0
Evance Aveva siku alipoenda kuchukua fomu ya kugombea Urais katika klabu ya Simba. ( picha na Global Publisher)


Tunapozungumzia juu ya kukua kwa klabu ya soka ambayo huundwa na binadamu kwa kujumuika pamoja ili kutekeleza malengo waliyojiwekea, tuna maanisha kuwa klabu hiyo kuwa na uwezo mkubwa zaidi siku hadi siku katika kufanya kazi yake vizuri zaidi.
Kubadilika katika mawazo na fikra zake kutoka kipindi hadi kipindi kingine kufuatana na mazingira ya wakati uliopo. Kwa hiyo basi, kukua kwa klabu ya Simba SC, kuna maana ya kuendeleza klabu kufikia hali ya kukomaa, katika kiuchumi na kimpira kwa uwezo mkubwa zaidi.
Tangu kuanzishwa kwa Simba, mwaka 1936, imepita miaka 78 sasa.
Kwanini nazungumzia juu ya kukua kwa klabu kama Simba? Moja ya sababu kubwa ni kufahamu klabu hiyo imetoka wapi, na inaelekea wapi, na wapi ilipo! Ni kweli, klabu hiyo imedumaa na kushindwa kuendana na wakati wa sasa? Kama imeshindwa, kwanini imeshindwa, na mbinu zipi zinaweza kukabili matatizo hayo?. Kuna mambo muhimu ya kuangalia hasa wakati huu, wanachama mbalimbali wakizidi kujitokeza kuchukua fomu za kugombea uongozi katika uchaguzi unaotaraji Kuanzia katika nafasi za juu za urais, na makamu wake wengi waliojitokeza ni sura zilezile zilizozoeleka kwa wapenzi wa soka. Kuna kipya chochote ambacho wanacho katika fikra za kuiongoza timu hiyo?.
Mmoja wa wagombea nimemsikia akijinadi kuwa anataka kuhitimisha miaka 78 ya Simba kutegemea watu binafsi, hali mbaya ya kiuchumi, wachezaji kumilikiwa na watu wenye fedha, kuipeleka mbele zaidi kiutawala katika misingi ya kiushindani.
Kama kuna ukweli katika maneno hayo ya Michael Wambura ambaye leo atarudisha fomu ya kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi wa Mei 29, huyu ni mtu sahihi. Simpigii ‘ debe’, wengi wanamfahamu, Wambura kuhusu mipango yake, kama aliweza kuacha kiasi cha millioni 80 katika akaunti ya timu hiyo kwa muda wa miezi sita, wakati akikaimu nafasi ya katibu mkuu wa Simba, 2005, ni wazi mtu huyu anajua namna ya kuingiza pesa. Ni msukumo upi ambao umewafanya wanachama wengine, Andrew Tupa na Evance Aveva kujitokeza kuwania nafasi muhimu na nyeti ya taasisi kubwa kama Simba?
Itakuwa ni vigumu sana kwa upande wa kiongozi kueleza juu ya kupinga unyonyaji kwa wanachama wao, wakati wao wenyewe ni wanyonyaji wanatoa nafasi kwa marafiki zao kumiliki mali na vyanzo muhimu vya mapato vya klabu hiyo.
Kiongozi makini ni Yule anayeishi katika fikra za wanachama wanavyotaka klabu kuwa. Nani asiyependa kuona, Simba ikipiga hatua kiuchumi na kiushindani?.Majuzi, nilimsikia, mwenyekiti wa zamani wati mu hiyo, Mzee, Hassan Dalali akisema kuwa alipanga kugombea nafasi ya urais, lakini kuna mtu amemfanya kuachana na mpango huo kwa kuwa yupo mtu sahihi. Nani huyo?. Ni, Aveva, mwenyekiti wa zamani wa kundi la ‘ Marafiki wa Simba! ‘.
Kuna watu wanatakiwa kuungwa mkono, ila Yule ambaye anakuwa na mtazamo wa kweli katika uongozi bora ndiye anayepaswa kupewa nafasi. Simba kama inataka kutoka katika hali waliyopo sasa ni lazima wakubali kuwa katika njia sahihi ya kuenda na na wakati. Mzee, Dalali alisema kuwa moja ya sababu kubwa zilizomfanya kumuunga mkono, Aveva ni kuwa tayari kufanya kazi na Wazee wa klabu ambao walitengwa sana katika kipindi cha utawala miaka minne iliyopita. Kivipi?.Hizi ni nyakati mpya, baraza la Wazee la klabu ni nafasi pekee ya wao kuonesha ni kiasi gani wanaguswa na maendeleo au matatizo ya Simba. Kikatiba, hata, Wambura atakuwa anatambua uwepo wao katika klabu, hivyo sababu nyingine za watu huwa hazina mashiko, na kitendo cha mgombea kutegemea kura za Wazee wa klabu kwa kuwa aliahidi uwepo wao wakati hata katiba inawakubali ni kukosa kujiamini, ama hoja na sababu za kumuunga mkono mgombea.
Michael Richard Wambura
 
