0
Kikosi cha Simba SC kimewasili salama Visiwani Zanzibar kilipokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza kesho.
Wakati Azam FC, Simba SC na Yanga SC zikiongoza makundi matatu ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, Simba itakuwa na mtihani mgumu itakapoikabili Mtibwa Sugar FC katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C itakayochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar leo Alhamisi kuanzia saa 2:14 usiku.

Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola amethibitisha kuwasili salama kwa kikosi chake visiwani humo kikiwa na nyota 18 kikiwakosa wachezaji watano wa kikosi cha kwanza.
Nyota hao ni pamoja na kipa Ivo Mapunda aliyekwenda Mbeya kuhudhuria arobaini ya baba yake, Waganda Emmanuel Okwi, Juuko Murushid, Simon Sserunkuma na Joseph Owino ambao walirejea kwao baada ya mechi waliyolala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar Desemba 26.

Kikiwa na nyota 18, kikosi cha Simba kimetua salama kwenye Bandari ya Zanzibar leo saa majira ya saa 8:18 alasiri huku daktari wa timu hiyo, Yasin Gembe akiweka wazi kwamba hakuna mchezaji aliyekuwa mgonjwa au majeruhi kati ya wachezaji hao waliotua visiwani humo.

Msemaji wa Simba, Humphrey Nyasio, amesema kuwa kikosi chao kimekwenda Zanzibar kikiwa na nyota mmoja tu wa kigeni, Mganda Dan Sserunkuma huku akidai kuwa nyota wao wengine wanne kutoka Uganda mabaeki Owino na Murushid pamoja na viungo washambuliaji, Simon na Okwi watatua Dar es Salaam kesho asubuhi na kuunganisha kwenda Zanzibar.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amesema kuwa kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinayahamishia makali yake ya VPL katika Kombe la Mapinduzi.
“Tuko kwenye basi kwa sasa tunatoka Manungu kuelekea Bandarini tayari kwa safari yetu ya Zanzibar,” amesema nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.

Mechi ya Simba dhidi ya Mtibwa itatanguliwa na mechi mbili za mapema baina ya JKU na Mafunzo (Kundi C) saa 9:00 alasiri na Polisi dhidi ya Shaba FC (Kundi A) itakayochezwa kuanzia saa 11:00 jioni.

Azam FC wataanza kampeni ya kusaka ubingwa keshokuwa watakapowavaa mabingwa watetezi KCCA FC ya Uganda katika mechi ya visasi ya Kundi B itakayochezwa kuanzia saa 2:00 usiku. Mechi hiyo itatanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo kati ya mabingwa wa Zanzibar, KMKM na Mtende Rangers saa 10 jioni.

Mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, Yanga wataanza kurusha karata yao keshokutwa kwa kuchuana na SC Villa ya Uganda katika mechi ya Kundi A itakayochezwa kuanzia saa 2:00 usiku ikitanguliwa na mechi ya Kundi C ya Mtibwa Sugar dhidi ya JKU saa 10 jioni.

Fainali ya michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya tisa yangu ianzishwe kuenzi Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, itachezwa kwenye Uwanja wa Amaan Januari 13 kuanzia saa 2:00 usiku.

MAKUNDI MAPINDUZI
KUNDI A:  Yanga, Taifa ya Jang’ombe, Polisi na Shaba FC
KUNDI B: Azam, KCCA, KMKM na Mtende
KUNDI C: Simba, Mtibwa, JKU na Mafunzo.

Post a Comment

AddThis

 
Top