0


Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, Dar Young Africans wameibuka na ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara uliopigwa jioni hii uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Yanga walikuwa wa kwanza kuliona lango la Kagera Sugar katika dakika ya 3 ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Mganda Hamis Kiiza `Diego` kufuatia kumalizia krosi nzuri iliyochongwa na winga machachari, Mrisho Khalfan Ngasa.

Yanga waliandika bao la pili katika dakika ya 34 kupitia kwa mshambuliaji wao raia wa Burundi, Didier Kavumbagu.

Kagera Sugar walifunga bao la  kufutia machozi katika dakika ya 63 kupitia kwa Daudi Jumanne baada ya beki wa pembeni wa Yanga, Oscar Joshua kuzembea kuosha mpira katika eneo lao la hatari.

Kwa matokeo hayo, Yanga wanafikisha pointi 52 baada ya kucheza mechi 24, pointi moja nyuma ya vinara Azam fc walioshindwa kucheza mechi yao ya 24 leo hii dhidi ya Ruvu Shooting baada ya mvua kubwa kunyesha na uwanja wa  Mabatini mkoani Pwani  kuwa katika hali mbaya.

Mchezo wa leo ulikuwa muhimu kwa Yanga, hivyo wamepambana nadani ya dakika zote 90 kutafuta ushindi, ingawa Kagera Sugar walionekana kuwa imara kwa kiasi kikubwa.

Kosakosa kwa timu zote zimeshuhudiwa ndani ya uwanja wa Taifa, na dakika za lala salama Kagera walikuwa wanawashambulia Yanga kutafuta bao la pili la kusawazisha, lakini mabeki walikuwa makini kuzuia hatari hizo.

Hata hivyo, yanga wangepata mabao mengi zaidi kama isingekuwa uzembe wa washambuliaji wake, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa na Hussein Javu.

Kwa nyakati tofauti, washambuliaji hawa walipata nafasi za kufunga, lakini walipungukiwa maarifa ya kumtungua kipa wa Kagera Sugar, Agaton Antony.

Sasa Yanga wamebakiza mechi mbili dhidi ya JKT Oljoro mwishoni mwa wiki hii katika uwanja wa Shk. Amri Abeid jijini Arusha, na watafunga msimu na Simba aprili 19 mwaka huu uwanja wa Taifa.



Hali ya uwanja wa Mabatini ilikuwa namna hii leo

Ili kutetea ubingwa wao, Yanga wanatakiwa kushinda mechi zote mbili, huku wakiwaombea dua mbaya Azam fc wenye michezo mitatu mkononi.

Endapo Yanga watashinda mechi zao mbili walizobakiza,  watafikisha pointi 58 ambazo Azam fc wataweza kuzivuka kama watashinda mechi mbili tu kati ya tatu walizosaliwa nazo.

Nafasi ya ubingwa bado ni wazi na mpaka sasa huwezi kutabiri nani atatwaa ndoo msimu huu.

Mechi nyingine ilitakiwa kupigwa katika dimba la Mabatini,  Mlandizi mkoani Pwani baina ya wenyeji wa uwanja huo, Maafande wa Ruvu Shooting dhidi ya Vinara Azam fc, lakini mechi hiyo imeahirishwa mpaka kesho baada ya mvua kubwa kunyesha na kuharibu mandhari ya uwanja huo na sasa mechi hiyo atachezwa hapo kesho.

Licha ya Yanga kushinda leo, Azam fc bado wapo kileleni kwa pointi moja zaidi ya Yanga, lakini wana michezo mitatu mkononi.

Kama watashinda mchezo wao wa 24 hapo kesho, basi watakuwa wanahitaji pointi tatu tu katika mechi mbili zitakazobaki ili kujitangazia ubingwa msimu huu.

Mechi ya kesho itakuwa na ushindani mkubwa kwa Azam fc kutokana na rekodi ya Ruvu Shooting katika dimba la Mabatini ambapo wanaonekana kuwa wagumu na hutoa ushindani mkubwa zaidi.

Baada ya mechi ya kesho, Azam fc mwishoni mwa wiki watasafiri kwenda Mbeya kuwafuata wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City katika dimba la Sokoine jijini humo.

Hii itakuwa mechi ngumu zaidi kwa kocha Joseph Marius Omog wa Azam fc kwasababu Mbeya City wapo katika ushindani wa nafasi ya pili msimu huu.

Pia hawana rekodi ya kufungwa katika dimba lao tangu kuanza kwa msimu huu.

Si Yanga wala Simba aliyetoka na pointi tatu katika uwanja huo mgumu kwa timu vigogo.

Baada ya Mbeya, mechi ya mwisho kwa Azam fc itakuwa aprili 19 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi, aprili 19 mwaka huu.

Post a Comment

AddThis

 
Top