0
Mgombea nafasi hiyo mwaka 2010, Profesa Ibrahim Lipumba.
Na Mwandishi Wetu
HUKU joto la uchaguzi mkuu wa urais mwakani likiwa nyuzi mia moja tayari, uchunguzi umeonesha mgombea nafasi hiyo mwaka 2010, Profesa Ibrahim Lipumba kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf) nafasi hiyo haimtaki tena.

Baadhi ya wapenda mambo ya siasa waliozungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii walitoa maoni yao wakisema wanaunga mkono muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuamua kumsimamisha mgombea mmoja mwakani.

Hata hivyo, walisema kwa maoni yao, hata kama hayatapita, Lipumba hafai kusimama katika nafasi hiyo na kugombea tena katika kipindi cha kuingia mwaka wa ishirini na tano.

“Lipumba angepumzika, awaachie wengine. Aligombea mara ya kwanza mwaka 1995 na Mkapa (Benjamini) wa Chama cha Mapinduzi. Akagombea naye tena mwaka 2000 na Mkapa huyohuyo.

“Mwaka 2005 akagombea na Kikwete (Jakaya) wa CCM, mwaka 2010 akagombea naye tena. Kama Cuf watamsimamisha mwakani ina maana atakuwa anagombea urais kwa mara ya tano akiwa anaenda mwaka wa ishirini na tano, si sawasawa,” alisema mdau mmoja.

Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa, kuna watoto walizaliwa wakati Lipumba anaanza kugombea urais mwaka 1995 na mwakani vijana hao watakuwa na sifa ya kupiga kura kuchagua rais. Lo!
Kumbukumbu zinaonesha kuwa, mwaka 1995, Lipumba alipata kura za urais 418, 973 sawa na asilimia 6.43. Mwaka 2000 alipata kura 1,329,077 sawa na asilimia 16.26.

Mwaka 2005 alipata kura 1, 327,125 sawa na asilimia 11.68 na mwaka 2010 alipata kura 695,667 ambapo ni sawa na asilimia 8.06.

Post a Comment

AddThis

 
Top