0
KAKA amesisitiza kuwa kamwe hajutii maamuzi yake ya kujiunga na Real Madrid na anahisi muda aliokaa klabuni hapo ulikuwa wa mafanikio.

Kiungo huyo mshambuliaji alijiunga na Real Madrid akitokea AC Milan kwa ada inayoaminika kuwa Euro milioni 65, lakini hakufikia matarajio makubwa kwa miamba hiyo ya La Liga.

Kaka alitumia muda wake mwingi Santiago Bernabeu kwa kukaa benchi, lakini bado anasema aliridhishwa na muda aliokaa Madrid na kuitetea rekodi yake ya Hispania.
“Muda niliokaa Madrid sikushindwa,” Kaka aliwaambia Globo Esporte. “Nilicheza mechi 120, nilifunga mabao 28 na nilicheza michezo kwa wastani wa 30 kwa msimu”.
“Kipi zaidi, nilishinda makombe matatu: La Liga, Copa del Rey na Supercopa de Espana”.

Nyota huyo mwenye miaka 32 ambaye kwa sasa anacheza klabu yake mama ya Sao Paulo kwa mkopo, aliendelea kwa kumzungumzia kocha wake wa zamani wa Real Madrid, Jose Mourinho kuwa alimsaidia kuimarika.

“Mourinho alinisaidia kukua. Alinifundisha kuwa mvumilivu, kuendelea kupambana na kuheshimu maamuzi ya kocha. Alinisaidia kuimarika na kuwa mwanaume”.

“Nilijifunza kumheshimu kocha na kujitahidi kuonesha juhudi kadiri niwezavyo nikiamini kuwa ninaweza kuwa mmoja ya watu watakaocheza. Na ndivyo nilifanya katika miaka yangu mitatu chini ya Mourinho”.


Post a Comment

AddThis

 
Top