MTANDAO huu umefanya mahojiano maalumu na Nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Taifa Stars na sasa kocha wa Mtibwa, Mecky Mexime kuhusu chimbuko la ukocha wake na falsafa anayopenda.
Pia ameeleza mambo mbalimbali ya mpira, leo tuanza sehemu ya kwanza ya mahojiano haya:
Mwandishi: Chimbuko au historia yako ya kuingia katika kazi ya ukocha ni nini?
Mexime: Kitu cha kwanza, mimi nimecheza mpira muda mredu, nilikuwa nahodha, ujue kuwa nahodha nako kunasaidia, unakuwa kama kiongozi.
Mpaka alipokuja Marcio Maximo akanichagua kuwa nahodha wake. Alituweka wengi wengi, akawa anachunguza, lakini akaona mimi naweza kuwa nahodha wake.
Tukafanya naye kazi mwaka wa kwanza, lakini siku moja Maximo baada ya kufanya naye kazi kwa mwaka mmoja akaniambie wewe ni kiongozi mzuri, ukimaliza mpira somea ukocha. Utakuja kuwa kocha mzuri.
Ujue alikuwa kama rafiki yangu, kama anataka mchezaji wa kimataifa ilikuwa ananiomba ushauri, hata kama anataka kuongeza mchezaji mwingine nilikuwa namshauri kwamba kuna mchezaji mmoja mimemuona. Nilikuwa namwambia mimi nimewaona wazuri sijui kama wewe utawaona wazuri, katika wachezaji wote niliowaona kila akiwaita na kufanya nao mazoezi, jioni ananiita na kusema kweli wewe unawajua wachezaji
Mwandishi: Wachezaji gani ambao ulimshauri Maximo awachukue na wakafanya maajabu?
Mexime: Wapo wengi ambao walikuwa hawapewi nafasi, mfano Ngassa (Mrisho), Boban (Haruna Moshi) walikuwa hawapewi nafasi timu ya taifa, watu walikuwa wanapiga kelele, Maximo alikuwa ananiuliza namwambia wale ni wachezaji wazuri. Sio hao tu, wapo wengi ambao walikuwa wadogo na mimi ndiye niliwapokea timu ya taifa. Yeye alikuja akakuta tupo wakongwe watupu, uliona alivyoingiza maingizo mapya.
Mimi haikuwa wachezaji wa Mtibwa tu, kama nimemuona Simba, Yanga, sijui timu gani ana uwezo namwambia kuna mtu tukijaribu kumuita anaweza kutusaidia
Mwandishi: Baada ya Maximo kukupa wazo la kusomea ukocha ulilipokeaje?
Kwanza nilikuwa nimeshapanga kustaafu, wakati nacheza ikatokea kozi Morogoro, baada ya mapumziko nikaenda kusomea, aliposikia akaniambia umeenda kusomea, basi vizuri. Akasema endelea na tulipokuja kutolewa na Msumbiji nikastaafu, akasema sijapenda, lakini sina jinsi, naheshimu uamuzi wako, endelea na ukocha.
Mwandishi: Ulikuwa na malengo gani ya muda mrefu baada ya kuingia kwenye ukocha?
Mexime: Mimi kwanza nilikuwa najifunza, unajua wakati nacheza kulikuwa na makocha wengi, ujue falsafa yangu ipo tofauti na makocha wengine, kipindi nacheza tulikuwa tunatumia nguvu sana, mbio nyingi, lakini mimi nimecheza miaka ya karibuni ninajua wachezaji uishi nao vipi.
Wachezaji huwa hawapendi mbio kwenye mpira, lakini mbio ni lazima. Ujue kuna mazoezi mengi sana ya mpira, lakini unatakiwa uyajue, ukimkimbiza mchezaji huku anachezea mpira anafurahi na kucheka. Zoezi lile linaingia kuliko umwambie kimbia raundi 10 au 20, mimi nadhani falsafa yangu hapo ndipo ipo tofauti.
Kipindi cha kabla ya msimu mbio zipo, lakini kwenye ligi tena ukipiga mbio, haifai, ujue watu wengi wanaamini sana hivyo, mimi falsafa yangu haiko hivyo, naamini mchezaji nimuumize na mpira, nimuumiza na mechi ndogo,ndio maana unaona kwenye timu yangu wachezaji huwa wanacheza mpira
Mwandishi: Fafanua falsafa yako au unaamini mpira wa aina gani?
Mimi naamini mpira ambao timu lazima icheze, sisi tunacheza mpira, mpira kama hela, kila mtu duniani anaishi anatafuta hela, kwahiyo ukitaka kuwa na maisha mazuri inabidi hela uitafute wewe, ukishaipata hela inabidi uitawale ili uweze kuishi maisha mazuri.
Kuipata hela sio kazi, kazi uitawale vipi? Sasa ndio mpira, wapo watu 22, kila mtu anautaka mpira, ndio mfano wa hela, inadibi wachezaji wote tuutafute ule, tunapoutafuta mchezaji wetu kaupata tutautawala vipi, sasa hapo ndipo inakuja hali ya kumiliki mpira. Hii ina mazoezi yake na mnafanya ile kazi ya kumiliki mpira, kwenye mechi mkiwa na mpira ni rahisi kufunga, mkiwa na mpira sio rahisi kufungwa. Hata Barcelona wakati wa Pep Guardiola iliwashinda wengi kwasababu ya kumiliki mpira, wakipoteza wanapambana haraka kuurudisha kwao, mkiwa na mpira ni rahisi kuwafunga watu, kwasababu ni ngumu kuutafuta mpira.
Post a Comment