0


 Ni rasimu ya pili mfumo wa Muungano

 Nape: Tusubiri tuone kitakachotokea

Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo itakabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, rasimu ya pili na ya mwisho ya katiba mpya, huku Watanzania wengi wakisubiri kwa hamu kubwa kuona inapendekeza muundo gani wa Muungano baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukataa serikali tatu.


Kwa mujibu wa Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashidi, hafla ya kukabidhi rasimu ya pili itafanyika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inachukuliwa na Tume hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, baada ya kupitia na kuchambua maboresho yaliyofanywa na mabaraza ya katiba ya wilaya ngazi ya kata kwenye rasimu ya kwanza ya katiba mpya miezi saba iliyopita.
Rasimu ya kwanza ya katiba mpya, ambayo ilijadiliwa na mabaraza ya katiba, kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Juni 4, mwaka huu.

Mambo makubwa yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya kwanza ya katiba mpya ni pamoja na mfumo wa Muungano wa serikali tatu.

Mengine ni kuruhusiwa mgombea binafsi, rais kutangazwa kushinda akipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa la sivyo uchaguzi urudiwe kwa wagombea wawili wa nafasi hiyo walioongoza kwa kura.

Mependekezo mengine yaliyopendekezwa ni tume huru ya uchaguzi, mawaziri kutokuwa wabunge, idadi ya mawaziri kutozidi 15 na spika wa bunge kutokuwa mbunge.
Pamoja na yote hayo, jambo kubwa lililopendekezwa na rasimu ya kwanza lililoishughulisha CCM ni mfumo wa Muungano wa serikali tatu.

Hali hiyo ilikifanya chama hicho Juni 10, mwaka huu, kutoa mwongozo kwa wanachama wake kuhusu rasimu ya kwanza ya katiba mpya, kikipinga mambo mengi yaliyomo ndani yake.

Kwa mujibu wa mwongozo huo ni kama vile CCM ilitaka kuendelea na katiba iliyopo, kwa kuwa inaunga mkono mambo mengi ya katiba hiyo na kupinga yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya kwanza ya katiba mpya.

Mwongozo huo ulitolewa baraka za kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, kilichofanyika mjini Dodoma, ikiwa ni siku saba tangu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoa rasimu ya kwanza ya katiba mpya.

Katika mwongozo huo CCM iliichambua Ibara ya 57-66 ya rasimu ya katiba ya kwanza inayoeleza kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu, ambao utakuwa wa shirikisho linaloundwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Tanzania Bara.

Sura hiyo pia inaeleza kuwa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano.

Katika mwongozo huo, CCM ilieleza kuwa pendekezo hilo ni tofauti na sera yake kuhusu muundo wa Muungano wenye serikali mbili, ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano na SMZ.

Mbali na kutoa mwongozo huo, Juni 11, mwaka huu, CCM ilitangaza uamuzi wake wa kuijadili rasimu ya kwanza ya katiba mpya, kuanzia ngazi ya matawi, wilaya na Taifa ili kupata maoni ya wanachama na kuweka msimamo wake.

Hata hivyo, CCM kupitia Katibu wake wa Nec, Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, ilisema maoni ambayo yangetolewa na wanachama wake yangepaswa kuzingatia maoni ya chama hicho yaliyotolewa mwanzoni mwa mchakato wa mabadiliko ya katiba.

Hata hivyo, hadi rasimu ya pili inakabidhiwa leo kwa marais hao, CCM haijawahi kuweka wazi msimamo wake kuhusu rasimu ya kwanza ya katiba mpya.

Lakini habari kutoka ndani ya kikao cha Nec, kilichofanyika mjini Dodoma, Agosti 25, mwaka huu, zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari, ambazo CCM haikuzikanusha, zilieleza kuwa michango iliyotolewa na wajumbe wa kikao hicho, wengi waling’ang’ania mfumo wa serikali mbili kama ilivyo kwenye ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya waliopinga walisema kuna haja ya kuendelea na mfumo wa serikali mbili, kwa kuwa ndio unaokubalika.

Hata hivyo, katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete alinukuliwa akiwataka wana CCM nchini, kujiandaa kisaikolojia juu ya muundo wa serikali tatu pindi Watanzania watakapoamua hivyo.

Chanzo hicho cha habari kilisema Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya Katibu wa Nec, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Dk. Asha Rose-Migiro, kuwasilisha hoja yake katika kikao hicho kilichokaa kama Baraza la Katiba. Licha ya Rais Kikwete kutoa wito huo kwa wana CCM, Oktoba 2, mwaka huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Abdallah Bulembo, aliendeleza kauli zinazoonyesha kumuingilia na kumshambulia vikali Jaji Warioba kwa kumtaka aache kuwasemea Watanzania juu ya aina ya katiba wanayoitaka.

Bulembo alimshambulia Jaji Warioba alipokuwa mkoani Tanga, wakati akihutubia moja ya mikutano ya hadhara ya wanachama wa CCM.

Bulembo alinukuliwa katika vyombo vya habari akisema kuwa siyo sahihi kwa Jaji Warioba kuwa msemaji wa Watanzania kuhusiana na mambo wanayoyataka yaingizwe ndani ya katiba.

“Jaji Warioba ni mmoja kati ya Watanzania mamilioni na kwa hali hiyo hawezi kubeba mawazo ya Watanzania wengine, ni vizuri akasimamia rasimu, badala ya kuwa msemaji wa wananchi,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa CC ya CCM.

Bulembo alitoa kauli hiyo wakati kukiwa na msuguano kati ya CCM na serikali yake kwa upande mmoja, na vyama vitatu vya upinzani vyenye wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya hapo, mwishoni mwa Septemba, mwaka huu, Jaji Warioba akizungumza na waandishi wa habari, aliwakemea baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kuiingilia mchakato wa kupata katiba mpya unaoendelea.

