Thomas Ulimwengu ataungana na timu nchini Afrika kusini
TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha mkuu, Mholanzi Mart Nooij imeondoka jioni ya leo kwa ndege ya Air Tanzania kuelekea nchini Afrika kusini itakapoweka kambi ya siku mbili kabla ya kwenda mjini Maputo kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Msumbiji.
Taifa Stars iliwasili leo asubuhi kwa ndege ya Fastjet kutoka kambini mjini Tukuyu, mkoani Mbeya na kuunganisha safari ya Afrika kusini jioni.
Mechi hiyo ya marudiano itapigwa agosti 3 mwaka huu uwanja wa Taifa wa Zimpeto uliopo nje kidogo ya jiji la Maputo.
Katika mchezo wa kwanza, Taifa Stars ilitoka sare ya mabao 2-2 na ‘Black Mambas’ ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam Julai 20 mwaka huu.
Taifa Stars wanahitaji ushindi wa aina yoyote au sare ya mabao 3-3 au zaidi ili kusonga mbele hatua ya makundi ya kuwania kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika, AFCON mwakani nchini Morocco.
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaocheza TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu watajiunga na wenzao nchini Afrika kusini leo wakitokea Mjini Lubumbashi nchini DR. Congo.
Wakati Mwinyi Kazimoto anayecheza soka la kulipwa nchini Qatar tayari alitua nchini na leo hii ameondoka na timu.
Post a Comment