Mwanadamu kawaida kaumbwa na ubongo unaomfanya kwa kiasi kikubwa kuwa tofauti na wanyama wengine.
Kwa mwanadamu kugundua kipi kinafuata ni rahisi kutokana na kusoma yaliyopita. Nilikuwa namsoma ndugu yangu Ally Mayay akisema Taifa Stars inafunga magoli magumu lakini inafungwa magoli rahisi sana.Uliona goli la kusawazisha la Mozambique? Lingeweza kukupa Jibu rahisi sana, lingeweza kukuonyesha tofauti Yao na yetu.
Lingeweza pia kukusaidia kutabiri nini kilikuwa kinakuja mbele yetu, kuyageuza matokeo ya Tanzania ilikuwa ngumu sana, labda kama Nsajigwa angekuwa bado anacheza Timu ya taifa, naamanisha wachezaji wanaocheza kwa ajili ya timu, wachezaji wanaotoa asilimia 200 ya nguvu Yao kwa ajili ya timu.
Ndio tunafungwa magoli rahisi wakati tunafunga magumu, tunatunza Vito ndani halafu tunalala mlango wazi kwanini usiibiwe. Ukijaribu kurejesha mshale wa saa nyuma kwa takribani miaka 7 utaona tofauti iliyokuwepo Kati ya Tanzania na Ethiopia, Tanzania na Cape Verde. Lakini Leo wao ni jabali sie tofali, hawajiulizi Mara mbili namna ya kutufunga.
Wakati nchi nyingine zikifanya mabadiliko katika mfumo mzima wa soka, Tanzania hatujaweza Hilo, wakati nchi zingine zikiwaandaa vijana kisoka watanzania hatutaki Hilo, tunaona ni dhambi kubwa ukimuacha Kiemba ukamtumia Singano, dunia imehama huko, ulimwengu unazunguka sasa, Tatizo linalowatafuna Uruguay na Italy pia linatutafuna sisi, tofauti Yao na yetu ni ubora wa wachezaji na soka Lao lakini ugonjwa wetu unafanana.
Uliwaona wote walivyokutana na Costa Rica, ungejua umri ulivyo na Tatizo. Wao wanaweza kuokoka hapa, wana mifumo stahiki ya kuwaleta watoto juu.
Wakati Colombia ikitengenezwa kupitia kijana James Rodriguez, wakati Brazil ukiwa kupitia Neymar, wakati Ujerumani ikianza kuwatumikisha vijana katika timu sisi hatujawaza Hilo, tunasubiri Ulimwengu afikishe miaka 26 Ndo tumpunguzie Ngasa muda uwanjani. Muda haupo na sisi.
Bahati mbaya ya akili zetu Ndo ipo hapa, baada ya kushindwa kwa mbinu zote utaona tunarudi katika zama za kutumia vijana, hiyo itakuwa mwaka 2016 mwaka mmoja kabla ya kombe la dunia. Kwanini usione Elias Pelembe ni ngumu kukabika, kwanini usione Pelembe ni mzuri maradufu kuliko sisi. Akili yetu imesimama hapa, akili mchawi wetu ni sisi wenyewe.
Kwa wale waliofanikiwa kuishi na babu zao ama kufuatilia mila nyingi wanaijua Laana. Babu yangu mzee Agwanda aliwahi kunieleza Kuna aina mbili ya laana, ile ya kukusudia na ile ya kutokukusudia.
Usipokusudia unatamka maneno kwa kuchukizwa ama kughafirika ambayo baadae umuathiri yule uliyemtamkia.
Unamfahamu Bela Guttman, huyu alikwaruzana na uongozi wa Benfica miaka zaidi ya hamsini iliopita, aliwaahidi hawatochuukua ubingwa wa ulaya kwa miaka 100, mpaka sasa imekatika zaidi ya miaka 50, huku Benfica ikicheza fainali nane UEFA bila kuibuka na ushindi, ishaanza kuaminika kuwa laana imewakamata.
Huyu Guttman alikusudia kulaani. Umewahi kuisikia kauli ya Tanzania kwenye michezo ni sawa ni kichwa cha mwendawazimu kila asiyejua kunyoa atajifunzia hapo.
Binafsi nimekua nikiisikia, niliambiwa alitamka mheshimiwa Rais wa awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi. Huyu alitoa hisia zake lakini pengine alitulaani bila kujua, alitoa laana ambayo imefumba mipango yetu yote, alitupa laana inayotufanya tuamini hatuwezi kuwazalisha akina Elias Pelembe 3 katika timu ya taifa.
Mwaka 1990 wakati wa fainali UEFA Kati ya Benfica na Milan, Eusebio aliamua kwenda kuomba msamaha katika kaburi la Guttman, aliamini alikuwa rafiki mkubwa wa Guttman na msamaha wangepata, lakini haikuwa hivyo.
Nilifundishwa laana ukiigundua ni vyema ikafanyika mipango ya haraka. Mojawapo ya mipango hiyo ni kuandaa tafrija Kisha unachinja mnyama aliyenona kwa ajili ya kufuta laana.
Nahisi basi yatupasa kufanya hivyo, Nahisi tunatakiwa kumchinjia mheshimiwa Mwinyi mnyama. Kama inawezekana ifanyike mipango haraka. Pengine laana Ndo inazuia kuwapata akina Yaya Toure, pengine laana ndio inachangia mipango yetu isiyoeleweka.
Ahsanteni.
Ahsanteni.
Post a Comment