Aveva, anaijua Simba, na bila shaka wanachama wa Simba watakuwa wanafahamu kuhusu uwezo wake wa kiutawala. Lakini, bado Simba haipaswi kutegemea nguvu ya ‘ Marafiki wa Simba’, kimawazo ni watu muhimu na wanachama ambao wana mchango mkubwa kwa klabu, Je, Aveva ataweza kuiendesha Simba bila nguvu ya kifedha kutoka kwa kundi la marafiki wa Simba?.Mwanamapinduzi yeyote anaweza kusimama imara wakati akipambana na mabepari, ni kazi sana.
Na, hata sababu ya uongozi unaomaliza muda wake ni kushindwa kuwa imara kwa aliyekuwa makamu mwenyekiti, Geofrey Nyange Kaburu ambaye ni mmoja wa wadau wakubwa wa kundi la marafiki wa Simba. Kama, Simba inataka kusimama yenyewe ni lazima kwanza apatikane mtu ambaye ataweza kujenga misingi imara ya klabu, kiuchumi na kimashindano na hilo ni kwa kuondoa utegemezi kutoka kwa kundi la marafiki wa Simba. Kwa miaka zaidi ya kumi sasa, Simba I nategemea kuwalipa mishahara na kuwasaini wachezaji kutokana na wanachama wanaounda kundi hilo, Simba inategemea nguvu yao kufanya vizuri, au vibaya.
Upande wangu nimependezwa na wagombea hawa wa nafasi ya urais, ila kama ‘ rais-mwanamapinduzi-kiongozi’, Simba inahitaji mtu mwenye sifa za Wambura, kabla wale wenye sera za ushindi pekee ndani ya uwanja. Unaweza kupata ushindi wa ligi kuu mara nne katika kipindi cha miaka minne ya uongozi, si kitu kipya. Ila, nani atahoji endapo timu itamaliza katika nafasi ya tatu au ya pili katika ligi kuu kwa kipindi cha miaka minne ijayo, wakati eneo la Bunju likikaribia au kuzidi ilivyo, Azam Complex Chamazi? Simba, inahitaji mtu muadilifu, mwanafunzi ambaye kamwe hatochoka kwenda huku na kule kujifunza, Simba inahitaji kuwa na rais-mbunifu katika mambo ya kiuchumi, mtu jasiri, asiye mlafi, mwenye hekima na busara, mwenye kutaka maendeleo yanayooneka, asiye na ahadi nyingi zaidi ya utekelezaji, Simba inahitaji mtu-msikivu na mwelevu wa mambo.
Wana- Simba wasiwe kwenye mapambano ya mamlaka, wawe kitu kimoja katika wakati huu wa kuchagua watu sahihi wenye uwezo wa kuvunja utegemezi ambao baadaye unakuwa ni sumu kali kwa mafanikio ya Simba kiujumla. Simba haijaangushwa na Aden Rage pekee, viongozi wengi waliopita walikuwa hivyo, bahati mbaya kwa Rage, yeye hakuwa mwanafunzi. Ila, kuna sumu ilisambazwa na kundi hilo la marafiki wa Simba ambayo ilimuathiri yeye na mipango yake. Kila, la heri, wagombea urais kataika uchaguzi ujao wa Simba. Mzee, Dalali anamuunga mkono, Aveva kwakuwa atawarudisha‘ Wazee wa klabu’, ila mimi ninaamini mtu sahihi yoyote mwenye kutaka kuitoa Simba katika utegemezi atafaa zaidi kwa kuwa, katiba ya Simba inatambua uwepo wa Wazee wa Klabu.

Post a Comment

AddThis

 
Top