0
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho inashuka dimbani kucheza mechi ya marudiano dhidi ya wenyeji Msumbiji katika uwanja wa Taifa wa Zimpeto, nje kidogo ya jiji la Maputo, kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali ya mataifa ya Afrika mwakaini nchini Morocco.
 
Taifa Stars itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam wiki mbili zilizopita.
Katika mchezo wa kesho, Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote ile au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele hatua ya makundi.

Kocha mkuu wa Stars, Mholanzi, Mart Nooij alisema vijana wake wapo fiti kwa ajili ya mechi ya kesho na wanaweza kuiondoa timu yake ya zamani ya Msumbiji.
Kabla ya kutua Maputo jana, Taifa stars ilipitia Johannesburg nchini Afrika kusini ilipoweka kambi ya siku mbili. Kambi hiyo imeelezwa kuwa ya mafanikio kwani imewajengea imani kubwa wachezaji wa Stars.
Mbwana Samatta (anayemiliki mpira kushoto) amejiunga na Taifa Stars mjini Maputo asubuhi ya leo
Wakati huo huo washambuliaji wawili wa kimataifa walioshindwa kujiunga na timu nchini Afrika kusini, wanaokipiga Tp Mazembe ya DR Congo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wamewasilia asubuhi ya leo mjini Maputo tayari kwa mechi ya kesho.
Wanandinga hao walilakiwa na mwenyekiti wa kamati ya ufundi ya shirikisho la soka Tanzania, TFF, Wilfred Kidau.
Samatta na Ulimwengu walionekana kuwa na furaha ya kujiunga na Taifa Stars wakitokea mjini Lubumbashi ambapo timu yao inajiandaa na mechi ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
 Katika mchezo wa kwanza jijini Dar es salaam, Stars ilicheza vizuri lakini kulikuwa na makosa kadhaa idara zote.
Safu ya ushambuliaji iliyojumuisha washambuliaji wanne, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, John Bocco na Mrisho Ngassa alishindwa kufunga mpaka alipoingia Khamis Mcha `Vialli` kipindi cha pili na kufunga mabao mawili.

Thomas Ulimwengu (kulia) amewasili leo asubuhi mjini Maput
Bocco, Ulimwengu na Samatta kwa nyakati tofauti walipoteza nafasi muhimu za kufunga kwenye mechi hiyo. Bila shaka mwalimu aliliona hilo na atawatumia vizuri washambuliaji wake.
Makosa binafsi ya Kevin Yondan na Nadir Haroub `Cannavaro` yalisababisha Stars kufungwa mabao mawili, ingawa pia lawama zinaweza kuwaangukia Erasto Nyoni na Mwinyi Kazimoto waliojisahau kutekeleza majukumu yao ya kuimarisha ulinzi kuanza safu ya kiungo.
Benchi la ufundi litakuwa limefanyia kazi makosa yote na kesho litaingia na mipango ya kushinda ili kusonga mbele.
Wachezaji wa Stars watakiwa kupigana kwasababu mazingira si rafiki kwao. Wapo ugenini, watakabiliana na Msumbiji iliyopo uwanja wake, mashabiki wake, hivyo itakuwa na nguvu zaidi ya Dar es salaam.
Lakini kama vijana watakuwa makini, wanaweza kufanya kazi nzuri na kuibuka na ushindi au kutoa sare na hatimaye kusonga mbele.
Mabeki watatakiwa kumlinda kiungo mshambuliaji wa Msumbiji, Elias Gasper Pelembe. Huyu ni mchezaji hatari sana na Msumbiji imejijenga mabegani mwake.
Ni mjanja sana, anaweza kupiga chenga na anatumia vizuri nafasi za kufunga. An uzoefu wa 10  kuichezea Msumbiji, hivyo walinzi wa Stars watatakiwa kumkaba vizuri kwasababu anaweza kuamua matokeo peke yake.
Kila la kheri Taifa stars. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa stars.
 

 

Post a Comment

AddThis

 
Top