Kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia, Zdravko Logarusic hana mzaha kwenye suala la nidhamu
MCHANA wa leo katika harakati zangu za kutaka kujua nini kimetokea ulimwengu wa soka barani ulaya, nimekutana na habari ya kocha wa FC Barcelona, Luis Enrique.
Kocha huyu alirithi mikoba ya kocha Tata Martino aliyeacha kazi baada ya kumaliza msimu uliopita bila kikombe.
Enrique amepewa jukumu la kurudisha ufalme wa Barcelona katika michuano ya La Liga, UEFA na ligi ya mabingwa wa dunia ya FIFA uliopotea baada ya kuondoka kwa Pep Guardiola na kufariki kwa Tito Vilanova.
Kocha huyu amenivutia jinsi alivyokuja na mipango mipya ya kuirudisha Barca katika hadhi yake. Moja ya maeneo aliyoyaangalia zaidi ni nidhamu ya mpira na mazoezi kwa wachezaji.
Moja ya tatizo lililomtafuna Tata wakati anaifundisha Barcelona ni kuwapatia uhuru mkubwa wachezaji tofauti na kipindi cha Guardiola.
Guardiola alikuwa na sheria zake binafsi na wachezaji walipigwa faini pale walipozivunja. Lakini alipoondoka zilikufa na Tata akazichinjilia mbali kabisa.
Enrique amefufua tena mfumo wa sheria kwa wachezaji na kurudisha ladha ya Guardiola Barcelona.
Miongoni mwa sheria za Enrique ni kwamba mchezaji anatakiwa kufika mazoezini saa moja kabla ya programu kuanza.
Pia wachezaji hawatakiwa kuchelewa wakati wa chakula cha klabu. Zaidi ni marufuku kunywa pombe wakati wa Chakula kambini.
Enrique pia amewabana wazee wa bata ambapo amesema kwamba siku mbili kabla ya mechi, wachezaji wote wanatakiwa kuwa nyumbani kabla ya saa sita usiku. Mambo ya kukesha kwenye kumbi za starehe ni marufuku.
Hata mitandao ya kijamii kama vile Twita, facebook na Instagram, Enrique amesema lazima wachezaji waitumie kwa njia chanya.
Mambo magumu: Enrique (kulia) ameanzisha sheria ili kurudia umwamba wa Barcelona na kutwaa makombe msimu ujao
Enrique anasema kama mchezaji atavunja sheria hizi atatozwa faini kuanzia Euro 1,000 na 6,000. Na akifanya makosa makubwa zaidi anaweza kufukuzwa klabuni.
Kwa haraka haraka unagundua kuwa kwenye kundi la wachezaji wengi wa kimataifa kuna tabia tofauti tofauti. Wapo wanaojielewa kwa asilimia 100 na hawahitaji kusimamiwa.
Watukutu wapo kama kawaida. Kocha hawezi kusema lazima wachezaji wafike saa moja kabla ya mazoezi kama hawakuwepo wachezaji wanaochelewa.
Wapo wazee wa kuzima moto. Kuchelewa ni sehemu yao na ndio maana kocha anakuja na sheria hii.
Hata wachezaji wa kimataifa wana matatizo yao inapofika wakati wa nidhamu. Wengine kwa jeuri kubwa ya pesa wanakesha kwenye kumbi za starehe, na ndio maana kocha ameweka sheria ya kuwazuia kufanya hivyo wakati wa mechi muhimu.
Mpira una miiko yake. Nidhamu ya mazoezi ni muhimu kwa mchezaji. Kwa kocha Enrique, pengine sheria hizi zinaweza kumsaidia.
Kuna vitu vingi vya kuangaliwa ili kuibadili Barca. Suala la mfumo wao wa `Tiki-Taka’ kuboreshwa halikwepeki. Dunia imegundua namna ya kucheza na Barca, hivyo Enrique anatakiwa kuja na mipango mipya ndani ya mfumo wao huo.
Sio rahisi kuua ‘Tiki-taka’ kwa Barcelona, lakini maboresho ya mfumo huu yanahitaji ili kurudi katika kilele chao cha mafanikio.
Wakati nasoma sheria za Enrique, ikanikumbusha wakati ule kocha wa Simba sc, Mcroatia, Dzravko Logarusic alipotua msimbazi.
Loga ni miongoni mwa makocha wa aina ya Enrique. Anafahamu wazi umuhimu wa nidhamu ya mazoezi kwa wachezaji na nidhamu ya mpira uwanjani.
Nakumbuka alileta sheria Msimbazi na wachezaji wakaona kama anawazingua vile. Alisema wachezaji lazima wafike nusu saa kabla ya mazoezi kuanza na wakifika lazima wawe wanachezea mpira na sio kukaa kupiga domo.
Pia alisema wachezaji watakaoshuka kiwango watakwa mshahara na wale watakaoonesha utovu wa nidhamu kwenye mazoezi watakatwa mshahara. Wachezaji wa kibongo waliona ni utaratibu mgumu na wengine kuanza kumuundia zengwe.
Lakini makocha aina ya Loga wanahitajika sana ili kuweka sawa nidhamu. Lazima ufuate miiko ya soka. Umeona hata Enrique kaja na sheria zake licha ya kufundisha klabu kubwa yenye wachezaji wakubwa.
Pia Maximo ni kocha mzuri inapofika suala la nidhamu. Ni kocha mwenye msimamo. Kwa aina ya wachezaji wa Tanzania wasiokuwa waumini wazuri wa nidhamu, wanaopenda kujirusha, anasa, ni muhimu kuwa na makocha wenye mitazamio kama ya Enrique.
Makocha wa ligi kuu kujifunza sio dhambi, kama kuna uwezekano wa kuwabana wachezaji kama anavyofanya kocha wa Barcelona kwa sasa, inaweza kuwajenga wachezaji katika misingi ya nidhamu nzuri.
Post a Comment