0
Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Dk Valentino Mokiwa.
 
Waumini wa Kanisa la Anglikana la Watakatifu wote Temeke, jana nusura wazipige wakati ibada ikiendelea ambapo hali hiyo ilijitokeza baada ya kusomewa barua ya utambulisho wa Padri Samweli Kilango ambaye waumini hawamtaki kwa madai ya ufujaji wa fedha.

 
Baada ya kusomwa barua hiyo na Katibu wa Kanisa hilo, Hamuli Kapungu, ndipo mtafuruku ukaanza ambapo mmoja wa waumini alitoka mbele, kuchukua kipaza sauti na kusema kwa sauti kubwa mbele ya waumini wenzake kuwa hawamtaki mchungaji huyo.
 
Wakizungumza na Mwandishi kanisani hapo Dar es Salaam jana, waumini hao walimshangaa Askofu wa Kanisa hilo Jimbo la Dar es Salaam Valentino Mokiwa wakidai ameshindwa kusikiliza malalamiko ya waumini wa kanisa hilo kwa sababu mchungaji huyo tayari ameshakataliwa katika makanisa matatu lakini Askofu anashindwa kuchukua hatua dhidi yake.
 
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema wao kama waumini wa kanisa hilo, hawamtaki kiongozi huyo kutokana na tabia zake lakini kubwa zaidi ni mfujaji wa fedha za kanisa.
 
Walisema mchungaji huyo tayari amekataliwa kwenye Kanisa la Anglikana Buza na Tabata Kisukuru lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa badala yake anapewa uhamisho.
 
Waliongeza kuwa, kitendo cha Askofu Mokiwa kushindwa kusikiliza kero za waumini wake dhidi ya mchungaji huyo, hali hiyo imesababisha waumini kuhama kanisa hilo na kwenda kusali makanisa mengine.
 
Chanzo hicho cha habari, kilisema sababu ya Askofu Mokiwa kufumbia macho tabia za mchungaji huyo ni ukaribu wao hivyo ni vigumu kumchukulia hatua kama wanavyotaka waumini.
 
Akijibu tuhuma hizo, Mchungaji Kilango alisema hizo ni mbinu za shetani zinazoingia makanisani na kama waumini hawawezi kumsikiliza Mungu au kiongozi waliyemteua inakuwa tatizo.
 
Alisema kwa mujibu wa kanuni za kanisa hilo, yeye ni mtawala wa kanisa pia ni mchungaji hivyo ni jukumu lake kuwaongoza waumini bila ubaguzi wa kikabila wala itikadi yoyote.

"Sina haja ya kueleza kwanini nimetoka Tabata Kisukuru au Buza na anayetaka kujua kwanini nimetoka huko basi aende kwa Askofu Mokiwa, sihitaji kutetewa na mtu yeyote wala rafiki kwani Mungu hakunituma kuja kusifia watu bali kufanya kazi yake," alisema.
 
Baada ya sakata hilo, Mwandishi  alifanya jitihada za kumtafuta Askofu Mokiwa kwa lengo la kujibu tuhuma hizo za waumini wa kanisa lake na baada ya kumpata, alisema hakuwa na taarifa zozote za malalamiko hayo hivyo hawezi kujibu chochote.

Post a Comment

AddThis

 
Top