Waziri wa Habari, vijana, utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara (katikati) alipokutana na kamati ya maandalizi ya ziara ya magwiji wa Real Madrid nchini leo ofisini kwake jijini Dar es salaam
SERIKALI imeahidi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa ziara ya magwiji wa Real Madrid maarufu kama ‘Real Madrid Legends’ wanaotarajia kutua nchini Agosti 22 mwaka huu na kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya kikosi maalumu cha nyota wa Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo, Dkt. Fenella Mukangara alipotembelewa na kamati ya maandalizi ya ziara hiyo katika ofisi yake katikati ya jiji la Dar es salaam.
Lengo la kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Farough Baghozah kumtembelea waziri ilikuwa ni kumueleza rasmi juu ya tukio hilo kubwa la kihistoria.
Wiki iliyopita, kamati hiyo ilimtembelea mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Saidy Mecky Sadick na kumjulisha ujio wa magwiji hao ambapo kwa upande wake alifurahishwa na tukio hilo na kusema Dar es salaam ipo tayari kuwapokea.
Sadick aliahidi kutoka ushirikiano mkubwa ikiwemo kuhakikisha suala la ulinzi na usalama kwa wakati wote ambao magwiji hao watakuwepo jijini Dar es salaam linaimarisha kwa kiwango cha juu.
Meneja wa ziara hiyo, Dennis Ssebo amesema wamepokelewa vizuri na Dkt. Fenella ofisini kwake na amesema serikali itashirikiana kwa ukaribu ili kufanikisha suala hilo.
“Tumekaribishwa vizuri na mheshimiwa Dkt. Fenella na amesema serikali inalipokea kwa mikono miwili tukio hili kubwa na la kihistoria”. Alisema Ssebo.
Mbali na kucheza mechi ya kirafiki Agosti 23 mwaka huu, magwiji hao watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini ikiwemo kupanda Mlima Kilimanjaro.
Magwiji hao wanakuja nchini kwa mwaliko wa kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Farough Baghozah.
Mreno, Luis Madeil Figo amethibitisha kuja nchini katika ziara hiyo, huku waratibu wakifanya mawasiliano na wachezaji wengine ili kuangalia uwezekano wa kuwapata.
Miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kutua nchini ni pamoja na Wabrazil Roberto Carlos na Ronaldo De Lima, Mfaransa Zidedine Zidane, Muitaliano, Fabio Cannavaro, na wengineo.
Vodacom Tanzania ni miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza kudhamini ziara hiyo. Mengine ni Fastjet, Tropical, Pembe Flower, Lake Gas, EFM Radio na Ladger Plaza Bahari Beach.
Post a Comment