0
MIAMBA ya soka ya DR Congo, AS Vita wameanza vyema kampeni zao za ligi ya mabingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya miamba ya Misri, Zamalek, mjini Kinshasa usiku wa jana.
 Ni wiki moja tu imepita tangu maafa yalipotokea katika uwanja huo, lakini AS Vita waliweza kuwafumua Zamalek wenye uzoefu mkubwa wa michuano hiyo.
 Tukio hilo la mashabiki kupoteza maisha lilitokea katika mchezo wa ligi kuu ya Congo, kati ya AS Vita dhidi ya wapinzani wao wakubwa TP Mazembe ambapo wenyeji walilala bao 1-0.
 Katika mchezo wa jana, bao la kwanza la AS Vita lilifungwa na Ndombe Mubele dakika ya 19 kipindi cha kwanza na goli hilo lilidumu mpaka dakika za lala salama.
 Moamen Zakaria aliisawazishia Zamalek bao hilo dakika ya 80 na ubao wa magoli kusomeka 1-1 na kuwapa matumaini makubwa Mafarao hao.
 Dakika mbili tu baadaye, AS Vita waliandika bao la pili na la ushindi kupitia kwa Emmanuel Ngudikana na kuwafanya wacongo hao wawe kileleni mwa kundi A.
 Wiki hii, Zamalek wataikaribisha Al Hilal ya Sudan , wakati TP Mazembe na Vita watakutana katika DRC `Dabi`.

Post a Comment

AddThis

 
Top