0


Kwa muda wa miaka mingi soka letu limekuwa katika misukosuko ya mara kwa mara; jambo ambalo limepelekea maendeleo ya soka la nchi hii kurudi nyuma. Kutokana na kuyumbayumba kwa soka letu kumepelekea vilabu vyetu vinavyocheza ligi kuu kudorora na hata timu ya taifa imekuwa haifanyi vizuri hadi ikabatizwa jina la ‘kichwa cha mwenda wazimu’. 

Lakini mambo haya yote hakuna wa kumlaumu zaidi ya sisi kujilaumu wenyewe. Mambo haya yafuatayo yamechangia kwa kiwango kikubwa kuharibu soka letu:

a) Uelewa finyu au kutokuwa na elimu ya ukombozi.

Tukisema elimu ya ukombozi, tunamaanisha elimu ambayo mtu huipata na humsaidia kujitambua yeye mwenyewe. Elimu hii sio tu kwenda shule au kuhitimu na kuwa msomi au kupata kazi au cheo cha juu, bali ni elimu ambayo kiini chake huanzia akilini; na ni wachache wenye kukigundua. 

Elimu ya utambuzi humfanya mtu kujitambua yeye mwenyewe kwa kufundishwa na baadhi ya wanajamii wenye uwezo wa kuielewa elimu hiyo.

 Binadamu anapojitambua yeye ni nani, basi huwa na uwanja mpana wa kuweza kumudu mazingira yake na kugundua kila kitu kinachomhusu, zikiwemo sekta zote katika maisha yake; sekta ya michezo ikiwa ni moja wapo.

Binadamu asiye na elimu hii, hawezi kufanya jambo lolote likawa na mafanikio.

Ilivyo katika sekta zote katika nchi hii kuwa na ulegevu wa mafanikio; ndivyo pia ilivyo katka sekta ya michezo, soka likiwemo. 

Soka limeshindwa kuendelea si kwa sabubu wahusika wake nndio chanzo, la hasha! Bali, watanzania walio wengi hawana elimu ya ukombozi inayowafanya wajitambue, na watu hawa ndio wanaohusika katika michezo. Ukosefu wa elimu hii muhimu umechangia mambo yafuatayo:


i. Watu kutothamini timu zao za mikoani kwao au wilayani kwao, huo ni ukosefu wa elimu hii ya ukombozi. Mtu aliyekomboleka kimawazo,mwenye kujitambua hawezi kukimbilia cha jirani na kuacha cha kwao. Simba, Yanga, na Azam kwa sasa ni miongoni mwa timu zenye mashabiki wengi katika soka la nchi hii. 

Lakini mashabiki hawa sio wa Dar es salaam tu, wengi wao ni wa mikoani. Je, hizi timu za mikoani zitapewa heko na nani kama kwa mfano, kama Kagera Sugar inacheza na Ynga, unakuta mtu wa Kagera anapenda Yanga ishinde kuliko timu yake ya nyumbai? Kwa namna hii timu za mikoani zitatoa wapi nguvu za kiuchumi za kuweza kupambana na timu hizi kubwa katika soka? Huo ni ukosefu wa elimu.

ii. Mashabiki kuingia uwanjani wakati timu inapokuwa na matokeo mazuri tu. Timu nyingi zinazoitwa timu za wanachama, hupata heko ya mashabiki pale timu hizi zinapofanya vizuri, kama zinapwaya kidogo, mashabiki wanaanza kususia kwenda uwanjani. Baada ya Simba, Prisons, na timu nyingine, zilipoteleza mashabiki waligoma kwenda uwnjani. 

Tulimskia Hans Popu akihojiwa kuhusu sakata la wachezaji wa Simba kutpofanya vizuri kwa sababu ya kukosa posho. 

Hans Popu alijibu kuwa tatizo la wachezaji kutopata posho linatokana na mapato kidogo kwa kuwa mashabiki hawaingii uwanjani kwani timu haifanyi vizuri. Matahalani, msimu huu Mbeya City inasifiwa kwa mashabiki wake kuihunga mkono na kwa ushirikiano. 

Ni kweli, lakini itokee timu hii ifanye vibaya mfululizo uone kama mashabiki hao watapatikana tena. 

Zaidi watakuwa wanaponda na kuukolomea uongozi na kulaumu. Timu zetu zinakuwa za wananchi pale zinapofanya vizuri, zisipofanya vizuri si zetu ni za viongozi peke yao. 

Huu ni ujinga, ambao chanzo chake ni kuikosa elimu ya ukombozi hasa, ukombozi wa kiakili.

iii. Kutokana na kuikosa elimu mwongozo, ambayo ndiyo humpa mtu maarifa ongozi; madhara yake ni kwa watanzania kushindwa kuwa na ung’amuzi wa mambo muhimu kimaisha na kuyathamini. 

