0

Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.Charles Magaya akiongea kuhusu maadhimisho ya Mwalimu Nyerere wakati wa kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma mapema leo.Kulia kwake ni Mkurugenzi Msaidizi Bw.Athanas Kolokota na Mkurugenzi Msaidizi Thomas Manyambula (kushoto).
 


Maadhimisho ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yanatarajiwa kufanyika kitaifa kesho katika viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma.

Hayo yamesewa na Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw.Charles Magaya alipokuwa katika kikao kazi cha maandalizi ya siku hiyo mjini Dodoma.

Bw.Magaya amesema Siku ya kumuenzi Baba wa Taifa itaongozwa na mmoja wa washiriki wa Baba wa Taifa Balozi Job Lusinde. “Maadhimisho hayo yataongozwa na mmoja wa washiriki wa Baba wa Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanganyika Mheshimiwa Balozi Lusinde ambaye pia ni muasisi wa Chama cha TANU”alisema Bw.Magaya.

Sambamba na maadhimisho hayo Bw.Magaya amesema kuwa Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeandaa sinema mbalimbali za Mwalimu Nyerere zitakazoonyeshwa katika viwanja vya Nyerere Square leo kuanzia saa 12 jioni hadi saa 3 usiku. 

Aidha,amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kushiriki katika maadhimisho hayo ya kumuenzi Baba wa Taifa.

Pia Bw.Magaya ametoa wito kwa viongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Nyerere Square ili kusikiliza hotuba mbalimbali kutoka kwa viongozi waliofanya kazi karibu na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. 

Maadhimisho ya Baba wa Taifa hufanyika Oktoba 14 ya kila mwaka ambapo mada mbalimbali hutolewa na viongozi waasisi wa Taifa la Tanzania.

Post a Comment

AddThis

 
Top