0

Kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya sherehe ya miaka minne ya Kandanda ‘facebook group’ napenda kuchukua fursa hii kuwatangazia rasmi udhamini wa vifaa kutoka Kampuni Bin Slum Tyres Limited.

Udhamini ambao leo hii tunaupokea kutoka kampuni hii,chini ya Mkurugenzi wake Nassor Bin Slum, utahusisha pia jezi zitakazovaliwa na timu shiriki siku hiyo ya Oktoba 25,mwaka huu.

Kutokana na umuhimu wa siku hiyo na mapenzi makubwa aliyonayo Bin Slum katika soka,ameamua ashirikiane nasi bega kwa bega kupitia kampuni yake kwa kuanza kutupa ufadhili huu.
Naomba niwaeleze kwa kifupi Wanahabari nia ya kuandaa sherehe hii ya miaka minne ya Kandanda ‘Facebook Group’.


Kwa kifupi,Kandanda ‘facebook group’ iliasisiwa miaka mine (07:23 23/10/2014) iliyopita,huku ikiwa na lengo kuu la kuwakutanisha wadau wa mpira wa miguu (kandanda) kwa pamoja ndani na nje ya nchi kupitia mtandao wa ‘Facebook’


Ndani ya Kandanda,wadau wa soka kwa muda wote wamekuwa watulivu na wakibadilishana mawazo,juu ya soka la ndani na lile la nje, kwa kujenga hoja zenye upembuzi yakinifu…bila kusahau utani wa hapa na pale.

Niwe mkweli tu,kwa muda wote huo wa miaka minne,’group’ hii imejikusanyia wadau wengi ndani nan je ya mipaka ya Tanzania,kutokana na jinsi inavyoendeshwa tofauti na ‘magroup’ mengine.
Tumekuwa tofauti sana,katika majadiliano na ufikishwaji wa habari,ndio maana leo hii mnamuona Bin Slum akitupa udhamini huu pia.

Lakini,kama tungekuwa tunatumia muda wa miaka hiyo kutukanana na kutojadili vitu vya kujenga,leo nani angekuwa tayari kutoa udhamini wake! Tungempata wapi Bin Slum?
Tunapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Bin Slum pamoja na kampuni yake,kwa kuungana nasi katika kufanikisha tukio hili adhimu.

Pia,katika kuelekea katika siku yetu hiyo tunatarajia kuwa na mchezo wa soka utakaozikutanisha timu #TeamDizomoja na #TeamIsmail, timu ambazo usajili wake wa wachezaji unaendelea hadi Oktoba 11.
Kwanini #TeamDizomoja na #TeamIsmail? kamati ilikuna vichwa juu ya timu hizo mbili zipewe jina gani kwamuda mrefu, lakini ilikuwa ngumu kupata jina ambalo litakuwa halijaegemea upande fulani miongoni mwa timu pendwa. (Katika kandanda timu yako tunaita Kabila).

Ninavyosema,hivyo nimaana kuwa katika familia yetu,tuna wanachama ambao wanatimu mbalimbali ambazo wanazishangilia,kwahiyo ili kuleta uwiano, tuliamua kutumia majina ya watu wanaochangia sana katika hiyo ‘group’ yetu.

Mshindi wa mchezo huo,atakabidhiwa kombe pamoja na kupewa fursa ya kukata keki ya kusheherekea miaka minne ya Kandanda.
Baada ya hapo wadau wote watakaoshiriki siku hiyo watapata fursa ya kujadili kwa pamoja mustakbali wa soka letu na nini kifanyike kwa siku za usoni, na nafasi yetu itakuwa ipi katika kandanda la Tanzania kama mashabiki.

Kwa hiyo,napenda kuwatangazia rasmi wadau wote wa soka,kuwa sherehe zetu za kusheherekea miaka minne ya Kandanda zinatarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu katika viwanja vya TCC Chang’ombe,Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Admin wa KandandaFB Group (KFBG)
Patoo

Post a Comment

AddThis

 
Top