Hii ni dhana ambayo inapenye hadi kwa watanzazia wengi katika michezo. Asilimia iliyokubwa watanzania wengi hatuna mwamko wa kimichezo, tukidhani kuwa michezo haiwezi kutusaidia kulinganisha na mambo mengine.

Hii ni kwa sababu hakuna mchezaji yeyote ambaye amenufaika kwa kiwango cha juu kutokana na michezo hasa Tanzania. Jambo hili huwapelekea wazazi kutowaruhusu watoto wao kushiriki kwenye michezo wakiwa wadogo. Kitendo hiki kinaficha vipaji vya wachezaji wakiwa wadogo na kupunguza monkali ya kimichezo, na hivyo kujikita katika fani nyingine na si michezo, huku soka likiwemo. Wachezaji wengi sio tu katika soka, bali pia hata michezo mingine, huibuka ukubwani, jambo ambalo linafanya wachezaji wetu kutokuwa na uelewa wakutosha na ujuzi katika kumudu vipaji vyao.

iv. Kwa sababu watanzania wengi hawana elimu ya kung’amua mambo, wanachama wengi wenye uanachama wa vilabu vyetu hawajui kwa undani suala zima la soka. 

Wanachojua wao, ni kuona timu yao inashinda ila hawawezi kutafakari ni kwa njia, au ni kwa vipi timu yao inaweza kupata ushindi. 

Wanachojua wao, ni kutambiana na bali sio timu yao iwe na mipango ya muda mrefu itakayofanya kilabu kuwa na misingi imara na hatimaye kuleta ushindi. Wanachama hawa, wao huachia uongozi majukumu yote. 

Kwao mambo yote yenye kuhusu kilabu chao kuwa na mafanikio ni jukumu la kutimizwa na uongozi wao. 

Ni watu wa kutaka mambo mazuri pasi na kujua yanakujaje! Kazi yao ni moja tu, kuhoji pale timu yao inapovurunda, au kushinikiza uongozi uondoke madarakani pindi timu inapoteleza, au kazi yao ni kuhudhuria mikutano ya vilabu vyao na kupiga mayowe na wala si kuhusika kubuni mbinu na mipango ili timu ishinde.

v.Kwa kuwa uelewa ni mdogo, watu wengi wako tayari kuingia viwanjani bure bila hata kulipa kiingilio, wako tayari kutumia mali za timu zao, mfano, fulana, bukta, nembo n.k. 

pasi kugharimia mali hizo kwa lengo la maslai ya timu yao. Timu isipofanikiwa wanashinikiza uongozi. Ni kwa sababu ya ukosefu wa fikra mwongozo, wanachama wako radhi kuharibu miundo mbinu ya kimichezo kama viwanja na timu zao kuadhibiwa.

vi. Ni kwa kuwa wanachama wa vilabu vyetu wanauelewa mdogo wa mambo, wako tayari kuhukumu mazuri au upungufu wa vilabu vyao kupitia vyombo vya habari. 

Watu hawa hawawezi kupata habari za vilabu vyao moja kwa moja kutoka makao makuu, ila huishia kulalamika katika vyombo vya habari.
vii. 

Mpira wa siku hizi unahitaji nafasi ndogo ya vilabu kumilikiwa na wanachama, bali watu binafsi ambao wanawekeza hisa zao katika vilabu hivyo na kuwa katika mfumo wa makampuni. 

Azamu ni mfano bora katika soka la bongo. Ila kwa uelewa mdogo wanachama hao hulaumu uongozi kwa kutowezesha maendeleo ya vilabu hivyo hasa wanapolinganisha na Azamu, pasi kujua Azamu iko katika mfumo wa kisasa zaidi wa kiuendeshaji. 

Mamlaka yote yapo kwa mtu mmoja na haingiliwi na mtu yeyote. Lakini katika vilabu vyetu, kila mtu ana maamuzi na analotaka yeye analazimisha lifuatwe. Waswahili hunena, “wapishi wengi huharibu mchuzi”. 

Wanachama hao hao ukiwahoji kuwa vilabu vyao vibinafsishwe, watu wawekeze hisa, wanachama wanagoma na kucharuka, lakini mwishowe wanategemea mafanikio.

viii. Kutokana na wadau wa mchezo wa miguu kuwa mbumbumbu, huishia kuchagua viongozi mbumbumbu, alafu wanawanyooshea vidole. Kiongozi anayepatikana kwa njia ya demokrasia kila akifanyacho huaksi wale waliomchagua, kwani anakuwa anawakilisha wale waliomuweka madarakani.

