0
Tarehe 22/8/2014 nilipata nafasi ya kukutana na Christian Karembeu, na Fernando Saz kwa ukaribu zaidi, hawa ni wachezaji wa zamani wa klabu ya Real Madrid. Wakati wakifanya mahojiano na mwandishi wa Habari Shaffih Dauda nilikuwa najaribu kutafakari majibu waliyokuwa wanampa. Kama ungewasikiliza ungejua kabisa kuwa mpira wenye mafanikio ni mgumu katika uraisi wake.
Namaanisha ili kufanikiwa kimpira unatakiwa upambane na kufanya maamuzi stahiki ili uwafanye watu wengine wanaokuona uwanjani waone ni kitu rahisi. Kabla ya kuanza Interview na Shaffih, Karembeu aliomba apewe saa moja la mazoezi maana ulikuwa muda wa ratiba hiyo, wala hakujali sana, aliamini alihitaji zaidi mazoezi ya mwili kuliko Interview ile, katika nafasi ile nikajaribu kumvika uhusika mchezaji wa kitanzania, je angeweza kufanya hivyo? Jibu ni Hapana, angemsikiliza kwanza mwandishi anataka nini, na angeweza kuamini kuwa angefanya hata kesho yake.

Kwa muonekano wa karembeu katika khali nyepesi ni ngumu kuchukuliwa mpira na Jonas Mkude wa Simba, au Simon Msuva hata Sure boy. Pamoja na kustaafu anaonekana anaupenda na kuuthamini mpira. Anaheshimu uwanja wa mpira, anaheshimu ratiba ya mazoezi na mwisho anaelewa nini mpira unataka. 

Kwa akili yake angekuwa Ngasa Leo angekuwa anauliziwa na Al Ahly au angekuwa katua moja ya klabu nzuri ulaya. Watanzania tumeshindwa hapa, akili ya Karembeu bado inafanya kazi kuliko sisi, akiwa kastaafu Fernando Saz anauthamini mpira kuliko Boban wetu, akiwa kastaafu Figo anavitafuta viwanja vya mazoezi kuliko Ramadhani Singano.

 Baada ya hapa kwanini tusimlilie Emmanuel Okwi pamoja na ubabaishaji wake wa mikataba, kwanini kocha wetu wa taifa asihisi kuwa Pelembe ana ubora wa Ronaldinho akicheza na sisi.
Umepata kujua wachezaji wangapi chipukizi na walio juu tayari waliopata kuhudhuria mchezo wa Tanzania 11 na Malijendari wa Madrid? Yawezekana hakuna au ni wachache sana. 

Wao nao walienda kuhudhuria kama ambavyo ningeenda mimi hata mimi nimewazidi maana nilitafuta picha ya kumbukumbu na sahihi zao. Tanzania hatuna mwamko kuanzia kwa viongozi mpaka wachezaji. Tumeibadili siasa kuwa soka na soka kuwa siasa. 

Tunaamini ubovu wa kocha kuliko mipangilio ya soka letu kwa ujumla. Wako wapi wahitimu kutoka U17, U20, copa coca cola na uhai?? Tunacheza soka kwa sababu lipo ili lichezwe lakini sio kwa sababu ni washindani. Bahati mbaya wafanyabiashara wanasiasa wamelijua hili, nao wanakula hapa hapa kwa akili yetu hii. Hawaendelezi soka Bali wamefungua biashara simba na yanga kama ninavyoweza kutafuta duka la biashara posta. 

Figo tunaweza kuwa tumenufaika nae kitalii na sio kisoka. Nilikuwa namsoma kaka yangu Edo Kumwembe, aliamini kama Una pesa unaweza kodi,uwanja wa taifa kufanyia tafrija ya kumbukumbu ya kuzaliwa. Hakukosea, Tanzania tumefumba macho, hatuupendi mpira Bali tunaufurahia, viongozi hawauhitaji mpira kama wenyewe unavyowataka, ndio maana uongozi ni ubabaishaji. Wachezaji ni wababaishaji, na taratibu zetu za kibabaishaji. Mara nyingine yawezekana tunashiriki kwa sababu tunafuata sheria na kanuni za FIFA. 

Hakuna njia fupi katika soka, wenzetu wanawekeza katika vijana sisi tunalia Kazimoto akikosa visa Qatar. Nawaza akina Kigi na Wenzie w Serengeti boys wanawaza nini kichwani. Naamini ukiwauliza kwanini unacheza soka atasema nataka Maisha mazuri, wachache watasema natamani nikavae jezi namba 9 ya Barcelona kama Eto’o. Na ndio maana,ukimleta Wanyama uwanja wa Taifa wengi hawatolipa viingilio hata hawamuonei wivu. Kigi ana ndoto akifisha umri wa Januzaj awe anapokea Milioni 3 Simba basi.

Christopher Columbus moja ya watu walioizunguka sana dunia aliwahi kusema “You can never cross the ocean until you have the courage to lose sight of the shore” alimaanisha huwezi kuivuka bahari kama utokuwa na imani ya kupoteza uelekeo wa nchi kavu. Hapa ndipo watanzania tulipo, viongozi walipotuweka, tunaogopa Ulimwengu na wenzie bila wakongwe tutafungwa nyingi. 

Tunaifikiria zaidi Septemba 2014 na tunasahau June 2018. Nasikia Rais wetu wa TFF anatamani Tanzania iandae mashindano ya AFCON mwaka 2017, bahati mbaya alitweet kwa kingereza, angetweet kwa kiswahili angeshangiliwa zaidi kama,kiongozi bora. 

Tunajaribu kumlaza tembo miguu juu yaani chali. Acha tusubiri pengine Ndo imeonekana ndio namna ya kutupeleka AFCON. Tumekuwa wavuvi tunaofia kupotea ndani ya bahari. Ahsante Figo siku nyingine ukija nenda moja kwa moja mlima Kilimanjaro, huku tunafanya BIG RESULSTS NOW. Ahsanteni

Post a Comment

AddThis

 
Top