VIJANA 29 wameitwa kwenye kikosi cha maboresho cha Taifa Stars ambacho kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni kuwajenga kiuwezo na vipaji vyao vijana waliopatikana walipoita Taifa Stars Maboresho kwa mara ya kwanza!
Kama unakumbuka, TFF iliwahi kuteua kikosi cha Taifa Stars Maboresho, wakaweka kambi kule Tukuyu, Mbeya baada ya timu ya wakufunzi mbalimbali waliopita mikoani kuwateua.
Baada ya kuteuliwa kwa vijana wale, wakaingia kambini zaidi ya mwezi. Baada ya hapo wakapewa mechi ya kimataifa ambalo lilikuwa kosa kubwa, Taifa Stars ikatandikwa mabao 3-0 na Burundi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lilikuwa kosa kubwa kwa kuwa haikuwa sahihi kuwapa nafasi vijana waliotoka timu za mitani, Ligi Daraja la Tatu, Ligi Daraja la Pili na kwanza kucheza na timu ya taifa ya Burundi.
Kikosi hicho kilianza na rundo la vijana hao wa maboresho, baada ya kufungwa, mabadiliko yalifanyika haraka na kuanza kuingiza baadhi ya wakongwe na wale walio kwenye timu za ligi kuu ili kuepusha aibu zaidi.
Kocha Mart Nooij alikuwa jukwaani, ndiyo alikuwa amewasili kwa ajili ya kuanza kuinoa Taifa Stars. Alishuhudia kila kitu na baada ya kuanza kazi, aliwatimua vijana wote wa maboresho.
Safari hii, TFF imeita tena timu hiyo ya maboresho itakayoingia kambini Desemba 9, mwaka huu jijini Dar na taarifa kutoka TFF ilisema hivi:
“Lengo hasa la programu hiyo ni kuwajengea uwezo vijana wenye vipaji ambao walipatikana katika awamu ya kwanza ya mpango wa maboresho mwanzoni mwa mwaka huu Tukuyu mkoani Mbeya, lakini wamekuwa hawatumiki.”
Vijana walioitwa ni hawa hapa na timu zao kwenye mabano.
Aishi Manula (Azam), Benedict Tinoco (Kagera Sugar), Aboubakar Ally (Coastal Union), Miraji Adam (Simba), Andrew Vincent (Mtibwa Sugar), Gadiel Mbaga (Azam), Emmanuel Semwanda (African Lyon) na Joram Mgeveke (Simba).
Edward Charles (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Kassim Simbaulanga (African Lyon), Pato Ngonyani (Yanga), Adam Salamba (Kahama), Hassan Banda (Simba), Mohamed Hussein (Simba), Hashim Magoma (Stand United), Makarani Ally (Mtibwa Sugar), Said Juma (Yanga) na Said Hamis (Simba).
Aboubakary Ally Mohamed (Zanzibar), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Malombe (Geita Gold), Muzamir Ally (Mtibwa Sugar), Shiza Ramadhan (Mtibwa Sugar), Omari Nyenje (Ndanda SC), Kelvin Friday (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Alfred Masumbakenda (Kahama) na Simon Msuva (Yanga).
Unaweza usione tatizo haraka, lakini kuna mambo mawili ambayo tunaweza kujifunza. Kwanza ni kujikanganya kwa taarifa kutoka TFF, kwamba vijana walioitwa ni wale waliotokana na maboresho na wamekuwa hawatumiki.
Lakini si wote walioitwa hapo wametokea maboresho wala si kweli akina Simon Msuva, Edward Charles na Hassan Dilunga hawapati nafasi ya kucheza Yanga.
Pili, kuitwa kwa vijana waliokuzwa na klabu, basi lingekuwa jambo jema TFF kuanza maandalizi ya timu za taifa za vijana kwa kuwa walikuwa wakitafuta fedha. Kwa nini leo hii wasiitwe timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ikaanza kuandaliwa mapema?
Hakuna haja ya kuendelea kuwaudhi wadhamini wenu Kampuni ya TBL ambao hawakufurahishwa. Nafasi hii ingepewa timu ya vijana chini ya miaka 17 ambayo baada ya miaka miwili, ndiyo itakuwa na nyota tegemeo wa taifa.
Uko wapi muda wa kung’ang’ania kuwakuza vijana wasiokuwa na nafasi ya kucheza kwenye klabu zao. Badala yake ilitakiwa kuwaendeleza wale wanaocheza kwenye klabu zao.
Katika kikosi hicho, kuna vijana kama akina Dilunga na Msuva, hilo ni jambo jema na wangeungana na vijana chini ya miaka 17 ambao wangekuwa na msaada sahihi kuliko maboresho ambao hata kwenye timu bado hawachezi.
Post a Comment