TIMU ya Coastal Union ya Tanga “Wagosi wa Kaya” leo inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na African Sports “Wanakimanumanu” kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani itakayokuwa ya kusheherekea sikukuu ya iddi Pili.
Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema maandalizi ya kuelekea mchezo huo yamekamilika kwa asilimia kubwa na kinachosubiriwa na mechi hiyo itakayoanza saa kumi jioni kwenye uwanja huo.
El Siagi amesema baada ya kumaliza mechi hiyo timu hiyo itaelekeza mipango yake ya kucheza mechi za kirafiki nyengine ili kuweza kujiweka imara kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Alisema wachezaji wa timu hiyo wataingia kwenye mechi hiyo kwa malengo ya kupata ushindi ili kuweza kuendeleza rekodi ya kuwafunga wanakumanumanu hao ambao msimu ujao watashiriki michuano ya ligi daraja la kwanza.
Kwa upande wake,Ofisa Habari wa timu ya African Sports,Wanakimanumanu” Said Karsandas alisema kuwa wamepania kushinda kwenye mechi hiyo ili kuweza kurudisha ile heshima ya timu hiyo kwa wagosi hao wa kaya.
“Tunajua mechi hii itakuwa ni ngumu kutokana na uwezo wa Coastal Union hivyo nasi tumejipanga kuweza kufanya vizuri ili kutoa burudani kabambe “Alisema Karsandas.
Hata hivyo aliwataka wakazi wa mkoa wa Tanga na viunga vyake kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani itakayokuwa ikitolewa kwenye mechi hiyo .
Post a Comment