, athari ya kufukuza makocha itaendelea kuwatafuna kwa msimu mwingine. Kumbuka ndani ya miaka mitatu au minne, tayari makocha wanne wameshatimuliwa.
Kuanzaia kwa Cirvociv, ndani ya muda mfupi akaja Patric Liewig kutoka Ufaransa,alikaa nusu msimu na kufukuzwa. Baadaye akackuliwa Abdallah Kibadeni , naye akaiongoza timu nusu msimu uliopita na kufukuzwa na sasa Loga.
Kama Loga anafukuzwa, manake ameiongoza timu kwa nusu msimu. Manake atakamilisha idadi ya makocha watatu (Liewig, Kibadeni, Loga) kuiongoza Simba kwa nusu msimu ndani ya muda mfupi.
Unadhani kwa staili hii Simba itakwenda mbele? Hata aje Mourinho, Van Gaal, Guardiola, hakuna mafanikio kama tabia hii itaendelea. Simba inahitaji kukaa na makocha kwa muda mrefu ili kujijenga upya.
Maamuzi pekee nitakayoyaunga mkono ni kusikia Loga amesaini mkataba na sio tumeshindwa kufikia makubaliano.
Kama viongozi watakuja na kauli hiyo, binafsi sitaamini kwasababu taarifa zilishavuja kuwa Loga hatakiwi kwasababu anakataa wachezaji wanaoletwa na viongozi.
Kila la Kheri Simba kuelekea michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Post a Comment