Alisema baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa kuendesha mabaraza ya katiba, ni kwa baadhi ya vyama vya siasa kuingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, wakiwafundisha nini cha kusema.

Jaji Warioba aliwasihi viongozi wa vyama vya siasa kuwaachia wananchi, cha kusema kwani, katiba inayotafutwa ni ya wananchi, na si ya vyama au kundi fulani.

Aidha, Oktoba 3, mwaka jana, Jaji Warioba alitoa karipio kwa Bulembo kwa kumtaka aache kupiga kelele dhidi yake kwa kuwa hakumtuma kazi ya kukusanya maoni ya katiba mpya, bali alitumwa na serikali kwa niaba ya wananchi.

Jaji Warioba alisema Bulembo amekuwa na ajenda ya siri dhidi yake (Warioba) na baadhi ya wajumbe wa Tume kwa kuwa amekuwa akiwazungumzia wao binafsi kila anaposisimama katika majukwaa ya kisiasa.

Alimtaka Bulembo kuthibitisha kuhusu kauli ambazo amekuwa akizitoa kwenye mikutano ya CCM katika mikoa ya Arusha, Tanga na Mbeya kuwa yeye (Warioba) amegeuka kuwa msemaji wa wananchi katika mchakato mzima wa kupata Katiba mpya.

Jaji Warioba alitamtahadharisha Bulembo na kumtaka kuacha kupiga kelele pamoja na kumshambulia badala yake azungumzie masuala yanayohusu rasimu ya katiba na siyo kuwajadili wajumbe.

Aidha, Jaji Warioba alimtaka Bulembo kuthibitisha kama kauli ambazo alizitoa kwa nyakati tofauti katika mikoa hiyo ametumwa na CCM ama ni kauli zake binafsi.
Jaji Warioba alisisitiza kuwa siku zote Tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa akiwamo Bulembo kujadili rasimu iliyotolewa badala ya Tume au wajumbe wake.

Alisema hakutumwa na CCM kufanya kazi anayoifanya na kwamba kazi hiyo alipewa na serikali kwa mujibu wa sheria na kwamba ataendelea kuifanya bila kusikiliza maneno yanayosemwa dhidi yake.

Jaji Warioba alisema kauli zilizotolewa na Bulembo kwa nyakati mbalimbali zilichangia mchakato wa katiba kuwa mgumu hususani wakati wananchi walipokuwa wakitoa maoni kupitia mabaraza ya katiba mkoani Mbeya.

Alisema haogopi wala hatetereki kwa kuwa anafanya kazi aliyotumwa na wananchi.
Alisema CCM iliishawasilisha maoni yake walipopewa nafasi ya kufanya hivyo, na kwamba masuala mengine yanayojitokeza zikiwamo kauli za Bulembo baada ya hapo hajui zinatoka wapi.

Mbali na Bulembo, makada mbalimbali wa CCM nchini tangu kutolewa kwa rasimu ya kwanza ya katiba walikuwa wanamshambulia Jaji Warioba binafsi kwamba ndiye anayeshinikiza mfumo wa serikali tatu kwa manufaa yake binafsi.

Wapo wanachama wa CCM na makada wa chama hicho ambao wakati wa mikutano ya mabaraza walisikika wakitoa kauli za matusi na kashfa dhidi ya Jaji Warioba kwa madai kuwa ana lengo la kuuvunja Muungano.

Ikiwa Tume leo itapendekeza mfumo wa serikali tatu, kuna uwezekano wa baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM ambao wataibuka tena nakumshambulia Jaji Warioba kutokana na maamuzi hayo.

Kama mfumo wa serikali tatu utaridhiwa tena na tume, suala hilo huenda likazua mjadala mkali na malumbano katika Bunge Maalum la Katiba ambalo CCM kina wajumbe wengi.

Kama tume itabadili msimamo wake wa awali na kutangaza mfumo wa Muungano wa serikali mbili, itakuwa imeipa CCM furaha na kicheko.

KAULI YA NAPE
Nape alipoulizwa na NIPASHE jana iwapo rasimu ya pili ya katiba mpya itapendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu CCM itachukua hatua gani, alijibu: “Kwanini tubashiri? Si usubiri kesho (leo) itokee.”

Tume ya Mabadiliko ya Katiba yenye wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar, ilitangazwa na Rais Kikwete, Aprili 6 na kuapishwa Aprili 13, mwaka jana.

Ilianza rasmi kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei mosi, mwaka jana. Baada ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Katiba.

Kazi ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia mikutano ya hadhara na ilikamilishwa na Tume Desemba, mwaka jana.

Baadaye Tume ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wakuu wastaafu na waliopo madarakani Januari 7-28, mwaka huu.

Baadaye, mabaraza ya katiba yaliipitia Rasimu ya Katiba kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2, mwaka huu na kutoa mapendekezo yake, ambayo yaliwasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume iliendelea kuyachambua kabla ya kukabidhi rasimu ya pili ya katiba kwa Rais Kikwete na Rais Dk. Shein leo.

Baada ya rasimu ya pili ya katiba mpya kukabidhiwa kwa marais hao, itachapishwa katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.
Katika kipindi hicho, Rais ataitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu ya pili ya katiba mpya iliyopendekezwa.

Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70, linatarajiwa kuanza rasmi Februari, mwakani, kwa ajili ya kujadili na kuipitisha rasimu ya pili ya katiba iliyopendekezwa.

Baada ya rasimu ya pili kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, itaitishwa kura ya maoni, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa. 

Post a Comment

AddThis

 
Top