Beki wa kati wa Simba, Mganda Joseph Owino amesema tabia ya wachezaji wa Yanga kujiamini kupita kiasi iliyowaponza katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, itawagharimu tena katika mchezo wao wa 'Nani Mtani Jembe' utakaopigwa keshokutwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika mchezo uliopita uliomalizika kwa sare isiyotarajiwa ya mabao 3-3 kwenye Uwanja wa Taifa, Owino alifunga bao la pili la Simba na kuwanyamazisha 'Wanajangwani' hao ambao hawakuamini na kuomba mechi iishe mapema baada ya kushuhudia bao moja likirudi baada ya jingine. Owino, ambaye yuko Zanzibar na Kikosi cha Simba chini ya kocha mpya Mcroatia Zdravok Logarusic, wakiwa wameweka kambi ya siku tano kujianda kwa mchezo wa keshokutwa, alisema jana kuwa watatumia udhaifu ule ule wa wachezaji wa Yanga kukipa dozi kikosi hicho cha kocha Mholanzi Ernie Brandts. "Yanga wana tabia ya kujiamini kupita maelezo, walipotufunga 3-0 kipindi cha kwanza katika mchezo wetu uliopita walijiamini kwamba tayari walikuwa wameshashinda, tukatumia mwanya huo kurudisha mabao yote. Kwa sasa wanaamini kikosi chao ni bora kuliko chetu kwa sababu wana wachezaji nyota bila kuangalia sisi tunajipanga vipi," alisema Owino. "Naamini Simba itaifunga Yanga katika mchezo huo kwa sababu kikosi chetu kwa sasa kiko vizuri na kila mchezaji anahitaji kumwonyesha kocha mpya kwamba anaweza," aliongeza Owino. Katika mchezo huo uliovunja rekodi kwa mapato makubwa zaidi ya mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, wachezaji wa Wanajangwani walikwenda mapumzikoni wakiwa na nyuso za furaha huku kocha wao, Brandts akichukizwa na furaha hiyo iliyopelekea waimbe nyimbo za kupongezana kwenye vyumba vya kubadilisha nguo, lakini mabao yote yakarudi kipindi cha pili. Simba walikwenda Zanzibar Jumatatu kujiandaa kwa mchezo huo ulioandaliwa na wadhamini wa Simba na Yanga, Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager. Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, kikosi chao kiliingia kambini jijini Dar es Salaam jana jioni kujiandaa kwa mchezo huo. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo linasimamia mchezo huo, jana lilitangaza viingilio vya mchezo huo kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu, Boniface Wambura kuwa vya chini vitakuwa Sh. 5,000 na vya juu vitakuwa Sh. 40,000. | |||
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment