0
WALIPOFIKIA Alex Ferguson na Roy Keane sasa panatisha, maneno makali, ya kibabe hali inayoonyesha wakizidi, hata heshima walizonazo zitaporomoka.
Wanasoka wa Tanzania wanaweza hivi? Kuingia kwenye utamaduni wa vitabu na kueleza ukweli wa kila walichonacho?

Tunajua wenzetu Wazungu wanaweza hilo, lakini safari hii kwa mara ya kwanza, kitabu kinachohusiana na masuala ya soka kinazua malumbano makubwa kati ya magwiji wawili.
Ferguson aliyekuwa kocha wa Manchester United tokea mwaka 1986, ndiye mwenye mafanikio makubwa kuliko mwingine yoyote kama ilivyo kwa Keane ambaye ni nahodha mwenye mafanikio makubwa zaidi.
Wote wawili waliwahi kutoa vitabu, Ferguson alifikisha hadi vitano. Lakini baada ya kustaafu vizuri na kwa mafanikio makubwa, akatoa cha mwisho ambacho alieleza mambo mengi yakiwemo yanayowahusu baadhi ya wachezaji wake akiwemo Keane.

Katika kipengele cha Keane (kwa wiki nne sasa kimekuwa kikielezewa kwenye magazeti ya Championi Jumatano&Ijumaa), kinaeleza mengi likiwemo suala la nahodha huyo kutopenda mafanikio ya wachezaji vijana.
Ferguson ameeleza Keane alivyojisahau baada ya kumpa madaraka makubwa, akaeleza alivyoanza kumdharau msaidizi wake Carlos Quieroz raia wa Ureno, alivyomfokea Ronaldo, Ruud van Nisterlooy.
Lakini akaenda mbali zaidi kwa kueleza alivyowashambulia wachezaji wa Manchester United kwenye runinga ya klabu hiyo ya MUTV kwamba ni legelege, hali iliyosababishwa wazomewe wakiwa Ufaransa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika kitabu chake hicho amewagusa hadi van Nistelrooy na David Beckham, akieleza walibadilika mwishoni kama ilivyokuwa kwa Keane.

Inaonekana nahodha huyo wa zamani ndiye pekee ameshindwa kuvumilia, amejibu mapigo na katika uzinduzi wa kitabu chake juzi, mambo yalikuwa mabaya zaidi alipotoa maneno makali kwa Ferguson na sasa ndiyo gumzo kwenye mitandao ya England.
Keane amesema: “Nashangazwa sana na Ferguson kutoa kitabu na kuanza kuwashambulia watu waliomba mafanikio, angalia alivyoingiza mamilioni ya fedha.
“Hiyo haitoshi, Manchester wamempa jukwaa (kwenye Uwanja wa Old Trafford), wamempa na sanamu. Lakini bado anawadharau na kuwasema vibaya waliompa nafasi hiyo ya mafanikio.
“Kawaida alikuwa ni mtu anayependa kutukuzwa, kuogopwa na watu, lakini mimi sikuwa kati ya waliofanya hivyo, ndiyo maana nasema sikutaka kuandika kitabu, lazima niwe mkweli lakini nimeshindwa kuvumilia lundo la uongo wa Ferguson, ndiyo maana nimeamua kumjibu na kufafanua ukweli ni upi.”
Ukiambiwa Ferguson ni muongo unaweza kukubali? Ukisoma yale ya kwenye kitabu chake (kupitia gazeti la Championi), unaweza kuamini kocha huyo anaweza kudanganya?
Vitu vingi alivyovieleza kama lile la Keane kuwadharaulisha wachezaji wa Man United kwenye runinga au kumtukana van Nistelrooy wakiwa vyumbani, ni kweli anaweza kudanganya wakati kulikuwa na wachezaji na makocha wengine vyumbani? Maana Keane vyote ameeleza ni uzushi na kuvifafanua tofauti kwenye kitabu chake cha Second Half.
Majibu ya Keane kwa Ferguson yanaonyesha mambo mengi sana ambayo pia unaweza kuyarudisha kwenye soka ya hapa nyumbani.
Kwamba kunapokuwa na kundi kubwa la watu mfano wa timu, lazima ndani yake kunakuwa na mengi ambayo yamejificha lakini chuki huchukua nafasi kubwa sana.
Angalia ulivyokuwa unawaona Keane na Ferguson wakishirikiana kuisadia Man United kupata mafanikio makubwa, kumbe ndani yake kulikuwa na chuki kuu miongoni mwao na ndani kabisa ya mioyo yao.
Leo wanaweza kutoa mengi kama hayo, wanaonyesha kuwa kwenye soka, unafiki ni sehemu ya maisha, huenda hata hapa nyumbani imekuwa ikitafuna mafanikio ya klabu zetu, ingawa wamekuwa wakijitahidi kufanya kila kitu kiwe siri.
Kwani mara ngapi umesikia klabu zikikanusha habari za ndani ambazo hutolewa na watu wake wanapokuwa wamechoshwa na jambo fulani? Pia jiulize, bila unafiki, ugomvi, kuchukiana, mchezo wa soka hauwezi ukaenda.
Angaliea kwenye kitabu cha Zlatan Ibrahimovic ambaye sasa yuko PSG. Ndani yake anaeleza mengi kuhusiana na Pep Guardiola akisema hajawahi kuona mtu mwenye roho mbaya kama kocha huyo wa sasa wa Bayern Munich.
Wakati huo walifanya kazi wote Barcelona, yeye anamuita ni myama, shetani mwenye ngozi ya kondoo huku akisistiza alitaka kuua kipaji chake.
Soka ni mchezo mzuri, lakini unafiki ni nguzo yake? Kama Wazungu wanasifiwa kwa upendo au kuwa wakweli au kutokuwa na roho za kwanini. Vipi hapa nyumbani, ndani ya timu zetu kukoje? Hebu watu nao wafunguke tujifunze, acheni uoga!

Post a Comment

AddThis

 
Top