Tatizo si rais wa TFF, Ndugu, Jamal Malinzi kudai makato ya asilimia tano kutoka kwa wadhamini wa klabu za ligi kuu . Muundo wenyewe wa Bodi la ligi hauko sawa. Wakati wa kuundwa kwa chombo huru, aliyekuwa rais wa TFF, Leodgard Tenga alitengeneza kamati maalumu, nazungumzia kamati ya kina W. Karia, Mzee Said, ambayo ilikuwa kamati maalumu ya kufanya mchakato wa uundwaji wa chombo hicho huru. Lakini kilichokuja kutokea sasa ni watu hao ambao walishiriki kuunda chombo hicho kurudi .
Wakati wa uundwaji, Tenga hakufanya chombo hicho kuwa huru ndiyo maana kuna mikataba mingi ambayo imesainiwa na TFF, jambo ambalo lisingefanyika endapo bodi hiyo ingekuwa huru kisheria. TFF wanatakiwa kuwa wasimamizi wa sheria tu na kuhakikisha kanuni hazivunjwi. Bodi ya ligi inapaswa kujitegemea, na TFF wanatakiwa kuwa wasimamizi tu ili kuweko na maadili katika mpira.
Tatizo limeanzia mbali, wala halijaletwa na Malinzi, muundo wenyewe wa bodi una mapungufu mengi.
Kwanza Bodi iliundwa kama Kamati nyingine ndogo ndogo za TFF, mfano; kamati ya nidhamu, kamati ya mashindano au kamati ya soka la vijana. Hivyo ndivyo ilivyo kwa mujibu wa katiba ya Shirikisho la Soka nchini, TFF. Kwa hiyo basi Kamati ya utendaji ya TFF ina mamlaka kisheria kuiagiza Bodi kutokana na muundo ulivyo kisheria tofauti na wanavyofikiria baadhi ya watu.
Kama, Bodi ya ligi ingekuwa huru, kamati ya utendaji ya TFF isingekuwa na mamlaka ya kuwaingilia na kuwaagiza. Hatupaswi kumtafuta ‘mchawi’ katika hili, kilicho muhimu ni kutafuta njia sahihi ya kuunda upya muundo wenyewe wa Bodi. Kuna mambo ya muhimu sana ambayo Bodi inatakiwa kuyatazama na si hilo la ‘asilimia tano za Malinzi’. Mwaka mmoja uliopita, Yanga walikuja na hoja yenye mashiko kuhusu mgawanyo wa mapato ya AzamTv. Yanga hawakuwa tayari kuona wakipata mapato sawa na klabu nyingine, ilikuwa hoja yenye ukweli ndani yake. Inakuwaje, Yanga na Simba wapate sawa na timu nyingine wakati mechi zao nyingi ndo zinaonyeshwa ‘LIVE’ kwenye Televisheni.
Bodi ya ligi ilipaswa kulishughulikia swala la YANGA na kulimaliza lakini wamelipotezea tu kwa ajili ya maslahi yao. Bahati mbaya ni kwamba, mambo yote haya yanatokea wakati huu huku watu walewale walioshiriki mchakato wa uundwaji wakiwa viongozi. Awali hawakuona ‘mantiki’ ya Yanga na kufikiri klabu hiyo ilikuwa na malengo ya kuwakwamisha katika mambo yao. Bado hawajachelewa sana, Bodi inaweza kukaa na kujitathimini kisha kufanyia kazi mapungufu waliyokuwa nayo wao wenyewe ndani ambayo ni makubwa kuliko hilo la kudaiwa asilimia tano na Malinzi.
Kutokana na mapungufu yaliyopo ndani ya Bodi hiyo, TFF imetumia ‘mwanya’ kutaka kuchukua fedha. Bodi ya ligi ni lazima itumie muda huu kuunda mazingira ambayo yatawafanya wawe huru na wasiingiliwe na TFF. Tusitazame ‘asilimia tano’, bali tutengeneze mazingira bora endelevu ambayo yatawafanya kuwa huru. Awali bodi hiyo iliundwa ‘kisiasa’ na uongozi uliomaliza muda wake kabla ya kuingia kwa Malinzi. TFF ya Malinzi imeikuta Bodi hiyo tayari imeundwa na kufanya kazi yake.
Kama ungekuwa uongozi wa Tenga umeagiza makato hayo ya asilimia tano yafanyike, je Bodi ya ligi ingekataa?. Wasingekuwa na uwezo wa kupinga jambo hilo kwa sababu waliwekwa kwa kuwa Bodi hiyo iliundwa ili watu Fulani ‘wapate kula’ ndiyo maana ilitengenezwa kwa muundo huo. Ila kinachotokea sasa baada ya kuingia madarakani kwa Malinzi, inaonekana ni tatizo kwao kwa maana ya kuingiliwa katika mipango yao waliyotumia muda mrefu kuisuka na kuiweka sawa.
Malinzi anafanya yote hayo kwa kuwa uongozi uliopita tayari ulikuwa umeandaa mazingira hayo, na kama Bodi ya ligi ingekuwa ikifanya kazi na baadhi ya viongozi waliokuwepo katika utawala uliopita wasingelalamikia makato hayo lakini wamekuwa wakilalamika jambo hilo kufanywa na uongozi wa sasa. Nia si kuisema vibaya Bodi ya ligi, wala lengo si kumtetea Malinzi, kama utakwenda katika uhalisia wa tukio lililotokea na njia ya kulitatua ni bora Bodi hiyo ikajitazama upya na kuweka misingi ya uhuru wa muda mrefu kwa maendeleo ya mpira wa Tanzania.
Post a Comment