0


MABAO 2-0 waliyopata Nigeria dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 20,Ngorongoro Heroes jioni hii uwanja wa taifa katika Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana yamempa kazi ngumu kocha mkuu John Simkoko kusonga mbele.

Ngorongora walipata nafasi kadhaa za kufunga kipindi cha kwanza, lakini bado ugonjwa wa kutotumia nafasi muhimu unazidi kuitafuna timu hii.
Mshambuliaji Saady Kipanga alishindwa kuonesha makeke yake baada ya kupoteza nafasi kadhaa za kufunga.

Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika milango ya timu zote ilikuwa migumu, huku kipa namba moja wa Heroes, Aishi Manula akiumia.
Kipindi cha pili, Manula alishindwa kurejea uwanjani na kumpisha kipa namba mbili, Peter Manyika.

Katika Kipindi hicho cha pili Ngorongoro waliingia kizembe na kujikuta wakifungwa mabao mawili na kumaliza mechi kwa kipigo cha nyumbani cha mabao mawili kwa sifuri.

Peter Manyika alifungwa bao la kwanza dakika ya 48 na Yahya Musa, aliyemalizia krosi ya Muhamed Musa.

Wakati Ngorongoro wakihaha kusawazisha bao hilo, Nigeria walifanya shambulizi la kushitukiza na kufanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Awoinyi Taiwo baada ya kutumia vizuri makosa ya beki Pato Ngonyani aliyezembea kuondosha mpira kwenye eneo la hatari. 

Kilichoonekana kwa Ngorongoro Heroes ni kukosa umakini na kushindwa kujiamini kila wanaposhika mpira.
Nigeria waliwazidi vijana wa Tanzania kwa vitu vingi, lakini kikubwa zaidi ni kucheza kwa kujiamini na kumiliki mpira kwa wakati wote.
Kwa dakika zote 90, Nigeria walikuwa wanajitahidi kumiliki mpira na kuwahangaisha vijana wa Tanzania.
Walilindi vizuri lango lao, walikaa na mpira na kupiga pasi nzuri, na kushambulia kwa kutumia akili nyingi, hivyo kuonekana kama wapo nyumbani kwao Lagos.
Hawakuwa na papara wanapofika langoni kama ilivyokuwa kwa vijana wa Heroes.
Nigeria hawakupata nafasi nyingi katika mchezo wa leo, lakini kila walipokuwa wanafikia lango la Ngorongoro walikuwa hatari zaidi.

Mabao ya Nigeria yamefungwa kutokana na mabeki wa Ngorongoro kufanya uzembe wa kuziba njia za kupita wapinzania wao.

Kuna wakati mabeki wa Ngorongoro walikuwa wanashindwa kufanya maamuzi ya kuondosha mpira ya hatari, hasa bao la pili ambapo Ngonyani alishindwa kuondosha mpira katika eneo la hatari.
Sehemu ya ushambuliaji ya Heroes imekuwa butu na kuwanyima watanzania ushindi leo hii.
Katika michezo miwili dhidi ya Kenya, kocha mkuu wa Heroes, John Simkoko alikiri kuwa safu ya ushambulaiji ilikuwa butu, hivyo kuahidi kufanya marekebishao.

Lakini leo bado safu hiyo imeonekana kukosa umakini na kushindwa kuandika mabao kwa nafasi muhimu walizopata.

Kelvin Friday alifanya kazi nzuri na kupiga mipira mingi katika eneo la hatari la Nigeria, lakini washambulaiji wa kati Juma Luizio na Saady Kipanga walishindwa kutumia vyema nafasi hizo.

Ngorongoro kwa muda mwingi walipooza na hawakucheza kwa kasi, hivyo kuwapa nafasi wageni kutulia na kucheza watakavyo.

Nigeria wameonekana kuwa bora kwasababu waliwazidi Heroes kwa kila kitu, japokuwa ukiangalia maumbo ya wachezaji yanafanana na vijana wa Tanzania.

Kwa matokeo hayo, Simkoko anahitaji kufunga mabao 3-0 nchini Nigeria mei 23 mwaka huu katika mchezo wa marudiano au kushindwa 2-0 ili mshindi apatikane kwa mikwaju ya penati.

Simkoko ana kazi ngumu ya kufanya marekebisho ya makosa ya kikosi chake kwasababu kiwango cha Nigeria cha leo kinadhihirisha ugumu wa mechi ijayo.

Hata hivyo kitu kibaya zaidi leo hii ni wapenzi wachache kujitokeza kuwashangilia Ngorongoro Heroes.

Vijana waliomba kupewa sapoti na mashabiki, lakini watanzania wamewaangusha kwa kushindwa kufika kwa wingi.

Mechi yenyewe imepigwa siku ya wikiendi, lakini watu wamesita kufika uwanjani. Uzalendo bado ni tatizo kwa soka la Tanzania hasa timu za taifa.

Post a Comment

AddThis

 
Top