0
PHILIPP Lahm amefichua siri kuwa alipanga kustaafu soka la kimataifa siku nyingi kabla ya kutwaa kombe la dunia akiwa nahodha wa Ujerumani.

 Nyota huyo mwenye miaka 30 aliushitua Ulimwengu wa soka baada ya kutangaza maamuzi ya kustaafu soka la kimataifa baada ya mashindano ya kombe la dunia , huku ikisalia miaka miwili tu kufikia fainali za mataifa ya Ulaya mwaka 2016.
 Lakini mchezaji huyo wa Ujerumani aliamua kustaafu ili kuwaacha vijana wenye vipaji waiongoze Ujerumani miaka ijayo.

 Lahm aliuambia mtandao wa Fifa.comkuwa alikuwa polepole, lakini maamuzi hayo aliyafikia msimu uliopita na alifahamu kuwa atastaafu baada ya kombe la dunia.
 “Nina furaha kubwa kumaliza soka langu la kimataifa nikibeba kombe la dunia nchini Brazil. Kwa heshima yangu, ni wakati muafaka wa kuacha soka la kimataifa”.
 “Timu ni nzuri, ina wachezaji wengi wazuri, kuna vijana wadogo wanakuja, acha na wao wapate nafasi ya kutanua mbawa zao”.

 Lahm alicheza nafasi zote, kama kiungo wa Ulinzi na beki wa kulia wakati wa mashindano ya kombe la dunia nchini Brazil, lakini aligoma kutajwa kama mchezaji wa soka aliyekamilika, akitaja mapungufu yake katika sehemu ya kushoto.
 “Naweza kusema wazi kuwa beki ya kushoto ilikuwa ngumu kucheza na kulitokea krosi nyingi upande wangu,” alisema. “Kwahiyo sitacheza beki ya kushoto tena. Madhaifu yangu ya beki ya kulia na kiungo wa ulinzi siwezi kuyataja. Ni juu ya wapinzani wangu kuyatafuta”.

 Nyota huyo wa Bayern pia alieleza kuwa amekuwa katika mkakati wa kuendeleza soka la Ujerumani kwa miaka 10 na kuiongoza kutwaa kombe la dunia, akitolewa mfano kuwa kuna uhusiano mzuri katika timu ya taifa na klabu za Bundesliga. 
“Kiukweli tumenufaika sana na uwezekezaji wa soka la vijana nchini Ujerumani kwa miaka 10 hadi 15,” alisema.
“Kila klabu ya Bundesliga ina akademi bora, mafunzo ni mazuri na ya kitaalamu na tuna muda wa kutosha na makocha wenye sifa zote”.

Post a Comment

AddThis

 
Top