Mbwana Samatta (kushoto) ni miongoni wa wachezaji wa Taifa Stars wanaotegemewa kuleta matokeo mazuri
TAIFA Stars imeondoka jana kwa ndege ya Air Tanzania kuelekea Afrika kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kutua Mjini Maputo kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Msumbiji ,kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
Ikiwa nchini Afrika kusini, Stars itajikamilisha kwa wanandinga wake wawili wanaocheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kujiunga na wachezaji wenzao.
Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini Qatar yeye alishajiunga na timu tangu ikiwa Dar es salaam.
Mechi hiyo itachezwa Agosti 3 mwaka huu uwanja wa Taifa wa Zimpeto uliopo nje kidogo ya mji mkuu wa Maputo na Stars inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele.
Taifa stars ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Msumbiji julai 20 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Baada ya mechi hiyo, kikosi kiliweka kambi mjini Tukuyu kwa malengo ya kufanya marekebisho ya makosa yaliyojitokeza.
Bila shaka baada ya sare ya Dar es salaam, benchi la ufundi limefanya uchambuzi wa makosa yaliyojitokeza na kutafuta mbinu mpya za kuwatoa Msumbiji.
Stars ikiwa Dar es salaam ilikuwa na mpango wa kushinda na kujilinda ili isifungwe, lakini ikaambulia sare na sasa mpango umebadilika.
Inakwenda Msumbiji kutafuta ushindi tu, kwa maana hiyo lazima kocha mkuu Mholanzi Mart Nooij kwa kusaidiana na Salum Mayanga wameshatafuta mbinu mpya za kuwatoa Msumbiji.
Taifa stars inahitaji ushindi Msumbiji, lakini inashindaje? hilo ni juu ya benchi la ufundi.
Thomas Emmanuel Ulimwengu atakuwepo katika mapambano ya kuwatoa Msumbiji
Kocha hatakiwa kulaumiwa kwa matokeo yoyote, kwasababu kuna wakati fulani makocha wanawapa mbinu wachezaji, lakini wachezaji hao hao wanashindwa kuelewa na kuzitumia, hivyo lengo mama halipatikani.
Mechi ngumu ya Msumbiji inatakiwa kila upande ufanye kazi yake vizuri. Kama kila upande unatekeleza majukumu yake kwa asilimia 100, basi ushindi utapatikana.
Ili kufikia kilele cha mafanikio, kila mdau anatakiwa kuchangia kwa asilimia 100. Kwa mfano tujifunze kwa Ujerumani ambao wamefikia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa kombe la dunia.
Wengi wanadhani Ujerumani wamefikia mafanikio yale kwasababu ya umahiri wa wachezaji kama Toni Kroos, Thomas Muller, Phillip Lahm na wengineo pamoja na benchi zima la ufundi linaloongozwa na kamanda mkuu Joachim Low
Eneo la Bahia ambapo Ujerumani waliweka kambi
Kumbe mambo ni tofauti. Ujerumani walipoona mashindano yanakwenda kufanyika Brazil, waliamua kutuma mtaalamu wa mazingira aliyeenda kuisoma Brazil na Amerika kusini kwa ujumla. Walihitaji kujua hali ya hewa ikoje na ni eneo gani litakuwa zuri kwa timu kukaa ili kurahisisha safari za kwenda viwanja mbalimbali watakavyocheza.
Mtaalamu aligundua kuwa eneo la Bahia ni zuri sana, lina hali ya hewa nzuri, na ni rahisi kwa usafiri wa ndege ili kufika viwanja mbalimbali.
Baada ya mtaalumu yule kurudisha ripoti, chama cha soka nchini Ujerumani DFB kwa kushikiriana na wadhamini, wakaenda kujenga kambi yao maeneo ya Baia ambapo waliweka vifaa vyote vya mazoezi na uwanja.
Kocha Joachim Low na Meneja mkuu wa timu ya Ujerumani, Oliver Bierhoff walifurahia kambi ya Bahia na kuweza kutimiza majukumu yao vizuri, hivyo kujenga morali kubwa kwa wachezaji wao.
Baada ya uwekezaji mkubwa kiasi kile, kwa kila mdau kutimiza majukumu yake, Ujerumani ikafikia kilele cha mafanikio.
Hata sisi Tanzania tunaweza kujifunza. Sio kulaumu makocha tu pale timu inapofanya vibaya. Lazima tujiulize, kila mdau anayehusika anatimiza majukumu yake kwa asilimia 100?
Je, TFF wanaandaa mazingira ya timu kufanya vizuri. Wanawajibika kwa asilimia mia moja? Kama hapana, basi nao wanatakiwa kubeba mzigo wa lawama.
Pia lazima tujiulize, wadhamini wanatoa pesa kwa wakati ili kurahisisha mazingira ya timu kufanya vizuri? Posho ya wachezaji inatoka kwa wakati? kambi inawekwa kwa wakati? Kama jibu ni hapana, basi nao wadhamini wanatakiwa kulaumiwa kwa matokeo mabaya ya timu.
Hatusemi wadhamini hawatimizi wajibu wao kwa wakati na kwa asilimia 100, lakini ni angalizo tu kuwa tujifunze kwa wenzetu ili kufikia malengo yetu.
Kuwalaumu wachezaji na makocha haitasiaidia, lazima tuhakikishe kila mdau anayehusika anatimiza majukumu yake.
Taifa stars kama itacheza kwa uangalifu na kufuta makosa yalitokea mechi ya kwanza, inaweza kupata matokeo mbele ya ‘Black Mambas’.
Kila la kheri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars.
Post a Comment