 Kwa maana nyingine, kiongozi bora/mzuri hutoka katika jamii nzuri/bora. Na kiongozi mbabaishaji hutoka katika jamii ya wababaishaji. 

Kwa hiyo, kiongozi akiburunda madarakani anadhihirisha ujinga wa watu hao waliomuongoza. Wanachama wenye uelewa na wenye kujua mambo watamchambua kiongozi na hatimaye kumchagua kiongozi bora. 

Hawachagui kiongozi kwa kwa ushabiki na mvuto au kwa pesa/mali alizo nazo. Tazama yanayoendelea Simba. 

Wanachama wenye kuujua mpira, hawawezi kukubali uongozi au wao kuingilia maamuzi ya timu ya ufundi. Hawawezi kukubali wachezaji wasajiliwe kwa makundi ya baadhi ya watu wenye kutaka maslai yao binafsi, ati kisa watu hao wana nguvu ya pesa.

ix. Ni kwa kuwa ni ujinga na ukosefu wa elimu ya ukombozi, ndio maana wachezaji wanakurupushwa kuhama timu zao na kwenda timu nyingine, na kurubuniwa au kusainishwa mikataba mibovu bila kuisoma kwa umakini; kukurupuka kusaini mikataba kwa kuwa wamewekewa maburungutu ya pesa mezani. 

Huu ni ujinga wa kupitiliza, na inadhihirisha wazi kuwa wachezaji wetu na viongozi wetu wanaingia katika soka pasipo kutambua wanahitaji kufanya nini katika soka.

Kwa hiyo, mkururo wa ujinga, katika maisha huwa na matokeo hasi na wala si chanya. 

Na ndivyo ilivyo hata katika sekta ya michezo, huku soka nalo likikumbwa na adha hizi kwa kiasi kikubwa. Kinachohitajika sasa ni wanachama wa vilabu vyetu kutafuta elimu ya ukombozi ili waweze kuwa nguzo ya mafanikio.

b) Udikiteta wa mashabiki na wanachama katika vilabu vyao.

Wanachama na wadau wa soka wa nchi hii wamekuwa madikiteta kwenye soka, hasa pale ambapo wao wanaona mawazo na matakwa yao yanapaswa au yanastahili kufuatwa pasipo kufuata taratibu na kanuni za mpira wa miguu.

Makundi yafuatayo katika soka ni waathirika wa kubwa wa udikiteta katika suala zima la kuendesha soka letu:

i. Wanachama.

Hawa ni watu wenye kadi za uanachama, ambazo zinawatambulisha kama sehemu muhimu ya jumuiya ndani ya vilabu vya mpira wa miguu na michezo mingine. 

Ni watu muhimu sana katika maendeleo ya soka na pia ni muhimu sana katika kuharibu maendeleo ya vilabu. Wanachama wanazo haki zao za kimsingi katika vilabu vyao, na miongoni mwa haki hizo ni pamoja na kuhakikisha wanahimiza maendeleo katika vilabu, kupigania na kuitetea timu zao, kuchangia mawazo yenye kuhimarisha na kuleta maendeleo ya vilabu hivyo. 

Kushiriki shughuli zote za vilabu kwa njia nyingi ukiwemo mikutano ya vilabu vyao. 

Lakini, wanachama hawa wanazitumia haki zao kinyume kwa wakati mwingine; hasa pale kila jambo wanalolidai ni bora kutaka lifuatwe na litekelezwe na uongozi, jambo ambalo si sahihi katika maendeleo ya soka na kufanya hivyo ni kuharisha udikiteta na kutumia nguvu kwa kuwa ni haki yao kutoa maoni.

 Ila wajue kuwa si kila maoni lazima yafuatwe. Mfano, hivi majuzi tumesikia wanachama wa kilabu cha Costal Union, wakiulazimisha uongozi wao uwape kadi za uanachama ati kisa wanataka kushiriki uchaguzi. 

Swali la kujiuliza ni hivi, uanachama unakuwa wa maana pale wanapotaka kufnaya uchaguzi? Je hakuna umuhimu wa kuwa mwanachama bila uchaguzi kufika? Kwa mujibu uongozi, uliwataka wasubiri ili taratibu zikikamilika wapewe kadi lakini jambo la kushangaza, wanachama walianza kulaumu na kushinikiza uongozi uwape kadi jambo ambalo ni udikiteta. 

Timu inapofungwa wanachama na mashabiki hulazimisha viongozi wawajibike ikibidi wajiuzulu, ila wao wanachama hawawezi kuamua kuwa nao wawajibike. 

