0


Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) limeandika barua kwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) likitaka ufafanuzi juu ya uhamisho wa mshambuliaji hatari Emmanuel Okwi aliyeuzwa kutoka SC Villa kwenda Yanga mwishoni mwa wiki.

Uongozi wa Yanga Jumapili ulithibitisha kumsajili kwa miaka miwili na nusu mshambuliaji huyo wa zamani wa watani wao wa jadi, Simba kwa dau kubwa linalotajwa kuwa dola za Marekani 150,000 (Sh. milioni 240 za Tanzania) huku huko nyuma Fifa ilimuidhinisha Okwi kujiunga kwa mkopo SC Villa ya Ligi Kuu ya Uganda akitokea Klabu ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia.

“Tumeiandikia barua FIFA kwa sababu tunahitaji watueleze kama uhamisho huo ni sahihi," amekaririwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fufa, Edgar Watson na mtandao wa MTNFootball.

Okwi, ambaye aliuzwa kwa mali kauli ya dola za Marekani 300,00 (Sh. milioni 480) na uongozi wa Simba kwa Klabu ya ESS mwaka jana, ameichezea SC Villa katika Ligi Kuu ya Uganda kwa kipindi cha takriban miezi miwili na kuifungia mabao matatu.

Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita Shirikisho la Soka Afrika (CAF) liliwataarifa Fufa kutowatumia Okwi na beki Godfrey Walusimbi (24), katika mashindano ya CHAN mwakani kwa sababu wawili hao hawana uhalali wa kukipiga katika mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji wa ndani kwa kuwa bado wana kesi ambazo hazijamalizika na timu zao za Etoile du Sahel na Don Bosco ya DR Congo.

Lakini, Mkurugenzi wa SC Villa, Edgar Agaba, aliuambia mtandao wa  MNTfootball kuwa Okwi (20), amejiunga na vinara wa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga akiwa mchezaji huru.

"Itakuwa jambo la kuvutia kuona Okwi, ambaye alizuiliwa kucheza CHAN akiwa na timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes), akiruhusiwa kujiunga na Klabu ya Tanzania (Yanga) huku akiripotiwa kuwa hajamalizana na klabu yake ya Etoile du Sahel,” alisema Watson.

"Itabidi tusubiri kuona tutakachoelezwa na Fifa, lakini sisi (Fufa) kama shirikisho, tutataka ushauri zaidi," alifafanua zaidi Watson. 

YANGA WANENA

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, alisema hawakukurupuka katika kumsajili mkali huyo wa kufumania nyavu za timu pinzani na ataitumikia timu yao katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Vodacom utakaoanza Januari 25, mwakani.

Bin Kleb alisema walimsajili Okwi siku sita kabla ya kupata Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) Jumapili, ndipo wakaamua kutangaza rasmi usajili huo.

Kuhusu utata wa sakata la straika huyo na Etoile ambalo limefika hadi Fifa, Bin Kleb alisema: “Tumefuatilia kote, hadi kwa wanasheria na tumefanikiwa kupata hadi ITC yake, nawaambia mashabiki wa Yanga wajue viongozi wao wanafanya kazi. Hatuna stori nyingi, sisi tunafanya vitendo na kazi zetu kwa umakini."

“Tumepitia sehemu zote, tumeona kabisa tuko sahihi katika kumsajili mchezaji huyo na hakutakuwa na tatizo lolote upande wetu,”alifafanua zaidi kiongozi huyo aliyefanikisha pia usajili wa nyota kadhaa wa Yanga akiwamo 'kiraka' Mbuyu Twite.

Etoile du Sahel ya Tunisia ilimnunua Okwi kutoka Simba Januari, mwaka huu, lakini baada ya miezi michache, mchezaji huyo akaamua kuachana na klabu hiyo na kurejea kupumzika kwao Uganda kwa madai hakulipwa mshahara wake kwa miezi mitatu.

Baada ya Okwi kukaa bila kucheza kwa miezi sita, Fufa ilimpigania aruhusiwe kurejea nyumbani kuichezea SC Villa ya huko ili kunusuru kiwango chake likiwa pia na matumaini ya kumtumia katika mashindano ya CHAN nchini Afrika Kusini mwakani akiwa na Kikosi cha The Cranes.
 

Post a Comment

AddThis

 
Top