MANCHESTER United ilikamilisha usajili mkubwa katika dakika za mwisho za dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka huu kwa kuinasa saini ya mshambuliaji hatari, raia wa Colombia, Radamel Falcao.
Falcao amelijenga jina lake na kuwa moja ya washambuliaji wazuri na hatari zaidi barani ulaya kwa miaka mitano iliyopita na mpaka hivi sasa.
Huyu ni mshambuliaji aliyefunga mabao 41 katika mechi 52 za ligi alizoichezea FC Porto na alifunga mabao 52 katika mechi 68 alizokipiga Atletico Madrid.
Akiwa AS Monaco ya Ufaransa katika msimu wake wa kwanza alishindwa kuonesha makali yake kutokana na majeruhi, lakini bado alifunga mabao 11 katika mechi 20 alizocheza.
Hakuna mtu mwenye wasiwasi juu ya ubora wake licha ya kusumbuliwa na majeruhi. Ni mshambuliaji hatari na anajua kuzitafuta nyavu.
LAKINI MANCHESTER UNITED WALIMHITAJI FALCAO WAKATI WANA ROBIN VAN PERISIE NA WAYNE ROONEY?
Ndiyo. Ni mchezaji mzuri. Kiwango cha Robin van Persie hakijawa kizuri tangu alipoanza kucheza msimu wake wa kwanza akiwa United. Wayne Rooney hajawa na muendelezo mzuri wa kufunga mabao. Amefunga mabao 20 tu kwa misimu miwili tangu alipojiunga na Man United mwaka 2004. Misimu mingine amekuwa akipanda na kushuka. Sio mashine ya magoli kama alivyo Falcao.
Falcao ana uwiano mzuri wa mabao kwa kila dakika kuliko Rooney na van Persie. Ni mshambuliaji wa aina yake. United imefunga mabao mawili katika mechi zake tatu za mwanzo wa msimu huu na kwa mazingira hayo wanahitaji mfungaji mzuri zaidi. Falcao amesajiliwa kwa ajili ya kumaliza ukame huo.
Matokeo ya usajili huu inawezekana ukamfanya Falcao aanze na Rooney na kumuacha benchi RvP.
Kama sio hivyo tunaweza kumuona Wayne Rooney akicheza namba 10 katika mfumo wa 3-4-1-2, nyuma ya Falcao na RvP ambapo itakuwa safu kali ya ushambuliaji.
Au uwezekano wa mwisho ni kwamba Rooney anaweza kurudishwa nyuma kama kiungo wa kati sambamba na Darren Fletcher.
Hii itamruhusu Juan Mata kucheza nyuma ya washambuliaji. Mfumo huu utakuwa wa hatari zaidi, lakini uwiano wa kikosi utakosekana. United hawaja huru kufunga mabao mengi kwasababu mfumo ndio umekuwa tatizo.
Walicheza mipira mirefu dhidi ya Burnley na kiujumla walikosa mawazo sahihi ya kufunga. Wakiwa na Falcao watakuwa na kitu cha ziada, lakini sio tiba ya matatizo yao mengine.
Wanahitaji kutengeneza nafasi nyingi na kuwa na ushirikiano mzuri katika timu. Uhusiano kutoka safu ya ulinzi na ushambuliaji unahitaji kuboreshwa. Falcao hataweza kufunga peke yake, hata kama atapata nafasi nyingi.
Kiukweli ni usajili mzuri, lakini United inahitaji kufanya vitu vingi na kuboresha maeneo mengine ya timu.
Post a Comment