Huu ni udikiteta wa wanachama kwa viongozi wao. Wachezaji wakikosea kidoko labda timu ikafungwa, zinaundwa sababu na mizengwe, kwa wachezaji, kwa kuwashinikiza pengine waondoke, tumemsikia Kaseja, Yondani, Chuji na wengineo wakishutumiwa kwa kuuza mechi jambo ambalo ni udikiteta wa wanachama kutaka kulazimisha ushindi kwa timu zao hata pale watakaposhindwa ki mchezo.

ii. Viongozi.

Katika mpira au sehemu yoyote yenye kuunganisha watu kwa shughuli moja lazima pawepo na uongozi. 

Katika soka letu la bongo, hasa kwenye vilabu vyetu, viongozi wamekuwa madikiteta wa nafasi hizo, kwa kujipa madaraka, kwa kukiuka katiba za vyama vyao, kwa kutotaka kuwajibika ki haki au kisheria pale wanapoviweka matatizoni vilabu vyao. 

Imefikia hatua viongozi hawa wanawakolomea wanachama na mashabiki wao na hata kutumia nguvu za kimadaraka kuwafungia uanachama. Mfano mzuri, mambo haya yamefanyika sana katika vilabu vyetu vikongwe vya Simba na Yanga kwa misimu hii ya karibuni. 

Kwa upande mwingine viongozi hawa wamekuwa wakijikuta katika utumwa pale wanapolazimika kufanya kile ambacho wanachama wao wanataka hata kama si cha manufaa, lengo waendelee kulinda nafasi zao na kufurahisha mashabiki wao. 

Huu ni udikiteta wanaofanyiwa viongozi wa vialabu. 

Vilevile, uongozi wa vilabu vyetu umekuwa na tabia za udikiteta zaidi, hasa pale wachezaji, makocha na safu nzima ya ufundi inaposhindwa kulipwa maslai yao ipasavyo, na pale wanapoamua kudai, wanachukuliwa kama watovu wa nidhamu. 

Tumeshuhudia kesi nyingi, TFF ikiingilia kati ili wachezaji walipwe mafao yao kisheria hasa pale wanapokatishwa mikataba yao bila kushirikishwa. 

Uongozi wa vilabu vyetu, wahusika wamekuwa madikiteta zaidi kwa kung’ang’ania madaraka hadi kufikia hatua ya kupinduana; kuundiana tuhuma zisizo na misingi yoyote na kuchafuana, ili kusudi yule anayechukiwa na viongozi wenzie aondoke kwenye madaraka. 

Simba ni moja wapo ya kilabu ambacho kamati ya utendaji imejaribu kumpindua mwenyekiti. Hii ni hatari sana kwa maendeleo ya nchi hii.
iii. Wachezaji.

Wachezaji hawa ndio wasakata kabumbu uwanjani, na hawa tunaweza kusema ndio uti wa mgongo wa vilabu, bila wao sidhani kama kilabu kinaweza kuwepo au kuwa na wanachama. 

Wachezaji wao sio wafanya udikiteta, bali ni waathirika wakubwa wa udikiteta unaofanywa na wanachama wa vilabu vyao. 

Tumeona na kushuhudia, pengine hata kusikia baadhi ya wachezaji wanakatishwa mikataba yao au hata kufukuzwa katika timu kwa sababu ya shinikizo ama kutoka kwa wanachama, vingozi au mashabiki wa kawaida. 

Wamekuwa wakiyakosa mafao yao ya kimchezo kwa sababu ya udikiteta unaoendelea kufanywa kwenye vilabu vyetu hivi. 

Ama pengine wanalazimishwa kufanya baadhi ya mambo kinyume na maadili na matakwa yao; mfano, kupewa rushwa, au kulazimishwa kuuza mechi n.k.

Kwahiyo, uozo unaolikumba soka letu nchini, ni kwa kuwa wanachama wengi wanakurupukia kuingia katika fani ya soka pasipo kujua nini wanatakiwa kufanya. 

Utatuzi wa matatizo haya, ni jamii ya watanzania, kuhitaji baadhi ya watu wenye uelewa wa mambo ya kimaisha, na ambao wanajua umuhimu wa elimu ya ukombozi. 

Watu hawa wakatoe elimu hii mashuleni na hata kwenye jamii zetu hadi vijijini ili kusudi watoto wanaochipuka katika fani hii wawe na uelewa na utambuzi wa fani zao. 

Na watoto hawa wakijengewa moyo wa kupenda michezo na kujitambua, na kuthamini michezo kwa kuwa wana elimu ya utambuzi; basi sekta zote za kimaisha zitaweza kupata maendeleo. 

Soka nalo pia, litakuwa na watu wenye utambuzi wa hali ya juu, kuanzia mashabiki hadi wachezaji. Na hivyo mchezo huu hautakumbana na maluweluwe tunayoyaona sasa hivi.




Post a Comment

AddThis

 
Top