0
KESHO ndiyo ile siku, imesubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, wengi walianza kuisubiri mara tu baada ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kutangaza ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu mpya.

Imekuwa ni kawaida, kila inapotangazwa ratiba mpya ya Ligi Kuu Bara, wengi huangalia mechi mbili kali zitachezwa lini, hakuna ubishi ni Yanga dhidi ya Simba na Simba dhidi ya Yanga.
 
Mechi hizo ni kubwa, hakuna anayeweza kubisha na kwa kuwa pamoja na kasoro luluki ambazo tumekuwa tukipata kwa klabu hizo kongwe, lakini si rahisi kukataa kwamba zinakubalika na ndiyo kina baba wa soka nchini.
 
Mashabiki wengi wa soka nchini ambao kwa asilimia 95 wanaziunga mkono timu hizo mbili wamekuwa wakitamani zikutane ili kupata burudani ya watani wa jadi ambayo huanzia siku kadhaa kabla ya mechi, uwanjani kabla ya mchezo, mchezo wenyewe na baada ya kwisha.
 
Kuna mambo mengi sana ambayo ni nadra kuyaona kwenye mechi nyingine zaidi ya hiyo inayowakutanisha watani kutoka Manispaa ya Ilala, lakini wanasimamisha shughuli za nchi nzima, watu wakitaka kuwaona wanapambana.
 
Kinachofurahisha ni kwamba, pamoja na mashabiki hao kutaka kuziona zikicheza, hakuna yeyote kutoka upande wowote ambaye anaweza kuwa tayari kuona timu yake inapoteza mchezo kwa kuwa anaamini anashabikia kikosi bora zaidi.
 
Utamu ni kwamba  moja ya mechi ngumu kutabirika ni hiyo ya watani, hivyo mashabiki huenda na uhakika uwanjani wakiamini watashinda kutokana na namna wanavyoziamini timu zao, lakini mpira hauna matokeo ya asilimia mia kabla haujachezwa.
 
Wanaokwenda uwanjani wakijiamini watashinda, wamekuwa wakichukizwa sana pale wanapopoteza, hali hiyo imesababisha tafrani ya kila aina katika vikosi vya timu hizo iwe Yanga au Simba, hali ambayo imekuwa ikizua hadi uadui.
 
Kawaida katika soka, lakini kuwe na makosa ili mmoja apoteze. Lazima kuwe na uzembe, ili upande mmoja ufunge bao. Ndiyo kawaida ya mpira kuwa ni mchezo wa makosa, kawaida hilo lazima litokee ili timu ifunge.
 
Kama mabeki, kipa au mmoja wa wachezaji wa Yanga au Simba hatakosea, basi bao halitapatikana. Hiyo ni asili ya mchezo wenyewe. Lakini jambo hilo linaonekana kutokukubalika hata chembe kutokea kila upande na kama itatokea, basi tafsiri inakuwa tofauti.
 
Tafsiri kuu ya hilo ni hujuma, anayeshindwa kufunga, au anayezembea au kufanya kosa ndiye anakuwa mchawi, ndiye anakuwa adui wa mashabiki ikiwezekana kwa msimu mzima. Wanachofanya ni kumuangushia machungu yao yote kwa muda wote huku akionekana ni kama adui.
 
Hakuna ubishi, wachezaji wa Yanga walifanya makosa katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, wakalala kwa mabao 2-0. Pamoja na kushinda dhidi ya JKT Ruvu na Prisons, bado walifanya makosa pia, wangeweza kushinda mabao mengi zaidi.
 
Halikadhalika Simba, pia nao walifanya makosa katika mechi zao zote tatu, upande wa ulinzi na hata washambuliaji. Sare tatu hazikuwa saizi yao kwa kuwa walionyesha kuwa na kikosi bora na kinachofanya vizuri. Lakini hakuna shabiki anayehoji makosa hayo kwa nguvu hadi kusababisha uadui.
 
Kupoteza dhidi ya Yanga au Simba kwa watani hao ni kidonda, kweli inauma na hakuna anayetaka kupoteza. Lakini hakuna ujanja, kama timu hizo ni za soka, haziwezi kuukimbia mzizi mkuu wa mchezo huo kuwa kuna kushinda, sare au kupoteza.
 
Itakapofikia mwisho, kuna kila sababu ya mashabiki kukubali kuwa wamepoteza, wawape moyo wanajeshi wao ili wafunge safari upya kwa kuwa ndiyo timu itakuwa imecheza mechi ya nne tu, ziko nyingine 22 za ligi kuu mbele yao. Kuanza kutafuta mchawi ni kujivuruga baadaye.

Utamaduni wa kutafuta mchawi umekuwa kawaida, wakati mwingine umewakumba hadi baadhi ya viongozi. Wakati umefika wa kuamini hata mechi ya watani ni sawa na nyingi za ligi linapofikia suala la uwanjani. Tubadilike, kesho si mbali.

Post a Comment

AddThis

 
Top