0


MWENYETI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, amewataka wanachama wa chama hicho wamuulize Mbunge Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe wapi alikomtoa hadi kufikia ngazi na hadhi aliyonayo sasa katika medani ya siasa nchini.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara, lililoandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chaso) kwa kushirikiana na Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA)
Katika kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Land Mark, Mbowe ambaye alianza kwa kutaja historia yake kama mwasisi kijana wa CHADEMA na mwenyekiti wa kwanza, alisema mwaka 2003 akiwa katika harakati za kukijenga chama, alipita katika vyuo mbalimbali ili kupata vijana wasomi wajiunge na CHADEMA na ndipo alipompata Zitto, akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Nikiwa katika harakati zangu za kukijenga chama, nilipita Chuo Kikuu cha Dar es Salaam …nilibahatika kuwapata kina John Mrema, Halima Mdee, Zitto Kabwe, John Mnyika wakiwa viongozi ambao walipenda siasa ya mabadiliko, nami nikaondoka nao bila ya kusita,” alisema.

Alisema nia ya kuwachukua vijana hao ni kujenga chama kama taasisi ili kisonge mbele tofauti na ilivyo sasa na siyo kujenga jina la mtu kama watu wanavyotaka iwe au wanavyodhani.

Mbowe alisema akiwa na vijana hao pamoja na viongozi wengine, walifanya kazi kama timu ili kuhakikisha wanakiingiza chama hicho Ikulu, akiamini kuwa asingeliweza peke yake kukipeleka mbele chama hicho.

Aliwataja viongozi aliowachukua kutoka katika vyama vingine vya siasa kuwa ni pamoja na Mkurugezi wa Fedha wa chama hicho, Antony Komu, Tundu Lissu, Mabere Marando ambao walitoka NCCR – Mageuzi.

Wengine ni Godbless Lema, Saidi Arfi na Mchungaji Peter Msigwa ambao walikuwa TLP na Ezekia Wenje aliyetoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa mwenyekiti wa tawi moja la chama hicho huku Mwanza.

Alisema safari ya kukijenga chama sio lelemama kwani ni sawa na treni inayotoka Dar es Salaam kuelekekea Kigoma huku akiamini wote watafiki, lakini imekuwa tofauti kwani wapo walioshuka njiani.

“Safari yetu ya Kigoma toka Dar es Salaam ilikuwa ndefu sana … wapo walioshuka katika kituo cha kwanza tu Pugu, wengine Morogogo na vituo vingine vilivyofuata na kupata vilevile lakini tutafika tu,” alisema.

Akitoa historia fupi ya maisha yake katika siasa, Mbowe alisema aliingia akiwa kijana mdogo muasisi ambaye alipata nafasi ya kukiongoza chama kama mwenyekiti wa kwanza wa vijana, baadaye kupata nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti.

Alisema aliingia katika chama hicho na kuchanguliwa kuwa kiongozi, lengo likiwa kufanya mabadiliko kwa vitendo na si kwenda kupata faida kama watu wengine wanavyofikiria.

“Lakini nilifanya kazi yangu ya kuijenga CHADEMA hatua kwa hatua kwa maana nyingine nimefanya kazi ya chama kwa miaka 23 sasa bila kulipwa mshahara wowote kwa sababu mimi ni mfanyabiashara,” alisema.

Alisema chama akitatoa maamuzi ya kumwonea mtu yeyote bali kitamhukumu mtu kutokana na makosa yake.

Post a Comment

AddThis

 
Top