0
Stori kuhusiana na watu wanaotengwa kwa kuhisiwa kuwa wana maambukizi ya Ebola bado zimeendelea kusikika kutoka sehemu mbali mbali duniani, ambapo kwa sasa mzazi mmoja ameifungulia mashtaka shule kutokana na shule hiyo kumzuia mtoto wake wa kike asihudhurie masomo shuleni hapo mpaka zitakapopita siku 21.

Baba wa mtoto huyo ameitaka mahakama kutoa amri kwa shule iliyopo Milford, Connecticut Marekani kumruhusu mtoto wake aendelee na masomo kwa kuwa hakuonesha dalili zozote za kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Shule hiyo haikutoa jibu lolote kuhusiana na maombi ya mzazi huyo, kitu kilichompelekea kufungua mashtaka katika mahakama ya wilaya ya Connecticut.

Mtoto huyo amekumbana na kadhia hiyo baada ya kusafiri kwenda na kurudi Lagos, Nigeria akiwa na baba yake kati ya tarehe 2 na 13 Oktoba, ndipo shule hiyo ilimzuia mwanafunzi huyo kuhudhuri masomo shuleni mpaka tarehe 3 mwezi Novemba na badala yake shule itakuwa ikimtumia mwalimu kwa ajili ya kumfundisha akiwa nyumbani kwao.

Tangu kulipuka kwa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi, kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kutengwa kwa watu wanaotokea Afrika Magharibi nchini Marekani ambapo chuo kimoja Texas kilisitisha kupokea maombi ya kujiunga na masomo kwa watu kutoka Nigeria kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Post a Comment

AddThis

 
Top